YANGA wanapambana kuhakikisha wanatimiza matakwa ya kocha mkuu wa kikosi hicho, Sead Ramovic ambaye ameagiza kufanyika maboresho kadhaa katika kipindi hiki cha usajili wa dirisha dogo akitaja maeneo yanayotakiwa kuongezwa nguvu.
Kati ya maeneo hayo ni beki ya kushoto na kulia ambako tayari amesajiliwa Israel Mwenda kwa mkopo akitokea Singida Black Stars.
Pia anahitajika beki wa kati, kiungo mkabaji, winga ya kushoto na mshambuliaji.
Katika kuanza na mikakati hiyo, haraka Yanga ilitua Coastal Union kuulizia uwezekano wa kuinasa saini ya beki Lameck Lawi ambaye Juni mwaka huu alitambulishwa ndani ya kikosi cha Simba lakini alishindwa kuitumikia timu hiyo kutokana na kile kilichoelezwa ni kutofuatwa utaratibu ipasavyo.
Hata hivyo, dili la Lawi kutua Yanga ni kama limekuwa na ugumu ndio mabosi wa timu hiyo wameamua kuhamishia nguvu kwa beki Mzenji, Laurian Makame anayeitumikia Fountain Gate.
Chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya Yanga, kimeliambia Mwanaspoti kuwa baada ya dili la Lawi kuingia ugumu, viongozi wameweka nguvu Fountain Gate ili kumpata Makame ambaye amekuwa nguzo muhimu ndani ya kikosi hicho kilichoweka ngome yake Manyara ikiutumia Uwanja wa Tanzanite Kwaraa.
“Ni kweli ishu ya Lawi imekuwa ngumu na muda unakwenda baada ya dirisha la usajili kufunguliwa, sasa tumeamua kufanya jitihada za kumnasa Makame ambaye pia ameonyesha uwezo wa kufanya vizuri akiwa mchezaji kiongozi wa Fountain Gate,” alisema na kuongeza;
“Mchakato wa mazungumzo unaendelea vizuri na tunaamini endapo tutafanikiwa kunasa saini ya mchezaji huyo tutakuwa tumepunguza presha kubwa iliyopo kwenye eneo hilo ambalo tumekuwa tukimtumia zaidi Dickson Job na Ibrahim Hamad ‘Bacca’ sambamba na nahodha Bakari Mwamnyeto.”
Endapo Yanga itafanikiwa kunasa saini ya beki huyo mzawa, wataongeza idadi ya walinzi wa kati katika kikosi hicho kufikia wanne na kuwa na uwanda mpana kumtumia mchezaji wanayemtaka kulingana na mahitaji ya benchi la ufundi na aina ya mpinzani wanayekwenda kukabiliana naye.
Mabingwa hao watetezi tayari wana nahodha Mwamnyeto, Job na ‘Bacca’ ambao kiasili ni mabeki wa kati huku wakilazimika kumtumia Aziz Andabwile kucheza eneo hilo licha ya kwamba yeye ni kiungo mkabaji.
Hata hivyo, wakati Yanga wakipambana kunasa saini ya beki huyo, inaelezwa kuwa Azam FC pia wanampigia hesabu. Inaelezwa kuwa matajiri hao wa Jiji la Dar es Salaam, nao wametuma ofa Fountain Gate kuangalia uwezekano wa kumpata beki huyo ili aende kusaidiana na Yeison Fuentes ambaye kwa sasa anacheza pacha na Yoro Diaby.
Rafiki wa karibu wa mchezaji huyo, aliliambia Mwanaspoti kuwa ni kweli Makame amepokea ofa kutoka timu hizo mbili na mazungumzo kati ya pande mbili yanaendelea.
Mwanaspoti lilifanya jitihada za kumtafuta Makame kuzungumzia dili hilo ambapo alisema yeye bado ni mchezaji wa Fountain Gate na kama kuna ofa wao ndio wanatakiwa kutolea ufafanuzi.
“Mimi kazi yangu ni kucheza na naweza kucheza timu yoyote kama mkataba utakavyokuwa unanitaka, kuhusiana na ofa hilo siwezi kulizungumzia, ninauachia uongozi wangu na kama kweli kuna uhitaji kwa hizo timu wanatakiwa kufuata utaratibu kwa kufanya mazungumzo na Fountain Gate,” alisema Makame.
Ipo hivi; Simba wameweka ngumu juu ya Lawi kwenda Yanga baada ya hivi karibuni kuibua kesi ya mchezaji huyo ambaye ndiye alikuwa wa kwanza kutambulishwa kwenye kikosi cha Msimbazi lakini mambo yakabadilika baada ya Coastal kuigomea na kusema kuwa bado ni mchezaji wao.
Lawi msimu uliomalizika aliichezea Coastal Union na akauzwa kwa Simba, lakini wamiliki wake hao walirejesha fedha kwa madai muda wa malipo waliowekeana ulimalizika, jambo ambalo lilizua utata.
Sakata hilo lilikuwa chini ya Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), ambayo iliamua kumuacha Lawi kuendelea kuitumikia Coastal Union hadi sasa ambapo dirisha dogo la usajili lililofunguliwa Desemba 15 likimuibua tena na kumuhusisha na Yanga.
Baada ya Simba kuibua tena kesi hiyo, Kamati imeamuru klabu hiyo na Coastal Union kukaa tena mezani kumalizana.
Novemba mwaka huu, Mwanaspoti lilikuhabarisha kwamba Yanga inamfukuzia mshambuliaji raia wa Uganda, Fahad Bayo ili kuimarisha eneo hilo.
Taarifa mpya ni kwamba, Bayo mwenye umri wa miaka 26 ambaye alikuwa akifanya mazoezi na kikosi hicho, inaripotiwa tayari amesaini mkataba wa miaka miwili.
Bayo anajiunga na Yanga akiwa ni mchezaji huru baada ya kuachana na MFK Vyskov inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza nchini Czech ambayo aliichezea mechi 42 na kuifungia mabao manane.
Kabla ya kujiunga na Vyskov, Bayo aliitumuikia Ashdod inayoshiriki Ligi Kuu ya Israel ambayo katika mechi 41 alizoichezea, alifunga mabao manane pia akitoa asisti moja.
Katika timu ya taifa ya Uganda, mshambuliaji huyo amecheza mechi 21 na kuhusika na mabao tisa, akifunga mabao manane na kutoa asisti moja.
Ni mchezaji mwenye uzoefu kutokana na idadi kubwa ya klabu alizowahi kuzichezea ndani ya nje ya Afrika ambazo ni MFK Vyskov, FC Ashdod, Bnehi Sakhnin, Buildcom FC, Vipers na Proline.
Usajili huo unaweza kumchomoa straika mmoja kikosini hapo ambapo jina la Jean Baleke likitajwa zaidi kwani ndiye aliyekuwa hana nafasi kubwa ya kucheza tofauti na Prince Dube, Clement Mzize na Kennedy Musonda, huku pia nyota huyo wa zamani wa Simba akihusishwa na mipango ya kutua Namungo.