RC Macha apiga ‘pini’ boda kubeba watoto kwenye tenki la mafuta

Shinyanga. Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Anamringi Macha amepiga marufuku madereva bodaboda kubeba watoto juu ya tanki la mafuta kwenye pikipiki zao.

Amesema kitendo hicho kina madhara makubwa kwa afya ya watoto na ni ukatili dhidi yao.

Macha ameyasema hayo leo Jumanne Desemba 17, 2024 kwenye hafla ya ufunguzi wa Jengo la Huduma Jumuishi (One Stop Center) lililojengwa kwa ushirikiano kati ya Serikali ya Finland na Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Idadi ya Watu (UNFPA).

“Madereva bodaboda wanawapakiza watoto mbele juu ya tanki la mafuta huku wakubwa wakikaa nyuma. Hili ni hatari kwa afya ya mtoto na ni ukatili wa wazi,” amesema Macha huku akiwataka akina mama kutambua hatari hiyo.

Kaimu Mganga wa Wilaya ya Kishapu, Faustine Mlyutu ametaja athari za kiafya za kuwabeba watoto mbele kwenye pikipiki ni pamoja na kupigwa na upepo mkali bila kinga, hali inayoweza kuwasababishia maradhi ya kupumua.

“Watoto wanaweza kupata maambukizi kwenye mapafu, hali inayosababisha ugonjwa wa ubalidi yabisi, maambukizi au magonjwa kama kifua kikuu, mafua yasiyoisha, kukohoa na kushindwa kupumua vizuri,” amesema Dk Mlyutu.

Kutokana na hali hiyo, Macha ameliagiza Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga, kuhakikisha madereva bodaboda wanaokiuka agizo hilo wanachukuliwa hatua mara moja.

Aidha, Mwakilishi Mkazi wa UNFPA, Mark Schreiner alizungumza katika hafla hiyo  amesema ili kukomesha vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto, wananchi wanapaswa kushirikiana na shirika na Serikali ya Tanzania.

“Kulingana na ripoti ya Tanzania Health Demographic Survey (THDS), asilimia 23 ya wanawake wamekumbana na ukatili wa aina mbalimbali, huku asilimia 6.01 wakiripoti ukatili wa kijinsia kati ya umri wa miaka 15 hadi 49. Serikali na wadau tunapaswa kushirikiana kuondoa hali hii,” amesema Schreiner.

Naye Dk Godfrey Kisusi, mwakilishi kutoka Huduma Jumuishi amesema jengo hilo lilianza kujengwa Agosti 2023 na kukamilika Machi 2024 kupitia mradi wa “Haki Yangu, Chaguo Langu” kwa ufadhili wa UNFPA na Serikali ya Finland kwa gharama ya Sh117 milioni.

Amesema tangu kituo kianze kazi, takwimu zinaonyesha waathirika 192 wameripoti kufanyiwa ukatili wa kingono, kimwili, kisaikolojia na utelekezaji wa watoto.

Related Posts