Dar es Salaam. Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila amesema teknolojia ya mkaa mbadala iliyobuniwa na Shirika la Taifa la Madini (Stamico), itawezesha kupunguza matumizi ya mkaa unaotokana na kuni.
Mkaa unaotokana na kuni unatajwa kuwa na madhara mbalimbali ikiwemo upumuaji, uharibifu wa mazingira na saratani, lakini kwa mujibu wa Chalamila mkaa mbadala uliobuniwa na Stamico ni salama na umepitishwa na Shirika la Viwango Tanzania (TBS).
Chalamila ameeleza hayo leo Jumanne Desemba 17, 2024 wakati akizungumza na viongozi wa Stamico kuhusu kampeni ya matumizi ya nishati safi ya kupikia inayotokana na mkaa uliotengenezwa na taasisi hiyo kwa makaa ya mawe.
Kampeni hiyo ya Stamico itaanza Desemba 20 hadi 22, kwa lengo la kuhamasisha wakazi wa Dar es Salaam kutumia mkaa mbadala ‘rafiki briquettes’ambao hauna athari kwa afya zao, tofauti na mkaa unaotokana na kuni.
Chalamila amesema hivi sasa Serikali inahamasisha matumizi safi ya kupikia ambayo yana manufaa makubwa kwa afya za Watanzania, hivyo hatua ya Stamico kuja na teknolojia hiyo inaunga mkono kampeni ya kuhakikisha wananchi wanatumia nishati safi.
“Niwakaribishe wananchi wa Dar es Salaam kuja viwanja Zakhem Mbagala kuona mkaa huu mbadala. Huu ni mkakati wa kwanza wa kunusuru afya za Watanzania zinazoathirika kutokana na matumizi ya mkaa wa kuni,”.
“Najua mtakuwa mnajiuliza kama huu unaitwa mkaa je, hautakuwa na madhara kama ule mkaa wa kuni? Ukweli ni kwamba mkaa huu, umefanyiwa utafiti wa kutosha na umepitishwa na TBS kwamba hauna madhara,”amesema Chalamila.
Chalamila amesema Dar es Salaam, ndiyo soko la mkaa unaotokana mikoani na kuna siku aliwahi kusema hawezi kuzuia suala hilo, akifananisha hatua ni sawa na kuzuia maiti isizikwe, kwa sababu hakukua na mbadala wake ukiachana na gesi.
“Sasa hivi jibu sahihi la kweli, ni Stamico kupitia mkaa huu rafiki na unapatikana kwa gharama nafuu, sasa ni muda mzuri wa kuzuia ule mkaa unaotokana na kuni, kwa sababu mbadala wake umeshapatikana kupitia Stamico,”amesema Chalamila.
Mkurugenzi Mkuu wa Stamico, Dk Venance Mwasse amesema wameamua kuanzia kampeni hiyo Dar es Salaam, kwa sababu ni moja wapo wa mkoa unaongozwa kwa matumizi ya mkaa na kuni kwa kiwango kikubwa.
“Stamico tumekuja na teknolojia ya kuzalisha mkaa unaotokana na makaa tunayochimba Kiwila. Tulifanya utafiti wa kina na kisayansi kwa ushirikiano na taasisi mbalimbali za kiutafiti kuanzia mwaka 2018 na kujiridhisha kuwa nishati hii safi kwa matumizi ya binadamu,”
“Utafiti umeshakamilika na tumeshakabidhiwa vyeti vya ubora, uzalishaji umeshaanza kwa kiwango kikubwa maeneo ya Kisarawe (Pwani) na Kiwila. Uzalishaji mwingine utaanza Januari kule Dodoma na Tabora, tutaanza kutoka elimu kwa umma kuhusu matumizi sahihi ya mkaa huo,”amesema Mwasse.