Matonya: Rais wa ombaomba aliyeanza kuomba kabla ya Uhuru

Unaweza kumwita kwa majina utakayo: rais wa ombaomba, nguli wa kuomba, mtoto wa mjini na mengineyo.

Hata hivyo, unaweza kumwita mwamba aliyefikia hatua ya kutunishiana misuli na mamlaka.

Unamkumbuka ombaomba huyu maarufu nchini?  Alijulikana kwa jina moja la Matonya. Jina lake likawa kiwakilishi na msemo unaowakilisha watu wanaoomba msaada wa fedha kwa jamaa, marafiki, au ndugu.

Ukiwa mtu wa kupenda ‘kupiga mizinga’ jina lililosadifu kwako lilikuwa matonya.

Matonya, ambaye jina lake halisi ni David Paulo, alizaliwa Kijiji cha Mpamatwa, wilayani Bahi, Mkoa wa Dodoma.

Safari yake ya maisha mjini ilianza mwaka 1961 alipohamia Dar es Salaam kwa mara ya kwanza kwa kazi ya kuomba.

Matonya pia aliingia katika vuta nikuvute na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Yusuf Makamba, alipokataa kurudi kijijini kwao Bahi.

Akijiamini kama “mtoto wa mjini,” alisisitiza kuwa Makamba hangeweza kumlazimisha kuondoka jijini, akionyesha msimamo wake thabiti dhidi ya mamlaka.

Ilifikia hatua alipachikwa jina la utani kuwa yeye ni ‘kiboko ya Makamba’. Hadi mwanamuziki wa kizazi kipya, Professor Jay alimuimba kwenye mashairi ya wimbo wake Bongo Dar es Salaam akiwa amemshirikisha mwanamuziki mwenzake mwanadada Lady Jaydee.

Baadhi ya mashairi ya wimbo huo ni;

Licha ya juhudi za wakuu wa mikoa waliopita kushindwa kumtimua Matonya jijini Dar es Salaam, ambaye kila mwisho wa mwaka (Desemba) alijipa likizo na kurudi kwao Bahi mkoani Dodoma kusherehekea Krismasi na familia yake, hatimaye aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Yusuf Makamba, aliweza kufanikisha azma hiyo.

Makamba alitangaza rasmi kumtimua Matonya jijini Dar es Salaam, huku akiziamuru mamlaka husika kuhakikisha kwamba hatorudi tena ndani ya mipaka ya jiji hilo.

Hata hivyo, Matonya hakukata tamaa. Alihamia mkoani Morogoro, ambako aliendelea na shughuli zake za kuomba mitaani. Huko nako alikamatwa na kufikishwa mahakamani.

Baadaye, Matonya alirudi kijijini kwake Bahi Sokoni, kitongoji cha Nghungugu, umbali wa kilomita tatu kutoka makao makuu ya wilaya ya Bahi. Alipohojiwa na gazeti hili kuhusu sababu za kurudi kijijini na iwapo alimuogopa Makamba, alijibu kwa mbwembwe:

“Mimi ni kiboko yao! Siyo Makamba tu, hata wengine wananijua. Wanatambua umuhimu wangu katika Jiji la Dar es Salaam na Morogoro kwa sababu ninachangamsha miji hiyo.”

Matonya aliongeza kwa kujivunia:

“Nilianza kuomba Dar es Salaam siku chache kabla ya Nyerere (Mwalimu Julius Nyerere) kutundika bendera ya Uhuru na kushusha ile ya mkoloni mnamo Desemba 9, 1961. Kwa hiyo, mimi niliingia pale kabla ya Nyerere kutawala. Huyo Makamba wenu asijaribu kunihangaisha; hata mimi ni mtoto wa mjini.”

Aidha, Matonya alifichua jinsi kazi ya kuomba ilivyomsaidia kiuchumi:

“Kwa kipindi hicho, nilikuwa namaliza miezi mitano hadi sita jijini, kisha narudi nyumbani. Kila niliporudi, nilinunua kati ya ng’ombe watatu hadi watano. Kwa mwaka mmoja, nilikuwa na uwezo wa kununua kati ya ng’ombe nane hadi kumi.”

Mahakama ya Mwanzo ya Nunge, Manispaa ya Morogoro, ilimhukumu Matonya kifungo cha nje cha mwaka mmoja kwa kukiuka amri ya kuacha kuomba mitaani.

Ofisa Ustawi wa Jamii wa Mkoa wa Morogoro, Oswin Ngungamtitu, alisema Matonya alikamatwa baada ya kurudi Morogoro na kuendelea kuomba licha ya kiapo cha kuacha kazi hiyo alichotoa mbele ya mamlaka.

Matonya aliahidi kuishi katika Kambi ya Wazee wasiojiweza ya Fungafunga, lakini alikiuka makubaliano hayo.

Baada ya hukumu, Matonya alipelekwa kwenye Kambi ya Wazee akisubiri kusafirishwa kurudi nyumbani Dodoma, ambako aliishi huko hadi kifo kilipomkuta mwaka 2012.

Licha ya baadhi ya watu kudai kwamba Matonya alikuwa tajiri na mwenye nyumba nzuri kijijini kwake, alipoulizwa enzi za uhai wake alikanusha madai hayo kwa kusema:

“Mimi sina nyumba. Hapa ninapoishi ni kwa mtoto wangu wa kike. Watu wanasema nina mali, lakini hao ni walambi (akimaanisha waongo).”

Matonya, aliyepata kipato cha Sh4,000 hadi Sh7,000 kwa siku kutokana na kazi ya kuomba, alisema fedha hizo alizitumia kununua ng’ombe.

Hata hivyo, mifugo hiyo alidai kuibiwa na ndugu zake, jambo lililomkera na kumfanya aache kabisa kumiliki mali.

“Mimi sina kabisa mali; hata mbuzi au kuku sina, wala sina mpango wa kununua tena hata kama nina pesa. Walizoea kuniibia, hivyo sitaki tena kuwa na mali,” alisema kwa masikitiko.

Kwa mwezi, Matonya alisema alikuwa akipata kati ya Sh50,000 na Sh100,000, na mara nyingi alikuwa akirudi kijijini kila baada ya miezi miwili au mitatu tangu aanze kazi hiyo mwaka 1961.

Kuhusu miji aliyofanya kazi, alisema Dar es Salaam ilikuwa na kipato kizuri kuliko Morogoro.

“Dar es Salaam ni kuzuri kuliko Morogoro. Huko naingiza kati ya Sh5,000 na Sh7,000 kwa siku, wakati Morogoro ni kati ya Sh4,000 na Sh5,000. Chakula Dar es Salaam pia ni bei rahisi na mji ni msafi; hakuna hatari ya magonjwa kama kipindupindu,” alisema.

Matonya pia alifichua kuwa hakuwa na mke tena baada ya kuachana na mke wake wa tatu wakati wa Vita ya Kagera (1978-1979).

“Tangu wakati huo sijaoa tena, na sina mpango wa kuoa. Huyo alikuwa mke wangu wa mwisho,” aliongeza.

Alisema ana watoto wawili, Eliza na Ernest, waliopatikana na mke wake wa mwisho, Paulina Ngalya, ambaye bado anaishi kijijini Mpamantwa. Ernest ni dereva jijini Dar es Salaam, huku Eliza akiwa kijijini.

Related Posts