KONA YA MALOTO: Lissu kumvaa Mbowe; halali kidemokrasia, batili kwa masilahi ya Chadema

Nimesoma ujumbe wa Makamu Mwenyekiti wa Chadema, Tanzania Bara, Tundu Lissu, kuhusu njama dhidi yake, zinazoratibiwa na “watu wasiojulikana”, ili likitokea la kutokea, tuhuma zielekezwe kwa Mwenyekiti wake, Freeman Mbowe.

Natambua uhusika wa Mbowe katika kuokoa maisha ya Lissu, alipopigwa risasi na wauaji Dodoma, miaka saba iliyopita. Mbowe ni mwema sana kwa Lissu, hilo halina shaka. Inawezekana vipi abadilike leo atake kumuua aliyempigania uhai wake? Binadamu atabaki kuwa binadamu.

Nafahamu, Lissu ameamua kugombea uenyekiti Chadema ili kumrithi Mbowe, anayekiongoza chama hicho kwa mwaka wa 20 sasa. Hali halisi inajionesha kuwa Mbowe atagombea tena. Bila shaka, unakwenda kuwa mtanange wa kikubwa sana ndani ya Chadema.

Kihistoria, alichokisema Lissu ni kawaida. Ajali ya aliyekuwa Makamu Mwenyekiti Chadema, Tanzania Bara, Chacha Wangwe, hata yeye (Lissu), aliposhambuliwa kwa risasi nyingi Septemba 7, 2017, sauti zilielekezwa kwa Mbowe.

Kiusalama, inaitwa “agent provocateur” (wakala wa uchonganishi). Mtu au watu, wanakula njama, wanatenda jambo, lengo likiwa kuchonganisha watu, taasisi, jumuiya au serikali. Ndiyo sababu ajali ya Wangwe, alitajwa Mbowe, vivyo hivyo shambulizi dhidi ya Lissu.

Ukumbusho, Wangwe alipoteza maisha kipindi ambacho alikuwa kwenye mgogoro na chama chake. Alisimamishwa uongozi kwenye chama kwa sababu za kinidhamu. Wangwe mwenyewe alisema, kilichomponza ni kuhoji kasoro nyingi ndani ya chama, vilevile nia yake ya kuwania uenyekiti.

Kabla ya kutangaza nia yake ya kuwania uenyekiti, Lissu alishakuwa kwenye hali ya kupishana mitazamo na Mbowe pamoja na viongozi wenzake wengine kwenye chama. Alishanukuliwa akimtetea Peter Msigwa, ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Nyasa, kabla ya kuhamia CCM.

Matamshi ya Lissu hayahitaji mkalimali ili kueleweka kwa kila mtu kwamba ameumia ndani ya moyo, Msigwa kuhamia CCM. Lissu amekuwa akitaka hoja za Msigwa zijibiwe. Shida kubwa ni kwamba maneno ya Msigwa kwa asilimia kubwa humshambulia Mbowe.

Msimamo wa Lissu tayari ulishajenga ufa baina yake na Mbowe. Huwezi kuwa rafiki au mshirika wa kutumainiwa kwa mtu, ikiwa kila uchwao unasikika ukimkweza au kumsemea mema adui yake. Hili Lissu analifahamu na anajali hisia za Msigwa hadharani, kwa kudhamiria, bila kuzunguka.

Jambo ambalo linatakiwa lieleweke ni kuwa uamuzi wa Lissu kuwania uenyekiti Chadema Taifa ni matunda ya demokrasia, vilevile gharama za demokrasia. Lissu amefanya jambo zuri kidemokrasia.

Uamuzi wa Lissu ni kipimo cha demokrasia ya chama. Je, haki itatendeka mwanzo hadi mwisho na uchaguzi utakuwa huru na haki? Matokeo ya mwisho yatatoa tafsiri ya hali ya demokrasia kwenye chama. Huu ni mtihani mkubwa kwa chama cha kidemokrasia.

Upande wa pili, Kamati Kuu Chadema, hivi karibuni ilitangaza maazimio yake kuelekea Uchaguzi Mkuu 2025. Hii ni baada ya kushuhudia faulo nyingi katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, uliofanyika Novemba 27, 2024.

Ukiyapitia maazimio hayo, utaona kuwa Chadema wanahitaji umoja ili kufanikisha malengo yao. Endapo uchaguzi wa ndani, hususan mbio za kuwania uenyekiti zitawaathiri, kama chama, watakuwa kwenye wakati mgumu kusukuma agenda zao zilizomo ndani ya maazimio waliyoyatangaza baada ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024.

Hapo sasa ndiyo unahoji nguvu ya demokrasia dhidi ya masilahi ya chama. Vilevile vipaumbele vya watu ndani ya agenda za chama. Uchaguzi ni mchuano na mnyukano. Je, matokeo ya mwisho yatambakiza kila mmoja akiwa mwenye tabasamu na ari ya kukipigania chama?

Kwa tafsiri, pamoja na kuheshimu demokrasia, vilevile kutambua haki yake kidemokrasia, uamuzi wa Lissu kuwania uenyekiti katika mazingira ya sasa yanarejesha kumbukumbu ya Karne ya 20.

Aliyekuwa Kamanda wa Vikosi vya Umoja wa Mataifa (UN), Jenerali Douglas MacArthur, alipendekeza kwa Serikali ya Marekani, kuendeleza uchochezi kwenye Vita ya Korea na China kama njia muhimu ya kuutokomeza Ukomunisti.

Hata hivyo, mbele ya jopo la wanadhimu wa majeshi ya Marekani, katika mkutano ambao ulihudhuriwa pia na aliyekuwa Rais wa Marekani wakati huo, Harry Truman, aliyekuwa kamanda Nyota-5 wa Jeshi la Marekani, hayati Omar Nelson Bradley, alipingana na wazo hilo la kuchochea Vita ya Korea na China.

Bradley alisema kuwa uchochezi huo wa vita ya China na Korea ni “wrong war, at the wrong place, at the wrong time, and with the wrong enemy” (vita batili, katika eneo batili, katika muda batili, na dhidi ya adui batili).

Kwamba nyakati hizo, Marekani kama baba wa ubepari, ilipaswa kujielekeza kupambana na Umoja wa Dola ya Kisovieti (USSR). Kujiingiza kwa Wachina na Wakorea, ilikuwa ni kupoteza rasilimali fedha, muda na watu, tena zaidi mafanikio yasingeonekana.

Mchuano wa Lissu na Mbowe Chadema si uadui, kama mfano wa China na Korea, ila mfanano wake ni uchaguzi wa vipaumbele. Mahali gani pa kuelekeza shabaha? Kumaliza nishati kwa kushughulikiana ndani au kulinda nguvu kukabiliana na CCM pamoja na dola ili kufanikisha malengo yaliyomo kwenye maazimio kabla ya Uchaguzi Mkuu 2025?

Kuweka masilahi ya chama mbele ni gharama kubwa. Kuvumilia viongozi na wanachama wenzako usiowapenda, chama kisonge. Kujizuia kufanya matendo yanayoweza kukera wengine. Kukubali usiyoyapenda yasonge mbele kufikia lengo mama. Kupunguza matarajio ili kuendana na wenzako.

Ni kama Lissu amechagua kusafisha chama, kisha ndiyo wakakabiliane na CCM. Je, kuna tahadhari Mbowe akishindwa uchaguzi? Vipi Lissu akianguka? Nani malaika kati yao, atakaposhindwa, atasimama bega kwa bega na mwenzake kuunganisha chama kuelekea agenda za uchaguzi?

Maswali hayo kwa wingi wake, yanajenga wasiwasi kuwa uamuzi wa Lissu kuwania uenyekiti dhidi ya Mbowe, unaweza kuwa vita batili katika muda batili. Chama kinahitaji kuunganishwa, ukizingatia imebaki miezi 10 ufanyike Uchaguzi Mkuu 2025.

Related Posts