La mgambo lalia TFS, wavamizi hifadhini kikaangoni

Tanga. Wakala wa Huduma za Misitu (TFS) Kanda ya Kaskazini inajiandaa kutekeleza maagizo ya Serikali ya kuwaondoa wananchi waliovamia hifadhi za misitu na kufanya shughuli za kibinadamu katika maeneo hayo.

Akizungumza leo Desemba 18, 2024 katika kikao cha pamoja na wadau wa uhifadhi, Meneja wa TFS Kanda ya Kaskazini, Kamishna Mwandamizi wa Uhifadhi, James Nshale amesema Serikali kupitia vikao vya wilaya imeagiza wavamizi wote waondolewe hifadhini.

Ametaja maeneo yaliyoathiriwa na wavamizi ni pamoja na hifadhi ya Chang’andu wilayani Korogwe.

Amesema hifadhi hiyo iliandikishwa kama hifadhi ya miti asilia mwaka 1958, huku akiitaja pia hifadhi ya Gendagenda iliyopo Wilaya za Pangani na Handeni iliyoandikishwa mwaka 1960 na kufanyiwa marejeo mwaka 1980.

Nshale amesema Kijiji cha Kwabojo kitatakiwa kuhamishwa ili kulinda hifadhi hiyo.

“Hifadhi ya Bondo, yenye ukubwa wa hekta 18,000 iliandikishwa mwaka 1960, imevamiwa na wananchi zaidi ya 2,000 wanaojishughulisha na kilimo, ufugaji na wamejenga makazi, makanisa 40 na shule ya msingi iliyo Kijiji cha Kovidi,” amesema.

Hata hivyo, amesema wameshanza mchakato wa kuwaondoa watu hao hifadhini ili kulinda misitu hiyo kwa vizazi vijavyo.

“Tukisema tuwaache na kuhalalisha vijiji vyao, maana yake ni kwamba watu watavamia hifadhi na kujenga makazi wakijua wataachwa. Hii haikubaliki, lazima watoke,” amesema Kamishina Nshale.

TFS Kanda ya Kaskazini inasimamia hifadhi tano za misitu asilia, ambazo ni Amani, Nilo, Magamba zilizopo mkoani Tanga, Chome iliyopo Same mkoani Kilimanjaro na Ismangoli mkoani Arusha.

Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Dk Batilda Burian, Mkuu wa Wilaya ya Korogwe, Kamishina Mwandamizi wa Uhifadhi William Mwakilema, amesema mkoa huo upo tayari kulinda na kuendeleza rasilimali za misitu zote na wavamizi wote wataondolewa kwa mujibu wa sheria.

“Serikali ya Mkoa wa Tanga kwa kushirikiana na TFS itahakikisha tunalinda rasilimali hizi za misitu na watu wote waliovamia hifadhi wataondolewa kisheria ili kulinda maeneo haya,” amesema Mwakilema.

Hata hivyo, ameitaka TFS kuhakikisha wanapanda miti katika maeneo ya uhifadhi, ikiwemo miti ya mianzi, ambayo sasa imekuwa ikitumika kutengeneza samani.

Related Posts