Kibaha. Tanzania imefanikiwa kuuza bidhaa mbalimbali za viwanda kwenye nchi zaidi ya 50 duniani, hatua inayochangia kukuza uchumi wa wananchi.
Hivyo, wamiliki wa viwanda wamehimizwa kuhakikisha uzalishaji wa bidhaa zao unazingatia viwango vya kimataifa ili kulinda heshima na hadhi ya Taifa.
Kauli hiyo imetolewa leo Jumanne Desemba 17, 2024, na Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Selemani Jaffo wakati anafungua maonyesho ya nne ya viwanda, biashara na uwekezaji ya Mkoa wa Pwani, yaliyofanyika mjini Kibaha.
Waziri Jaffo amesema ni fahari kuona bidhaa za Tanzania zinakubalika na zaidi ya nchi 50 duniani na kusisitiza umuhimu wa kuendelea kupanua masoko kwa masilahi ya uchumi wa Taifa na diplomasia.
“Jambo la kujivunia kuona bidhaa za viwanda vya Tanzania zinakubalika duniani kote. Tuendelee kuheshimu viwango vya kimataifa na kufungua masoko mapya kwa mataifa mengine,” amesema Waziri Jaffo.
Waziri huyo amekiri kuwa bado kuna changamoto zinazowakabili wawekezaji wa viwanda, ikiwemo miundombinu, upatikanaji wa maji na nishati ya umeme.
Hata hivyo, amesema Serikali inaendelea kuchukua hatua madhubuti za kuboresha maeneo hayo kwa lengo la kutatua changamoto hizo haraka.
Awali, Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakari Kunenge amesema sekta ya viwanda imekuwa chachu ya maendeleo ya mkoa huo, hasa kwa kutoa ajira kwa vijana.
Naye Meneja Uhusiano wa Benki ya CRDB Kibaha, Richard Mkakala amesema benki hiyo itatumia maonyesho hayo kutoa elimu kwa wananchi kuhusu fursa za uwekezaji kupitia hati fungani ya miundombinu.
Amesema hati hiyo ya Mama Samia itawawezesha wawekezaji kupata faida ya asilimia 12, huku kiwango cha chini cha uwekezaji kikiwa Sh500,000.