Chirwa, Sey tumaini jipya KenGold

WAKATI kikosi cha KenGold kikiwa na mchezo jana wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Simba, mabosi wa timu hiyo tayari wameanza hesabu za kukinusuru mkiani, huku wakianza na majina makubwa ambayo wanaamini yatawasaidia kukibakisha kwa msimu ujao.

Hesabu za mabosi hao zimetua kwa mshambuliaji nyota wa zamani wa Yanga na Azam FC, Obrey Chirwa ambaye inaelezwa yupo hatua za mwisho kujiunga kwa mkopo akitokea Kagera Sugar, ikiwa ni pendekezo la kocha mkuu wa timu hiyo, Omary Kapilima.

Kama haitoshi, Mwanaspoti imepata taarifa mbali na Chirwa, nyota mwingine aliyekuwa kwenye mazungumzo na kikosi hicho ili kuongeza nguvu ni aliyekuwa mshambuliaji wa Namungo, Stephen Sey aliyekuwa anaichezea Anwar Al-Abyar ya Libya.

Chanzo cha ndani cha timu hiyo kililiambia Mwanaspoti nyota mwingine ni kiungo mshambuliaji, Lassa Gradi Kiala ambaye aliwahi kuichezea FC Saint Eloi Lupopo ya kwao DR Congo, huku akizichezea pia Kitwe United na Zanaco FC zote za Zambia.

“Ni kweli wachezaji hao tuko katika mazungumzo nao na kama kila kitu kitakamilika tutawatangaza kuichezea timu yetu kwa lengo la kuongeza nguvu, hatutaki kuona tunashuka daraja hivyo, lazima tujipange mapema na hilo,” kilisema chanzo chetu.

Kwa upande wa Ofisa Mtendaji Mkuu wa Kengold, Benson Mkocha alisema kwa sasa asingependa kuzungumza jambo lolote juu ya usajili kwa sababu bado hawajakamilisha, ingawa ni kweli taratibu hizo zimeanza kutokana na matakwa ya benchi la ufundi.

“Tukikamilisha taratibu zote tutaweka wazi kwa sababu bado mchakato unaendelea na kama unavyojua hiki ni kipindi ambacho ushindani ni mkubwa kutokana na mahitaji ya kila timu, ingawa nikiri mashabiki wetu watarajie mambo mazuri,” alisema.

Related Posts