Dar es Salaam. Siku chache baada ya kuzinduliwa kwa rasimu ya dira ya Taifa 2050, Mtandao wa Wanawake na Dira umetoa mapendekezo 10 waliyotaka yapewe msisitizo katika miaka 25 ijayo.
Wanawake hao wametoa maoni yao jana Desemba 16, 2024 mbele ya Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Stanslaus Nyongo aliyeambatana na wataalamu na waandishi wa dira ya Taifa 2050.
Mjumbe wa mtandao huo ambaye pia ni Mkurugenzi wa Mfuko wa Wanawake Tanzania (WFT), amesema dira hiyo inapaswa kuonyesha kwa msisitizo nini kinafanyika kutokomeza vifo vinavyotokana na uzazi.
“Tunataka dira iseme wazi kwa sababu zozote zile kusiwe na mwanamke hata mmoja anayepoteza maisha yake anapozalisha rasilimali watu. Vifo vya wanawake kutokana na uzazi bado ni vingi na inakatisha tamaa hivyo tunataka inapofika 2050 tunataka iwe historia,” amesema.
Pendekezo lingine lililotolewa na mjumbe wa mtandao huo, Profesa Ruth Meena ni mwelekeo wa nchi katika kukabiliana na idadi kubwa ya watu kuwa kwenye uchumi usio rasmi.
Amesema, “Hatuwezi kuwa na jamii ambayo zaidi ya asilimia 60 ya watu wanakuwa kwenye uchumi usio rasmi. Hapa ndio wapo wanawake wengi na wanakutana na changamoto kadha wa kadha kwenye hizo shughuli zao.
“Tunataka uwekwe mkazo wa kukabiliana na vikwazo vinavyowafanya wanawake wengi kuwa kwenye uchumi usio rasmi.”
Kwenye sekta ya utalii, Profesa Ruth amesema licha ya sekta hiyo kukua, ukuaji wake unapaswa kwenda sambamba na maendeleo ya kijinsia.
“Wanawake bado hawana uwezo wa kushika nafasi kubwa kwenye sekta na kumiliki kampuni za utalii, wengi wanaishia kufanya kazi za chini malipo yao ni madogo hivyo wanaishia kutegemea huruma za wateja ambayo wakati mwingine inawaweka hatarini,” amesema.
Eneo lingine aliloshauri ni dira kutoa mwelekeo wa huduma rasmi za kifedha kushushwa chini hasa kwa wanawake ili kuwaondoa kwenye hatari ya mikopo umiza.
“Tusifungie macho hili la wanawake kuchukua mikopo ya kausha damu. Wanawake wanajiona hawana sifa za kwenda kwenye taasisi rasmi za kifedha. Hapa tunataka huduma za kifedha zirahisishwe ili kuzifikia”.
Mjumbe mwingine wa jukwaa hilo ambaye pia ni Mkurugenzi wa Shirika la Mshichana Initiative, Rebeca Gyumi amesema suala la usalama na amani linapaswa kufafanuliwa kwa mapana.
“Unapozungumza amani ni zaidi ya kukosekana vita. Hili suala liwekwe vizuri. Amani inaanza nyumbani, sasa kama tutakuwa na jamii ambayo ina watu wanaofanyiana ukatili ni vigumu uchumi kukua.
“Kwa sasa mtoto akitoweka kwa dakika 10 unaanza kuwa na wasiwasi, hivyo tunapozungumzia suala la amani tuanzie kwenye ngazi ya kaya. Dhana ya usalama kama nchi tuitoe kwenye vifaru na silaha tuangalie namna gani nchi yetu inaweza kujilinda kimtandao,” amesema Rebeca.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Ulingo, Dk Avemaria Semakafu amesema dira hiyo inapaswa kuwa msisitizo Tanzania ni Taifa lisilovumilia utamaduni unaoendekeza aina zote za rushwa ikiwemo ya ngono.
Dk Semakafu ambaye aliwahi pia kuwa naibu katibu mkuu wizara ya elimu amesema msisitizo mwingine unapaswa kuwekwa katika kuhakikisha shule na maeneo mengine yote yanayotoa elimu kuwa mahali salama kwa watoto wote wa kike na wa kiume.
Pendekezo la Mkurugenzi wa shirika la Wajiki, Janeth Mawiza limejielekeza kwenye upatikanaji wa huduma za afya akitaka Serikali kuondoa matabaka hasa kwenye mfumo wa bima ya afya.
“Inapofika kwenye suala la afya wanawake tunakutana na changamoto nyingi pale tunapohitaji matibabu. Ikumbukwe kwamba kundi hili kwa kiasi kikubwa halina uhakika wa kipato chake hivyo tunahitaji kuwepo na mifumo thabiti itakayowezesha upatikanaji wa huduma za afya.”
Naye Mkurugenzi wa Chama cha Wanawake katika Sheria (Wildaf), Anna Kulaya amesema utekelezaji wa dira hiyo utafanikiwa endapo utafanyika uwekezaji mkubwa kwa wanawake.
Akizungumza mara baada ya kusikiliza maoni hayo, Nyongo amesema Serikali inatambua mchango mkubwa unaotolewa na wanawake hivyo itayafanyia kazi mapendekezo yaliyotolewa na kundi hilo.
Amesema kama ambavyo imefanyika kwa makundi mengine ikiwemo vyama vya siasa kupata nafasi ya kutoa maoni baada ya rasimu kutoka, vivyo hivyo imefanyika kwa kundi hilo la wanawake linalogusa masilahi mapana ya jamii.
“Mara ya kwanza mlitoa maoni tukayaingiza kwenye rasimu, tumerudi tena baada ya rasimu kutoka tuwasikilize kama kuna yaliyoachwa ili tuweke sawa na kuhakikisha mapendekezo yenu yanakuwa sehemu ya dira ya Taifa.
“Tunatambua umuhimu na mchango wa wanawake ndiyo maana timu ya wataalamu na waandishi wa dira imeyapokea yote mliyoyasema inakwenda kuyachakata na bado tutapokea hata mapendekezo mengine mkiyaleta kwa maandishi,” ameahidi Nyongo.