Wenyeviti wa Vijiji na Vitongoji 601 kutoka kwenye kata 20,vijiji 93 halmashauri ya Mtama Mkoani Lindi wamepatiwa mafunzo maalum ya uongozi bora yenye lengo la kuwajengea uwezo katika kutekeleza majukumu yao ya kuwatumikia wananchi.
Mafunzo hayo yanayotolewa na Ofisi ya Rais Tamisemi kwa kushirikiana na wakufunzi kutoka Chuo cha Serikali za Mitaa cha Jijini Dodoma yanafanyika kwa siku mbili kuanzia Desemba 16 hadi 17,katika Shule ya Sekondari Nyangao.
Akizungumza katika ufunguzi wa mafunzo hayo,Mkuu wa Wilaya ya Lindi Victoria Mwanziva amewasisitiza viongozi hao kuzingatia mafunzo ili wakatimize wajibu wao wa kutumikia wananchi kwa uadilifu wakifuata misingi, kanuni na taratibu zote za uongozi bora na hatiamaye kutimiza adhma ya Rais Dkt. Samia yakufikisha huduma bora kwa wananchi.
Amemsisitiza Mkurugenzi wa halmashauri ya Mtama Underson Msumba kuhakikisha viongozi hao wanakwenda kufanya kazi bila kupata urasimu wowote na waweke utaratibu mzuri wa kuwapa taarifa juu ya Miradi na mapokeo yote ya fedha zinazopelekwa kwenye maeneo yao kwani wao ndio wahamasishaji wazuri wa wananchi katika kushiriki shughuli mbalimbali za kujitolea.
Awali, Afisa uchaguzi wa halmashauri ya Mtama Alphonce Ngongi kwa niaba ya Mkurugenzi wa halmashauri hiyo ameeleza kuwa matarajio yao baada ya mafunzo hayo,wenyeviti hao watakuwa na maarifa ya kutosha katika kuongoza wananchi ambao wanamatarajio ya kupata mabadiliko makubwa kutoka kwao.
Kwa upande Mwakilishi kutoka Ofisi ya Rais Tamisemi Joseph Bengesy amebainisha kuwa mafunzo hayo ni kwaajili ya kuwakumbusha maadili ya uongozi na utumishi wa umma ikiwemo utunzaji wa siri za serikali,sheria za uendeshaji wa Mamlaka za Serikali za Mitaa,majukumu na Madaraka ya vijiji,na Vitongoji, uongozi na utawala bora huku baadhi ya wenyeviti waliopatiwa mafunzo wakishukuru kwa mafunzo hayo kwakisema yatawasaidia kujua majukumu yao hasa wale wapya ambao wameingia kwenye nafasi hizo kwa mara ya kwanza.