Sativa amlipia Lissu fomu ya uenyekiti

Dar es Salaam. Makamu Mwenyekiti wa Chadema Bara, Tundu Lissu amesema kuwa fomu ya kuwania uenyekiti wa chama hicho aliyoichukua leo imelipiwa Sh1.5 milioni na mwathirika wa tukio la kutekwa, Edgar Mwakabela, maarufu Sativa.

Mbali na Sativa, Lissu amesema pia baadhi ya wanachama wa chama hicho walishachanga fedha pia kwa ajili ya kulipia fomu hiyo.

Sativa alidaiwa kutekwa Juni 23 na watu wasiojulikana na kisha kuokotwa Juni 27 porini mkoani Katavi akiwa na majeraha kichwani.

Lissu ameyasema hayo leo Jumanne, Desemba 17, 2024 alipozungumza na waandishi wa habari baada ya kuchukua fomu hiyo.

“Amenipigia simu (Sativa) kuniambia mheshimiwa naomba nikulipie hiyo fomu na akaniambia nakulipia nikijua utafanya kazi ile ya kututetea tusitekwe tena,” amesema.

“Hii fomu italipiwa na Sativa na jukumu ambalo ameniambia Sativa ni kuhakikisha kwamba kama nitakuwa mwenyekiti niongoze mapambano ili kuwa na Tanzania mpya.”

Ameeleza iwapo atashinda nafasi hiyo, atahakikisha Tanzania inakuwa nchi yenye haki, wananchi wanainuka na kuwa na furaha.

Hata hivyo, amesema kesho anatarajia kuirejesha fomu hiyo baada ya kuijaza.

“Nimekabidhiwa fomu na Katibu Mkuu (John Mnyika) nitajaza kama inavyotakiwa na kesho nitazirudisha na kuzikabidhi tena baada ya kulipia,” amesema.

Lissu alifika katika ofisi hizo Mikocheni jijini Dar es Salaam, saa 6:20 akiwa na gari lake aina ya Land Cruiser V8.

Hakukuwa na mbwembwe za msafara wa magari ya wafuasi wake au wa chama hicho, kama ambavyo aghalabu hufanywa na wanasiasa nyakati zote.

Mwanasiasa huyo aliyekuwa amevalia shati lenye nembo ya Chadema na suruali ya jinsi, aliingia katika ofisi hizo akiwa na wasaidizi wake wanne.

“Hamjambo?” Ndiyo kauli iliyosikika kutoka katika kinywa cha Lissu baada ya kushuka kwenye gari lake, akiwasalimu wanahabari.

Moja kwa moja, aliingia hadi ofisini kwa ajili ya utaratibu wa kuchukua fomu hiyo uliochukua takriban dakika 30 kisha alitoka nje akiionyesha.

Saa 7:16 Lissu alipanda gari na kuanza kuondoka kutoka ofisini hapo, akiwa na watu walewale aliokuwa amepanda nao kwenye gari.

Aeleza tishio la usalama wake

Alipoulizwa kuhusu taarifa aliyoichapisha X kuhusu hofu ya usalama wake, amesema mmoja ya viongozi wakubwa wa nchi ndiyo waliomdokeza.

“Juzi nimetafutwa sana na mmoja wa wazee wa nchi hii, mmoja wa viongozi wa nchi hii. Viongozi sio wa kisiasa ila alinitafuta sana juzi kwa sababu ya hekaheka hakunipata,” amesema.

Amesema alipomtafuta ndipo alipomweleza juu ya kupokea taarifa kutoka kwa mtu mwingine ndani ya Serikali kuwa, kuna mpango wa kumdhuru kisha asingiziwe Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe.

“Nikamuuliza nifanyeje, akaniambia fanya lolote unaloweza lakini huyo bwana akaniambia niongeze ulinzi na niwe extra carefully (kuwa makini zaidi),” amesema.

Amesema baada ya kuruhusiwa na mtoa taarifa, ndipo amechapisha katika mitandao ya kijamii na atasambaza kwa balozi mbalimbali na vyombo vya habari vya kimataifa.

“Sitaki tena kuja kuambiwa watu wasiojulikana. Hatutaki tena wanakuja kuuwa watu waje kusema Mbowe ndiye kaua,” amesema.

Alipoulizwa iwapo amesharipoti polisi, amejibu kwa kuwa anazungumza na vyombo vya habari, bila shaka jeshi hilo linamsikia na hata Rais Samia Suluhu Hassan amemsikia.

Related Posts