Na Mwandishi wetu, Simanjiro
WANAFUNZI wanne wa shule ya awali na msingi ya mchepuo wa kiingereza Glisten English Medium primary school iliyopo kwenye Kata ya Endiamtu Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, hivyo kuwa shule iliyoongoza kiwilaya.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Waziri wa TAMISEMI, Mohamed Mchengerwa akitangaza majina ya wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na shule mbalimbali za sekondari nchini, shule za Simanjiro zimetoa wanafunzi wawili au mmoja kujiunga na shule za bweni.
Shule ya Glisten inayomilikiwa na mfanyabiashara maarufu wa jijini Arusha na mchimbaji maarufu wa madini ya Tanzanite wa mji mdogo wa Mirerani Justin Nyari imetoa wanafunzi wanne kati ya wanafunzi 36 waliohitimu darasa la saba, hivyo kuongoza kiwilaya.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo ya Waziri Mchengerwa, mwanafunzi kutoka shule ya Glisten, Martha Laizer amechaguliwa kujiunga shule ya sekondari ya vipaji maalum ya Msalato iliyopo jijini Dodoma.
Mwanafunzi mwingine wa shule hiyo, Eliya Kirina amechaguliwa kwenda shule ya sekondari Kilosa iliyopo mkoani Morogoro.
Mwanafunzi mwingine wa shule ya Glisten, Veronica Kimambo amechaguliwa kwenda kujiunga na shule ya sekondari Dkt Samia Suluhu Hassan Girls iliyopo jijini Dodoma.
Kwa upande wake mwanafunzi mwingine wa shule hiyo, Radhia Msuya amechaguliwa kwenda shule ya sekondari ya wasichana ya Manyara iliyopo mjini Babati.
Hata hivyo, wanafunzi wengine 32 wa shule hiyo wamepangiwa kuanza masomo yao kwenye shule ya sekondari Tanzanite iliyopo mji mdogo wa Mirerani wilayani Simanjiro.
Kwa upande wake, mwalimu mkuu wa shule hiyo, Kennedy Omondi amesema wanafunzi wake wanastahili pongezi kwani wakati wanafanya mitihani kulikuwa na matukio yasiyo mazuri kutokana na ulinzi mkali uliokuwepo eneo hilo.
“Wanafunzi wetu walihofia kuona askari wenye silaha na wasimamizi kubadilishwa ghafla ila tukawajenga kisaikolojia kuwa wasiogope hivyo wafanye mitihani yao vyema kama walivyofundishwa miaka yote saba ,” amesema Omondi.
Amesema wanafunzi hao waliopangiwa shule za vipaji na bweni wameanza kusoma elimu ya awali (baby class) kwenye shule hiyo hivyo wamestahili kupata kilicho bora ndiyo sababu wamefaulu vyema na kupangiwa shule hizo.
Mmoja kati ya wazazi wenye watoto katika shule hiyo Shaban Masanja amesema usimamizi mzuri wa mkurugenzi wa Glisten, Justin Nyari umesababisha matokeo hayo mazuri
“Mkurugenzi Nyari huwa anawafuatulia na kuwasimamia vyema walimu kwani muda wa masomo yeye anahakikisha walimu wanakuwa darasani na wanafunzi wanafanya mitihani mingi ya majaribio,” amesema Masanja.