Trump aahidi tena kumaliza “mauaji” ya vita vya Ukraine – DW – 17.12.2024

Akizungumza kwa mara ya kwanza na waandishi habari tangu alipochaguliwa kwa mara nyingine kuwa rais wa Marekani, Trump amesema ni lazima mauaji yanayotakana na vita hivyo yakomeshwe, akiahidi kwa mara nyingine kuumaliza mzozo huo atakapoingia madarakani.

“Tutazungumza na Rais Putin, na tutazungumza na wawakilishi, Zelensky na wawakilihsi wa Ukraine,” amesema Trump kwenye mkutano huo ba waandishi habari uliofanyika kwenye makaazi yake huko Florida.

“Ni lazima tukomeshe (vita), ni mauaji yasiyoelezeka,” amesema kiongozi huyo atakayeapishwa kuchukua hatamu za uongozi mnamo Januari 20 mwaka ujao.

Trump mara kadhaa amedai kuwa na uwezo wa kumaliza mzozo wa Ukraine haraka lakini hadi sasa hajaweka wazi hadharani mkakati wake wa kufanya hivyo.

Hivi karibuni alitoa mwito wa kushitishwa mara moja kwa mapigano na akasema “mazungumzo yanapaswa kuanza haraka.”

Trump alikutana na Zelensky katika mkutano ulioandaliwa na Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa mwezi huu, baada ya kiongozi huyo wa Ukraine kusema kwamba serikali yake inatafuta “aamni ya kudumu” na “uhakika wa usalama.”

Poland, mshirika muhimu na taifa jirani ya Ukraine, imesema siku ya Jumatatu kwambua utawala mjini Kyiv haupaswi “kulazimishwa” kufanya mazungumzo ya amani. Waziri wake wa mambo ya nje Radoslaw Sikorski  amejenga hoja kwamba “upande uloanzisha uchokozi na siye upande unaoonewa ndiyo unapaswa kulazimishwa” kufanya mazungumzo.

Trump akosoa uamuzi wa Ukraine kuruhusiwa kushambulia ndani ya Urusi kwa makombora ya Marekani 

Macron, Trump na Zelensky
Donald Trump alipokutana na Rais Zelensky wa Ukraine na Emmanuel Macron wa Ufaransa.Picha: Sarah Meyssonnier/AFP

Katika suala jingine, Trump aliashiria kwamba anaweza kutengua uamuzi wa hivi karibuni wa Rais Joe Biden wa kuruhusu vikosi vya Ukraine kutumia silaha za masafa marefu za Marekani kulenga maeneo ya ndani zaidi ya Urusi.

Kwenye mkutano na waandishi habari, Trump ameuita uamuzi uliotolewa na Biden mwezi uliopita “kuwa ni wa kijinga.” Pia ameonesha kukasirishwa kwamba serikali yake inayokuja haikushirikishwa kabla ya Biden kutangaza uamuzi ho.

Matamshi yake ameyatoa wakati Rais Vladimir Putin wa Urusi amesifu mafanikio ya jeshi lake kwenye vita nchini Ukraine akiutaja mwaka unaomalizika kuwa wa “kihistoria”.

Akiwahutubia viongozi wa ngazi ya juu wa kijeshi jana jumatatu, Putin amesema jeshi la nchi hiyo linao udhibiti mkubwa kwenye uwanja wa mapambano.

Duru kutoka uwanja wa vita zinasema vikosi vya Urusi vimesonga mbele kwa kasi kubwa mnamo wiki za hivi karibuni na vinaukaribia mji muhimu wa mashariki mwa Ukraine wa Pokrovsk.

Related Posts