Majaji watano wajifungia TCB kusaka Kahawa bora

Moshi. Mashindano ya tano ya kusaka kahawa bora Tanzania yameanza rasmi, hatua ambayo inatajwa kuwa muhimu na inayotarajiwa kuongeza upatikanaji wa bei nzuri kwa zao hilo katika masoko ya kimataifa.

Mashindano hayo yanafanyika katika Idara ya Uonjaji Kahawa na Minada, ndani ya jengo la Bodi ya Kahawa Tanzania (TCB).

Mashindano hayo yalianza rasmi Jumatatu Desemba 16 na yatahitimishwa Alhamisi Desemba 20, 2024.

Jumla ya sampuli 76 za kahawa zimewasilishwa na 18 zimetolewa na wakulima wakubwa huku 58 zikitoka kwa vyama vya msingi na vikuu vya ushirika.

Akizungumza leo Jumatano, Desemba 18, 2024 wakati mashindano hayo, Mkurugenzi wa Maendeleo ya Kahawa TCB, Kajiru Francis amesema mashindano hayo yanalenga kuhamasisha wakulima kuzalisha kahawa yenye ubora wa hali ya juu ambayo huleta bei nzuri katika masoko ya dunia.

“Mashindano haya yanahusisha wakulima na wazalishaji wa kahawa kuwasilisha sampuli ambazo zinaonwa na majaji, ili kuchagua kahawa bora,” amesema Kajiru.

Amesema sampuli bora zitakazoshinda zitaingizwa kwenye minada ya mtandao ya kimataifa, hatua inayolenga kuongeza thamani na umaarufu wa kahawa ya Tanzania.

Kwa mujibu wa Kajiru, mashindano ya mwaka huu yanafanyika kwa ukubwa zaidi kwa kushirikiana na Chama cha Kahawa Bora Afrika. Ushirikiano huu utawezesha wakulima wadogo kutoka vikundi na AMCOS kushindana na wazalishaji wakubwa duniani kote.

“Tumeamua kuyafanya mashindano haya kuwa ya kimataifa ili kuiweka kahawa ya Tanzania katika ramani ya dunia, tukionyesha kuwa kahawa yetu ni bora na inakidhi viwango vya kimataifa,” amesema Kajiru akisisitiza umuhimu wa kanuni bora za kilimo ili kuhakikisha uzalishaji wenye tija.

Ofisa Masoko Mwandamizi wa TCB, Naishoki Lucumay amesema lengo kuu la mashindano hayo ni kuwahamasisha wakulima kuandaa kahawa yenye ubora unaoweza kushindana kimataifa.

“Leo tunaendelea na mashindano ya tano ya kutafuta kahawa bora Tanzania. Wakulima wanapaswa kuelewa kuwa kahawa bora husimama sokoni hata wakati bei ya zao hilo inashuka. Hivyo, mashindano haya yanatoa chachu ya kuzalisha bidhaa yenye thamani,” amesema Lucumay.

Kwa upande wake, Albertus Paschal kutoka Chama Kikuu cha Ushirika Karagwe amesema wamewasilisha sampuli zao ili kupima ubora wa uzalishaji wao na kujifunza maeneo yanayohitaji maboresho.

“Mashindano haya ni fursa ya kujifunza na kuboresha mnyororo mzima wa thamani ya kahawa, kutoka uzalishaji hadi usindikaji,” amesema Paschal.

Related Posts