Watoto wawili wadaiwa kujinyonga Tabora, sababu zatajwa

Tabora. Watoto wawili mkoani Tabora wanadaiwa kufa kwa kujinyonga katika matukio tofauti, akiwemo mwanafunzi wa darasa pili shule ya msingi Igunga anayedaiwa kukutwa amejinyonga juu ya mti wa mwembe karibu na nyumba wanayoishi.

Akielezea matukio hayo leo Jumatatu, Desemba 16, 2024, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Richard Abwao amesema jana, Desemba 15, saa 12 jioni, Mtaa wa Gengeni uliopo Manispaa ya Tabora, Ramadhan Sabayi (10) ambaye ni mwanafunzi alikutwa amejinyonga juu ya mti wa mwembe karibu na nyumba wanayoishi.

“Huyu alikuwa akiishi kwa mama yake mdogo na wakati anajinyonga alitumia kamba iliyotokana na mfuko wa saruji. Marehemu akiwa kwa mama yake mzazi Wilaya ya Igunga aliwahi kufanya majaribio ya kujiua mara mbili na hata alipokutwa akitaka kufanya majaribio hayo na kuhojiwa, alisema amekuwa akifanya hivyo bila kujitambua,” amesema Abwao.

Katika tukio jingine, Kamanda Abwao amesema leo Desemba 16, saa 12 asubuhi, mtaa na kata ya Mpera, Manispaa ya Tabora, imebainika mtoto Gilson Charles (13) amejinyonga mbele ya nyumba wanayoishi.

“Leo asubuhi tumepata taarifa kutoka kwa mzazi aliyegundua kuwa mtoto wake, Gilson amejinyonga kwa kutumia kamba ya chandarua ambayo aliitundika kwenye mti uliopo nje ya nyumba yao,” amesema Abwao na kuongeza:

“Marehemu alikuwa amemaliza darasa la saba mwaka huu katika shule ya msingi Ipuli, sababu za kifo ni mtoto kugombezwa na mama yake kutokana na kutowapikia wadogo zake na kutofanya usafi wa nyumba. Alitoweka nyumbani hadi alipogundulika akiwa amejinyonga nje ya nyumba yao.”

Mdogo wa marehemu, Erick Charles amesema kaka yao aliagizwa na mama yao awapikie chakula, kwani alikuwa akielekea kazini, baada ya kupewa maagizo hayo, kaka yao alikula chakula chote kilichobaki usiku na aliposhiba aliondoka.

Ameeleza mama yao aliporudi nyumbani jioni alikuta hawajala na kaka yao aliporudi usiku alikataa kuingia ndani akihofia kuchapwa na mama yao, ndipo alipotokomea kabla ya kukutwa amefariki dunia kwa kujinyonga.

Mjumbe wa serikali ya mtaa wa Mpera, Mwanaid Maulidi amesema alipokea taarifa za kifo cha mtoto huyo kutoka kwa mwenyekiti wake aliyekuwa safari.

“Nilipokea simu ya mwenyekiti wetu wa mtaa akiniomba nifike hapa panaitwa Kwa Wambura kwamba kuna mtoto amejinyonga, kweli baada ya kufika nikaona hali hiyo, tumesikitika kwa kuwa ni tukio ambalo hatukulitarajia.

“Natoa wito kwa wazazi kuwalea watoto katika maadili mema ili uepukana na haya yanatokea kwenye familia zetu,” amesema.

Mwanaidi amesema kwa mujibu wa wazazi wa marehemu, mtoto huyo alitarajiwa kujiunga na kidato cha kwanza mwaka 2025 na ndoto yake kubwa ilikuwa awe daktari.

Related Posts