SIMBA imeanza safari ya kurejea juu ya msimamo baada ya kuichapa timu ya mkiani ya Ken Gold kwa mabao 2-0, shukrani kwa mabao mawili ya mipira ya kutengwa, kisha wekundu hao kuhama kutoka nafasi ya tatu mpaka ya pili kwenye msimamo.
Ushindi huo wa Simba unaifanya kufikisha pointi 31, mbili tu nyuma ya vinara wa Ligi Azam wenye pointi 33, lakini Mnyama akiwa na mechi tatu mkononi akiendelea kupunguza viporo vyake.
DK 11 MABAO MAWILI
Ushindi wa Simba ulitengenezwa kipindi cha kwanza wekundu hao wakitumia dakika 11 kupika mabao yao ambapo dakika 35 ilitangulia kupata bao kwa mkwaju wa penalti ya Lionel Ateba iliyotokana na kiungo wake Awesu Awesu kuangushwa ndani ya eneo la hatari na beki wa Ken Gold.
Alikuwa ni Ateba tena aliyeweka chuma cha pili katika dakika ya 44 akimalizia kwa kichwa mpira wa Kona wa beki wake wa kushoto Valentine Nouma na kuifanya timu yake kwenda mapumziko na mabao hayo 2-0 yaliyodumu hadi mwisho wa mchezo. Ateba alikuwa na nafasi ya kuwa mchezaji wa kwanza kufunga ‘hat-trick’ ya Ligi Bara msimu huu katika dakika 90 lakini alipaisha mpira akiwa jirani na lango na ushindwa kuitendea haki kazi nzuri Jean Ahoua aliyeingia kibabe katika boksi mbele kushoto na kupiga ‘v-pass’ moja matata sana.
BASI LA KEN GOLD
Ken Gold licha ya kuonekana kucheza soka la kuiheshimu Simba zaidi ikicheza kwa kujilinda lakini nidhamu yao hiyo ilidumu kwa dakika 34 tu na kujisahau kisha kufanya makosa ya haraka yaliyowapa mabao ya haraka wenyeji.
MHAGAMA KIPA
Licha ya Ken Gold kuruhusu mabao hayo watalazimika kumpongeza kipa wao Castor Mhagama ambaye alikuwa na dakika 90 za viwango akizima mashambulizi makali ya Simba.
Ken Gold ilifanya mashambulizi ya kushtukiza ambayo hata hivyo hayakuwa na nguvu mbele ya ukuta wa Simba yakiishia kwa kipa Moussa Camara.
Kipa huyo ukiondoa bao la penalti alikuwa imara kucheza mipira ya kona akifungwa kwenye kona ya nane kati ya tisa za Simba zilizopigwa kipindi cha kwanza baada ya Ateba kuruhusiwa kuruka akiwa huru.
ROTESHENI YA FADLU
Kocha wa Simba Fadlu Davids akiendelea kutoa nafasi kwa wachezaji wake akifanya mabadiliko matano kwenye kikosi chake tofauti na kile kilichocheza mchezo wa mwisho wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya CS Sfaxien ya Tunisia ambao wekundu hao walishinda kwa mabao 2-1.
Fadlu aliwaanzisha Nouma, Karaboue Chamou, Kelvin Kijili, Ladack Chasambi na Mzamiru Yassin ambao walianza tofauti na mchezo uliopita wakianzia benchi.
KEN GOLD HOI
Matokeo hayo yanaendelea kuwa ishara mbaya kwa Ken Gold ambayo imeendelea kudidimia mkiani kwenye msimamo wa Ligi ikishika nafasi ya 16 kwa pointi 6, baada ya kupoteza mechi yake ya 11 ndani ya michezo 15 iliyocheza.
MPANZU BADO
Mchezo huo wa jana mashabiki wa Simba walitarajia kumuona winga wao mpya Elie Mpanzu angeanza kuitumikia timu hiyo lakini haikuwa hivyo kwani imeelezwa bado haikupatikana ruhusa ya kuanza kucheza licha ya mabosi wa klabu hiyo kuwasilisha jina lake TFF. Simba tayari ina wachezaji 12 wa kigeni kama kanuni zinavyoelekeza hivyo inapaswa kumtema mmoja kwanza kabla ya kuingiza jina la Mpanzu TFF.