Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi amekuwa akisistiza kwamba wakati mwaka ukimalizika tukikaribia kuingia mwaka 2025, Wazanzibari watunze amani wakati safari ya kuelekea uchaguzi mkuu ujao ikiwa imeshika kasi.
Dk Mwinyi amesema maendeleo yaliyopatikana katika miaka minne ya uongozi wake yametokana na kupoa kwa uhasama wa kisiasa, watu kuelewana na kuweka maslahi ya nchi mbele kuliko maslahi yao binafsi na vyama vyao.
Katika moja ya hotuba zake msikitini baada ya swala ya Ijumaa, Dk Mwinyi aliwataka viongozi wa dini na kila mtu kuomba dua ya kuvuka salama katika uchaguzi ujao.
Wito wa Rais Mwinyi una umuhimu mkubwa, ukitilia maanani chaguzi zilizopita za vyama vingi Visiwani zimekuwa na vurugu za watu kupigwa, kujeruhiwa, nyumba zao kuvamiwa na watu kuuawa. Mamia hukimbilia Bara au Kenya kwa usalama wao.
Huu ni wakati unaposikia watu wamekwenda mwituni kujificha wasiuliwe, wengine kuwa wakimbizi na baadhi yao wapo huko mpaka leo na kuukana uraia wa Tanzania na kuwa raia wa Kenya na nchi za jirani.
Uchaguzi wa Zanzibar umegeuzwa leseni ya kufanya uonevu na ujahili na kuwa chanzo cha kuzalisha vilema, vizuka na mayatima na wengine kubakwa.
Ni hali ya kusikitisha ambayo ni tofauti na sifa ya uungwana na watu kupendana iliyokuwepo Zanzibar miaka ya nyuma.
Kwa watu wa Visiwani, zaidi ya asilimia 98 ya waumini wa dini, dua ni muhimu kwa kila jambo la heri na muumini anatakiwa asichoke kuomba hata akiona shida inamwandama kila pembe.
Hata hivyo, waumini wanaambiwa pamoja na kuomba dua, binadamu hutakiwa afanye mema na kujiepusha na kauli au vitendo viovu.
Ni muhimu kwa Rais Mwinyi, kama kiongozi mkuu wa serikali, viongozi wengine wa serikali na vyama vya siasa na kutafakari kwa nini chaguzi zinakuwa za ovyo na kuchochea uhasama wenye gharama kwa maisha, mali na uchumi wa Zanzibar.
Ukitafakari utaona ipo orodha ndefu ya mambo inayopelekea kuwepo hali hii na yote yanafaa kupigwa tochi na kutafuta njia sahihi na siyo hadaa.
Kwanza, ni kuhakikisha uandikishaji wapigakura unakuwa wa haki na usio na mazonge kama ya watu kunyimwa haki hiyo kwa visingizio vya sheha kutowajua, hata waliofunga ndoa na binti zao au kukosa kitambulisho cha Mzanzibari.
Tumeona wagombea, wakiwemo waliokuwa madiwani, wawakilishi au mawaziri kuenguliwa kugombea kwa kukosa sifa. Hili lililotokea kwa wapinzani tu siyo haki na inatia dosari uchaguzi.
Katika chaguzi zilizopita, wapo watu waliotambuliwa kujiandikisha zaidi ya mara moja na picha zao kuonyesha wamejiandikisha zaidi ya mara moja katika vituo tofauti, lakini hakuna aliyeshitakiwa.
Kila ukifanyika uchaguzi hutokea vijana wanaopiga watu vijiweni na majumbani kwao na hata kuuwa. Watu hawa waliopewa majina ya janjaweed hapo mwanzo na baadaye mazombi, walikuwa huru kutoa roho za watu na hakuna hata mmoja aliyewajibishwa kisheria.
Je, ni wapi watu hawa wanapata nguvu hizi na nani anawalinda? Kura ya mapema inapigiwa makelele na kudaiwa inatumika kufanya mizengwe. Tujiulize ni lazima iwepo wakati Bara haipo?
Mara nyingi husikia mawakala wa vyama vya upinzani wametolewa kwenye vituo. Tujiulize hawa wa CCM ni malaika na kwa nini kama wakala anatolewa pasiwepo mawakala mbadala wa kuingia pale wakala akitolewa?
Uteuzi wa Mkurugenzi aliyedaiwa kuvuruga uchaguzi wa 2020 kupewa tena kuifanya kazi hiyo kwa uchaguzi ujao, hatua inayolalamikiwa, ni dosari na imeibua wasiwasi.
Ni kawaida mshitakiwa au mlalamikaji akieleza kutokuwa na imani na hakimu mahakama hukubali hilo ombi na kuweka hakimu mwengine. Hivyo hivyo katika kandanda. Kwa nini iwe nongwa katika uchaguzi wa Zanzibar?
Katika chaguzi za Visiwani, vyombo vya habari vinabanwa, hata kutangaza matokeo yaliyobandikwa ukutani kwenye vituo. Hii siyo haki, maana kinachobandikwa ukutani siyo siri.
Kwa jumla, mambo haya na uteuzi wa wasimamizi wa uchaguzi yanahitaji marekebisho ili haki ionekana inatendeka. Haya yakifanyika, pamoja na dua, uwezekano wa Zanzibar kuwa na uchaguzi salama utakuwa mkubwa.
Watu wa Zanzibar lazima wajifunze kwa yaliyopita. Vinginevyo kila siku watahesabu ongezeko la vilema, mayatima, vizuka na watu wasiokuwa na hatia kuuawa.
Mungu isaidie Zanzibar kuvuka uchaguzi ujao kwa amani na kwa haki.