WAZIRI KOMBO AWASILI NCHINI ETHIOPIA KWA ZIARA YA KIKAZI

Waziri
wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud
Thabit Kombo (Mb.) tarehe 16 Desemba, 2024 amewasili jijini Addis Ababa,
Ethiopia kwa ziara ya kikazi ya siku tatu kuanzia tarehe 16 hadi 18
Desemba, 2024 na kupokelewa na Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
nchini Ethiopia, Mhe. Innocent Shiyo katika ofisi za ubalozi huo.

Baada
ya kuwasili Mhe. Kombo alifanya kikao kazi na watumishi wa Ubalozi huo
pamoja na Ujumbe wa Tanzania unaoshiriki Mkutano wa Kwanza wa Tume ya
Pamoja ya Mawaziri (JMC) kati ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na
Jamhuri ya Shirikisho la Ethiopia unaotarajiwa kufanyika tarehe 17
Desemba, 2024 jijini Addis Ababa.

Waziri Kombo anatarajiwa
kuongoza ujumbe wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika mkutano huo wa
JMC akiwa ameambatana na Waziri wa Uchukuzi, Mhe. Prof. Makame Mbarawa
(Mb.) ambapo pamoja na masuala mengine mkutano huo unatarajiwa kujadili
utekelezaji wa maeneo mbalimbali ya ushirikiano yaliyokubaliwa na nchi
hizo mbili ikiwemo masuala ya ulinzi na usalama, diplomasia, afya, maji,
elimu, fedha, mifugo na uvuvi, kilimo, biashara na uwekezaji, viwanda,
nishati, ushiririkiano katika sekta ya anga na michezo, Sanaa na
utamaduni.

Mkutano wa Mawaziri ulitanguliwa na Mkutano wa ngazi
ya Maafisa Waandamizi uliofanyika tarehe 16 Desemba, 2024 ambapo ulikuwa
na jukumu la kupitia nyaraka mbalimbali ikiwa ni sehemu ya maandalizi
ya mkutano huo muhimu wenye lengo la kukuza ushirikiano wa kimaendeleo
kwa maslahi ya pande zote mbili.

 

Related Posts