Unguja. Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Utumishi Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali Zanzibar (CAG), Dk Idrissa Muslim Hija amewataka watumishi wa ofisi hiyo wanapofanya kazi ya ukaguzi kuwaelekezaji badala ya kukemea.
Ametoa kauli hiyo leo Desemba 17, 2024 wakati akifungua mkutano mkuu wa ofisi hiyo ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya wiki ya ukaguzi kisiwani hapo, amesema wakati mwingi yapo yanayofanyika kwa nia njema ila kwa sababu ya uelewa au kukiuka taratibu inaweza kuonekana mtu kafanya vibaya.
“Tunapowakagua watendaji tuwe waelekezaji zaidi badala ya kuwakemea, tunafanya kazi na watu ambao wengi wetu wana malengo mazuri ya kuendeleza nchi yetu,” amesema
Ametumia fursa hiyo kuwataka wawe na lugha nzuri kwa wanaowakagua, “lugha nzuri ni kitu muhimu sana, ila kwa kukosa usipoitumia unashindwa kupata unachokitaka kwa sababu ya kutumia lugha yenye ukakasi.”
Mbali na kuwataka kuwa waelekezaji na kutumia lugha ya stara, kadhalika amewataka watendaji hao kuwa wabunifu, waadilifu na kujifunza mbinu mpya katika utendaji kazi ili kuleta ufanisi wa kuimarisha rasilimali za umma.
“Weledi katika kazi hii ya ukaguzi ni muhimu sana hasa katika kuwasilisha yale ambayo umeyafanyia kazi kwa wale mnaowakagua na ngazi mnayopeleka ripoti hiyo,” amesema
Amesema kazi za udhibiti zitasababisha mafanikio na uwajibikaji na hatimaye kuleta tija kwa wananchi ikiwamo kuchochea utoaji wa huduma za jamii.
Naibu CAG, Khamis Juma amesema
awali walikuwa na programu ya siku ya ukaguzi sasa wameona waende mbali wawe na wiki ya ukaguzi kutambulisha ofisi zaidi kitaifa na kimataifa.
Amesema katika wiki ya ukaguzi wanafanya shughuli mbalimbali zikiwamo kuwatembelea watoto wenye mahitaji, wazee na kufanya usafi na kutoa elimu kwa jamii ikiwa ni sehemu ya kutambulisha zaidi ofisi hiyo na majukumu yake.