Tendwa amefariki dunia akipatiwa matibabu Muhimbili

Dar es Salaam. William Tendwa mtoto wa aliyekuwa Jaji na Msajili wa Vyama vya Siasa, John Tendwa amesema baba yake amefariki saa nane usiku wa kuamkia leo, akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Taifa MuhimbilI (MNH).

Mtoto huyo wa pili wa marehemu, akizungumza na Mwananchi leo Desemba 17,2024 nyumbani kwao Kibamba jijini hapa,  amesema kwa sasa bado watoto wote wa marehemu hawajafika, hivyo wanasubiriwa ili kupanga taratibu za mazishi kifamilia.

“Kwa sasa msiba upo nyumbani kwa marehemu Kibamba hospitali, taratibu za mazishi zinaendelea kifamilia tunasubiri watoto wengine wa marehemu, lakini pia kwa upande wa Serikali zipo taratibu zinaendelea”amesema.

Hayati Jaji Tendwa kwa mujibu wa William, ameacha watoto wanane, wa kike wanne na wa kiume wanne.

Jaji Tendwa ni msajili wa vyama mstaafu ambaye alitumikia nafasi hiyo kwa miaka 13 mfululizo, akipewa kijiti na mtangulizi wake George Liundi ambaye kwa sasa ni marehemu pia.

Hayati Tendwa alianza kutumikia wadhifa huo kuanzia 2001 hadi 2013 akimuachia kijiti Jaji Francis Mutungi anayehudumu kwenye nafasi hiyo hadi sasa.

Endelea kufuatilia Mwananchi.

Related Posts