CHAMA cha Wanasheria Tanganyika (TLS), kimekosoa kauli ya Dk. Damas Ndumbaro, Waziri wa Katiba na Sheria; na kusema chama hicho kiko imara na kitaendelea kuishauri Serikali, Bunge na Mahakama katika masuala anayohusu sheria, kukosoa kwa maslahi ya umma bila woga, hofu wala upendeleo. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea)
Aidha, kimesema pamoja na kwamba TLS inaheshimu uhuru wa kila mtu kutoa maoni, kauli ya Waziri Ndumbaro haiakisi uhalisia wa utendaji wa taasisi hiyo.
Taarifa ya Baraza la uongozi la TLS, iliyosainiwa na Rais wa chama hicho, Boniface Mwabukusi, iliyotolewa Dar es Salaam leo 17 Desemba 2024, imesema TLS itaendeleza uhusiano wake na Mahakama, Serikali, Bunge, wadau wa maendeleo (DPs) na wananchi kwa ujumla kwa maslahi mapana ya Taifa.
“TLS inapenda kuwahakikishia wanachama wake na wananchi kwa ujumla kwamba, TLS iko imara na haitayumba wala kuhama kwenye misingi yake ya kisheria ya kushauri Serikali, Bunge na Mahakama katika masuala anayohusu sheria, na pale itakapolazimika, kukosoa kwa maslahi mapana ya umma na Taifa kwa ujumla bila woga, hofu wala upendeleo,” amesema Mwabukusi katika taarifa hiyo.
Chama hicho kimetoa ufafanuzi huo kufuatia kauli ya Waziri Ndumbaro aliyoitoa jana tarehe 16 Desemba, 2024 wakati wa kusaini Hati ya Makubaliano ya Ushirikiano (MoU), kati ya TLS na Wizara hiyo, ambapo pamoja na mambo mengine, Waziri Ndumbaro alisema “kama kuna kitu ambacho serikali haipendi kabisa ni yale matamko ya kukurupuka kutoka TLS.”
Mwabukusi amesema kauli hiyo ya Waziri imeleta taharuki ndani ya TLS na umma, kuhusu hadhi na heshima ambayo mawakili wameijenga kwa miaka mingi.
Amesema chama hicho kilianzishwa na Sheria ya Bunge Sura No. 307 na Majukumu yake yameainishwa kwenye kifungu cha nne (4) cha Sheria hiyo, ambayo ni kuwawakilisha, kuwalinda na kuwasaidia wanachama wa TLS katika masuala yanayohusiana na taaluma ya sheria na utendaji kazi wao; kuishauri Serikali, Bunge na Mahakama kwenye masuala yanayohusu Sheria, Katiba, Haki za Binadamu na Utawala Bora.
Amesema tangu taasisi hiyo ilipoanzishwa, imekuwa ikifanya kazi zake kwa mujibu wa taratibu, kanuni na sheria na haijawahi kukurupuka kutoa tamko.
“Matamko yamekuwa yakitotolewa baada ya kufanya utafiti wa kina na kujiridhisha kwamba kuna taratibu, kanuni na sheria zilizokiukwa na mamlaka husika au wadau mbalimbali,” amefafanua Mwabukusi.
Amesema miongoni mwa matamko ya hivi karibuni ya TLS ni lile la kupinga wanachi wa Ngorongoro kuhamishwa kinyume na Sheria pamoja na kukemea utekaji na mauaji ambayo yamekuwa yakifanywa kwa Wananchi.
“Baada ya matamko hayo ya TLS, wananchi wa Vijiji vya Ngorongoro wameendelea kuwa kwenye maeneo yao na hata Polisi wamekuwa wakijitokeza mara kwa mara kutoa ufafanuzi kwa umma kuhusu matukio ya utekaji na mauaji, kitu ambacho awali Polisi walikuwa hawafanyi hapo kabla, jambo ambalo limepunguza hofu na wasiwasi kwa umma,” amesema.
Amesema chama hicho kitaendelea kutoa matamko na kitatumia njia zote muhimu, katika kutekeleza majukumu na kwamba kitafanya hivyo kwa weledi kutegemeana na changamoto husika au jambo litakalohitaji kauli, ushauria au uwajibikaji kutokaTLS.
Kuhusu gari ambalo TLS imepewa na Serikali, amesema linabakia kuwa mali ya serikali na kwamba litatumiwa na chama hicho kutekeleza majukumu ya kutoa huduma kwa kijamii hususan msaada wa kisheria na masuala ya uragibishi.