Wataalamu wa Ununuzi na Ugavi wametakiwa kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu na kufanya kazi kwa kuzingatia sheria, kanuni na miongozo mbalimbali inayosimamia kada ya Ununuzi na Ugavi nchini.
Akizungumza katika ufunguzi wa kongamano la 15 la Wataalamu wa Ununuzi na Ugavi nchini linalofanyika katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano (AICC) Jijini Arusha, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko, amewataka Wataalamu hao kuzitendea haki taaluma zao kwa kufanya kazi kwa uadilifu ili kuhakikisha sekta ya ununuzi na ugavi inawatoa watu kwenye umasikini.
Mhe. Dkt. Biteko alisema kuwa Sekta ya Ununuzi na Ugavi ndio eneo pekee linalochukua takribani asilimia 70 ya Bajeti ya Serikali, hivyo uadilifu pekee ndio utakaosaidia fedha kutumika kwa malengo yaliyokusudiwa hasa katika kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Aidha, Dkt. Biteko aliwaasa Wataalamu hao kuzingatia na kuyaishi yale yaliyopo kwenye sheria za manunuzi kwa kufanya kazi yenye tija, uwazi na kujiepusha na vitendo vya rushwa kwenye masuala yote ya manunuzi ya Umma.
‘’Serikali iliamua kuanzisha sheria ya manunuzi ili kuwa na manunuzi yenye tija, kupata bidhaa zenye ubora na wakati, na kuondoa mianya ya rushwa., hivyo naomba mkutano huu uzingatie yale yanayotafsiriwa kwenye sheria hiyo’’alisema Mhe. Dkt. Biteko.
Mhe Biteko aliipongeza Bodi ya Usimamizi wa Ununuzi na Ugavi (PSPTB), kwa hatua mbalimbali inazochukua hasa kwa wale wanaoenda kinyume na maadili ya sekta hiyo na kusisitiza kuwa Serikali kupitia bodi hiyo haitasita kuwachukulia hatua kali watumishi ambao watashindwa kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia sheria zilizopo.
Awali akimkaribisha Naibu Waziri Mkuu, Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Hamad Hassan Chande (Mb), alisema kuwa Wizara ya Fedha imeendelea kuwapa thamani na kutoa kipaumbele kwa wataalamu wa ununuzi na ugavi ili kuhakikisha wanafanya vizuri katika eneo lao la kazi ili kukuza uchumi.
‘’Kupitia Sheria ya Ununuzi wa Umma, Sura 410 tumewapa hadhi ya kuwa Wakurugenzi, Mameneja n.k kwa kuzingatia ukubwa wa Taasisi nunuzi na hivi sasa, Wizara inaendelea na jitihada za kurekebisha Muundo wa Vitengo vya Ununuzi na Ugavi ili kuwezesha utekelezaji wa majukumu kwa ufanisi’’ alisema Mhe. Chande.
Kongamano la Wataalamu wa Ununuzi na Ugavi ambalo lilikuwa na kauli mbiu ya Mabadiliko ya Ununuzi na Ugavi kwa Usimamizi Bora wa Rasilimali linafanyika kila mwaka kwa lengo la kutoa fursa kwa Bodi ya Usimamizi wa Ununuzi na Ugavi kukutana na wataalamu wake pamoja na wadau wa mnyororo wa ununuzi na ugavi, ili kujadiliana kwa pamoja jinsi ya kuboresha utendaji kazi katika mnyororo mzima wa ununuzi nchini.