Hekaheka kimbunga Chido kikiacha balaa Mayotte, Msumbiji

Dar es Salaam. Watu 34 wameripotiwa kufariki dunia Msumbiji baada ya Kimbunga kilichopewa jina la Chido kuipiga nchi hiyo.

Mbali na maafa hayo, inaelezwa hadi kufikia jana Desemba 17, 2024, jumla ya watu 174,158 wameathiriwa wameathiriwa namna mbalimbali na wengine 319 kujeruhiwa.

Kimbunga hicho kiliipiga Msumbiji tangu Jumapili, Shirika la Umoja wa Mataifa la misaada ya kibinadamu (OCHA) liliripoti jana.

Taasisi ya Kitaifa ya Kudhibiti Hatari na Majanga ya nchi hiyo, imesema kimbunga hicho pia kimeharibu zaidi ya nyumba 23,000.

Kwa takwimu za awali Chido kimepiga katika Jimbo la Cabo Delgado, Jumapili na kati ya watu waliofariki dunia ni kutoka maimbo ya Nampula na Niassa.

Taasisi hiyo imesema upepo wake ulifikia kilomita 260 kwa saa na mvua ya milimita 250 ilinyesha katika saa 24 huku boti 170 za uvuvi zikiharibiwa.

Mbali na Msumbiji, inaelezwa kuwa kimbunga Chido pia kimekikumba Kisiwa cha Mayotte kinachomilikiwa na Ufaransa, huku maelfu ya watu wakiaminika kupoteza maisha, kabla ya kuelekea Msumbiji.

Taarifa zinasema maeneo mengi ya Mayotte bado hayawezi kufikiwa huku ikielezwa kwamba inaweza kuchukua siku kadhaa kubaini ukubwa wa athari, imeeleza tovuti ya TRT Afrika.

Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron kesho Alhamisi Desemba 19, 2024, atatembelea maeneo yaliyopata madhira ya kimbunga hicho.

Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (Unicef) limesema takribani watoto 90,000 wameathiriwa na kimbunga hicho.

Kwa sasa Unicef inahofia kusambaa kwa magonjwa yanayosababishwa na maji.

Mwakilishi wa Unicef nchini Msumbiji, Mary Eagleton amesema: “Msumbiji inachukuliwa kuwa ni moja ya nchi iliyoathirika pakubwa wa mabadiliko ya tabianchi duniani na watoto walikuwa tayari wanakabiliwa na dharura nyingi zinazotishia maisha yao ikiwemo machafuko, ukame na magonjwa ya milipuko.”

Ameongeza kuwa; “Unicef pamoja na Serikali, mashirika dada ya Umoja wa Mataifa, mashirika yasiyo ya kiserikali na washirika wengine wanachukua hatua mbalimbali kukabiliana na athari za kimbunga hicho kwa kutoa kipaumbele katika masuala ya dharura ya kibinadamu.”

Nalo Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi (UNHCR), limesema athari za kimbunga hicho kwa watu ni kubwa na maelfu wamelazimika kukimbia kwenda kusaka mahala salama pa kukaa kutokana na uharibifu mkubwa wa makazi, mundombinu ya barabara na mfumo wa mawasiliano.

Related Posts