Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba amesema rafu zilizojitokeza katika chaguzi za serikali za mitaa tangu wa mwaka 2019 na huu wa 2024, pamoja na Uchaguzi Mkuu 2020 zinamkumbusha mambo mengi.
Profesa Lipumba ameyasema hayo leo Jumatano, Desemba 18, 2024 wakati akitoa tathmini ya chaguzi hizo zilizofanyika ndani ya miaka mitano.
Akitolea mfano wa mwaka 2019, Profesa Lipumba amesema walisimamisha wagombea wao ambao walienguliwa karibia nchi nzima kwa sababu alizoziita si za msingi.
“Wengine walikuwa wenyeviti wa vijiji na mitaa waliambiwa hawana sifa kwa sababu hawajui kusoma na kuandika jambo ambalo halikuwa kweli, wengine waliambiwa wameshindwa kujaza fomu vizuri. Tulilalamika tukatoa taarifa na mwisho wa siku wagombea wetu hawakushiriki,” amesema.
Hata hivyo, Profesa Lipumba amesisitiza kwamba hawakukata tamaa wala kususia Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020, ingawa matokeo yake yaliwashangaza.
“Pamoja na kufanya kampeni nchi nzima katika uchaguzi wa mwaka 2020, tulipata kura za urais 75,000, mbunge mmoja bara na Zanzibar wabunge wawili,” amesema Profesa Lipumba.
Akikumbuka hali iliyowashangaza, amesema; “Kuna wilaya moja niliyofanya kampeni ambapo nilikaribishwa kwa heshima kubwa na hata kupewa mbuzi, lakini matokeo yalipotangazwa wilaya nzima yenye majimbo mawili sikupata hata kura moja.”
Akizungumza mkutano mkuu unaofanyika leo, Profesa Lipumba amesema una ajenda moja kuu ambayo ni uchaguzi wa viongozi watakaohudumu kwa kipindi cha miaka mitano ijayo.
Hata hivyo, amesema mkutano huo ulikuwa ufanyike Machi, ni kutokana na kukosekana kwa fedha.
“Mkutano ulipangwa ufanyike Machi, ukasogezwa hadi Septemba 15, 2024, lakini tena ukaahirishwa hadi Desemba 13, na hatimaye unafanyika leo,” amesema Profesa Kabudi.
Wajumbe wa mkutano huo watamchagua mwenyekiti, makamu mwenyekiti wa Bara na Zanzibar sambamba na wajumbe wa Baraza Kuu la chama. Profesa Lipumba ambaye anatetea kiti cha mwenyekiti, ameshahudumu kwenye nafasi hiyo kwa miaka 25.
Msajili Msaidizi wa Vyama vya Siasa, Sisty Nyahoza, ameipongeza CUF kwa kufanikisha mkutano mkuu na kuendeleza demokrasia ndani ya chama hicho.
“Ofisi yetu ipo kuhakikisha vyama vya siasa vinazingatia demokrasia kwa mujibu wa sheria ya vyama vya siasa, sura ya 258, inayotaka viongozi wa vyama wachaguliwe au kuteuliwa kwa kufuata katiba ya chama husika,” amesema Nyahoza.