Changamoto lukuki zawakabili wahamiaji | Mwananchi

Dar es Salaam. Wakati dunia ikiadhimisha siku ya kimataifa ya wahamiaji, changamoto zinazowakabili zimetajwa kuwa pamoja na kuchelewa kupata utambulisho, kukosa ajira, huku wananchi wanaoishi mipakani wakinyimwa huduma kwa kuhusishwa na wahamiaji.

Maadhimisho hayo yalianza Desemba 18, 1990 baada ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kupitisha azimio kuhusu Mkataba wa Kimataifa wa Kulinda Haki za Wafanyakazi Wahamiaji na Wanafamilia wao.

Shirika la Kimataifa la Uhamiaji (IOM), huadhimisha Siku ya Kimataifa ya Wahamiaji kwa kusisitiza mchango wa takribani wahamiaji milioni 272 duniani kote, wakiwemo zaidi ya milioni 41 waliokimbia makazi yao ndani ya nchi zao.

Kauli mbiu ya mwaka huu ni kutambua michango wa wahamiaji na kuheshimu haki zao.

Katika taarifa iliyotolewa hivi karibuni na taasisi ya Dignity Kwanza imeeleza changamoto zinazowakabili wananchi kutokana na mwingiliano wa wahamiaji katika Wilaya za Kibondo na Kasulu mkoani Kigoma.

“Kiwango kikubwa cha uhamiaji Kasulu na Kibondo kimesababisha ukaguzi mkali wa uhamiaji kwa waombaji wa Vitambulisho vya Taifa, hali inayowakwamisha wengi.

“Baadhi ya watu, wanapoona kuwa mahitaji ya mchakato huo ni magumu na yanachukua muda mwingi, huamua kuachana nao kabisa, hali ambayo inahatarisha uwezekano wa watu hao kukosa utaifa,” imesema taarifa hiyo.

Taarifa hiyo imetaka haki za wananchi zilindwe ikiwa pamoja na kupewa utambulisho.

“Hali hii imesababishwa kwa kiasi kikubwa na ukosefu wa nyaraka rasmi za kiraia kwa muda mrefu nchini Tanzania, pamoja na uhusiano wa kijamii na watu kutoka nchi jirani, mambo ambayo yapo nje ya uwezo wao.”

Akizungumzia kadhia hiyo, Mkuu wa Kitengo cha mawasiliano ya Serikali wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida), Geoffrey Tengeneza amesema ucheleweshwaji wa kutoa vitambulisho hutokana na mchakato mrefu wa kuwatambua wananchi.

“Tunaifahamu hiyo changamoto kwa wananchi wa mipakani, kwa sababu kunakuwa na mwingiliano na ahamiaji wan chi nyingine, unapotoa vitambulisho ni lazima tujiridhishe vya kutosha ili tusije kutoa kwa watu wasio na sifa,” amesema.

Amesema katika utoaji wa vitambulisho wanashirikiana na wadau wengine zikiwamo kamati za ulinzi na usalama za wilaya ambazo nazo hushirikiana na wananchi.

“Katika mchakato huo, waombaji huleta picha, tunaziweka kwenye matangazo ili wananchi wazione na waweke mapingamizi,” amesema.

Amesema pia hushirikisha idara ya uhamiaji kutambua walio raia wa Tanzania na wasio raia.

Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali wa Uhamiaji, Paul Msele amesema katika kutambua uraia wa watu, sifa za kisheria huangaliwa.

“Sio kila mtu anapewa kitambulisho cha uraia, bali ni wale tu wenye sifa ya kuwa raia wa Tanzania, wageni waliokidhi matakwa ya sheria na wakimbizi walioingia kihalali,” amesema.

Amesema wahamiaji wanaoingia nchini wanapaswa kupitia kwenye vituo vya uhamiaji vilivyopo mipakani wakiwa na pasi za kusafiria na viza.

“Kwa sasa tumerekebisha sheria ya viza, zamani kwa mfano watu wanaotoka Ethiopia walitakiwa kulipia viza kabla hawajaja Tanzania, lakini kwa sasa wanalipia wakishafika, kwa hiyo ni rahisi kulipia na kupewa pasi ya kuingia na kutoka,” amesema.

Mbali na wahamiaji wa hiari, wapo pia wasio wa hiari ambao ni wakimbizi. Mtafiti wa kujitegemea, Uwezo Ramadhani amesema miongoni mwa changamoto zinazowakabili ni kukosa ajira.

“Changamoto iliyopo kwa wakimbizi wanaoishi makambini, hawaruhusiwi kutoka kufanya kazi, sanasana huishia kujitolea kwenye mashirika yanayowahudumia kwa ujira mdogo,” amesema

Hata hivyo, amesema wapo wanaoendelea na masomo na wengine huruhusiwa kutoka kambini kwa vibali maalumu kama vya kwenda kupata matibabu.

“Hata wanapomaliza masomo vyuoni, bado kuajiriwa inakuwa ngumu, kwani baadhi ya waajiri huona kero kupeleka nyaraka zao kwenye vyombo vya Serikali, ilihali wanaweza kupata Watanzania wasio na nyaraka nyingi,” amesema.

Ameongeza, “Wahamiaji nao ni watu, Serikali iangalie haki zao za kazi kwa kutumia nguvu kazi na vipaji walivyonavyo.”

Hata hivyo, Mkurugenzi wa Idara ya Wakimbizi, Sudi Mwakibasi amesema wakimbizi wanaruhusiwa kufanya kazi lakini sio katika sekta ya umma.

“Wakimbizi wanaruhusiwa kuomba kazi katika soko la ajira. Hata kama hawaruhusiwi kutoka nje ya kambi, wanaweza kuomba hata mitandaoni.

“Tena Serikali imerekebisha sheria na imeondoa ada ya vibali vya kufanya kazi kwa wakimbizi. Wasioruhusiwa kufanya kazi ni waomba hifadhi ya ukimbizi kwa kuwa bado Serikali haijajua kama itawapa au haitawapa,” amesema Mwakibasi.

Related Posts