Mbowe ajibu mapigo, kutangaza hatima yake Chadema Jumamosi

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe amevunja ukimya kuhusu kuendelea kugombea uenyekiti kwa mara nyingine akisema haitaji kuingia kwenye vita ya kukipasua chama hicho.

Mbowe ametoa kauli hiyo leo Jumatano, Desemba 18, 2024 alipozungumza na viongozi na wanachama wa Chadema waliofika nyumbani kwake Mtaa wa Mwanamboka, Mikocheni Dar es Salaam, kumwomba agombee uenyekiti.

“Sihitaji kwenda kwenye vita itakayopasua chama, nitaangalia mwenendo wa kampeni nikiona chama changu kinakwenda kuzamishwa, kamanda naingia mzigoni,” amesema.

Mbowe ambaye ameshakiongoza chama hicho kwa miaka 20 tangu 2004, anakabiliwa na shinikizo la kutogombea, wakati mwenyekiti wa chama hicho, Tundu Lissu ameshachukua na kurejesha fomu ya kuwania nafasi ya uenyekiti.

Miongoni mwa kauli alizotoa Lissu Desemba 12, 2024 wakati akitangaza nia ya kugombea uenyekiti wa chama hicho ni pamoja na ukomo wa madaraka kwa viongozi wote wa chama hicho, mfumo wa fedha na mfumo wa uchaguzi.

Mbali na hayo, kwa nyakati tofauti Lissu amenukuliwa akidai kuwepo kwa fedha za rushwa katika uchaguzi wa chama hicho, huku akidai kutaja majina ya baadhi ya makada waliozipokea katika kikao cha kamati kuu.

Kutoa msimamo baada ya saa 48

Akizungumza mbele ya makada waliofika nyumbani kwake, Mbowe amewaomba wampe saa 48 za kutafakari ombi lao la kumtaka kuwania tena nafasi hiyo.

“Nimesikia ombi lenu, nawaomba mnipe saa 48 za kutafakari, kisha nitazungumza na wahariri wa vyombo vya habari Jumamosi (Desemba 21, 2024) hapa hapa nyumbani kutoa msimamo wangu,” amesema.

Akionekana kujibu hoja zilizoibuka katika mnyukano wa uchaguzi, Mbowe bila kutaja jina la mtu ameeleza kutoridhishwa na msigano wa makundi na kauli za viongozi wa chama hicho, huku akisisitiza kuwa mambo yanayotekelezwa na chama ni uamuzi wa vikao.

“Ni matumaini yangu kwamba kama kuna kiongozi wa chama mpaka leo haamini tunachokifanya kina ukweli, pengine yuko katika nyumba ambayo sio sahihi,” amesema.

Amesisitiza kuwa chama hicho kinaongozwa na vikao na sio matamko ya mwenyekiti.

“Mimi ni kiongozi wa chama ndio, lakini maamuzi ya chama tunayafanya pamoja kwenye vikao. Kwa hiyo anapotoka kiongozi miongoni mwetu ambaye ni mjumbe wa kamati kuu kwa miaka 20, ambaye kwa vyovyote anawajibika kwa kila uamuzi uliotoka kwenye chama kuulinda na kuutetea, ndio demokrasia.

“Akitoka akasema tofauti tunaweza kumhoji mwenzetu, ina maana miaka yote hiyo hatukuwa pamoja?” amehoji.

Huku akisisitiza umoja na kukilinda chama hico, Mbowe amesema kumekuwa na mnyukano miongoni mwa wagombea katika nafasi mbalimbali na kuwataka kusameheana.

“Mnapokwenda kupambana na kutafuta nafasi mbalimbali huhitaji kutumia uongo kujenga hoja zako, tumia akili na ukweli kujaribu kujenga hoja itakayokupandisha. Huwezi kuikanyaga na kuitoboa taasisi hii ambayo unataka kuiongoza kesho. Unaiongozaje taasisi uliyoitoboa?” amehoji.

Akionekana kujibu hoja ya mfumo wa fedha, Mbowe amesema kwa historia yake na mambo aliyoyafanya kwenye chama hicho hahitaji kujinadi, huku akisema kila mwanachama na viongozi wanafanya kazi kwa kujitolea.

“Chama hiki hakijajengwa na Serikali, hakijajengwa na wizi wa mashirika ya umma, chama hiki kimejengwa na kipato cha Mtanzania mmoja mmoja, wote mmejinyima viongozi. Lakini mimi nimepewa sifa kwamba peke yangu naleta mzigo?…Kama unaona tupimane kwa mizigo tupimane,” amesema.

Mbowe akionyesha kusaka suluhu kwa mvutano uliopo katika uchaguzi huo, ametumia mfano wa Biblia uliotumiwa na Mfalme Suleiman aliyeamua kesi ya wanawake wawili waliokuwa wakigombea mtoto kwa kuamuru mtoto huyo akatwe katikati, lakini baadaye mama mwenye mtoto alipinga akiomba mtoto huyo alelewe na hasimu wake.

Amewataka wanachama wanaunga mkono kila upande kutokanyaga wenzao na kutangaza msamaha.

Katika hilo, Mbowe amesema hatawania nafasi ya uenyekiti kwenye mvutano utakaotishia kukipasua chama hicho. “Nitaingia kwenye vita itakayokijenga chama chetu.”

Akionekana kujibu hoja ya ukomo wa madaraka, Mbowe amesema amekuwa akipata maoni kutoka kwa familia yake inayomtaka aachane na uongozi wa chama hicho, lakini wakati huohuo, amekuwa akipata maoni ya familia ya Chadema.

“Hakuna kipindi familia yangu imenikalia mguu pande kama kipindi hiki, wananiambia ‘baba inatosha, toka achana na siasa rudi nyumbani uendelee na maisha mengine.

“Sasa familia yangu nayo ina nguvu katika maisha yangu, lakini vilevile na familia ya Chadema nayo ina nguvu,” amesema.

Wenyeviti wa mikoa waapa kumlazimisha

Awali, akizungumza katika kusanyiko hilo, Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Iringa, William Mungai aliyewawakilisha wenyeviti wa mikoa 24, ametaja hoja tano za kwa nini wanataka Mbowe aendelea kuongoza chama hicho kwa miaka mitano ijayo.

Hoja hizo ni pamoja na ubunifu, kuijenga Chadema, mfano bora, mshikivu na mshirikishaji, wakisema wanamuhitaji Mbowe kwa sababu ni jenerali anayekuwa mstari wa mbele kuongoza mapambano.

Amesema kutokana na hoja hizo, wameamua kumuunga mkono, wakisema bado ana nguvu, hivyo watamchukulia fomu ya kugombea nafasi hiyo.

“Tumeamua tuje kukutia moyo na kukupongeza, bado una nguvu na kufanya mikutano, sasa tutakuwa vichaa kama tutakuacha.Tunataka uendelee kuwa mwenyekiti kwa sababu tuna hoja utake, usitake tunakwenda kukuchukulia fomu,” amesisitiza Mungai.

Hali ilivyokuwa nyumbani kwa Mbowe

Tangu leo asubuhi wanachama na wapenzi wa Chadema wakiwa na magari, pikipiki na wengine waliofika kwa miguu nyumbani kwa Mbowe, Mtaa wa Mwanamboka au nyumbani kwa Mbowe, Mikocheni.

Hata hivyo, mambo yalikwenda kinyume baada ya tukio hilo kusogezwa mbele hadi mchana kutokana na sababu mbalimbali, ikiwemo kuwasubiri viongozi na makada wengine waliokuwa wakitoka maeneo mbalimbali.

Licha ya mvua kubwa kunyesha makada na viongozi Chadema, wakiwemo wa wilaya waliendelea kumiminika na wengine hawakujali kuloana, badala yake walisikika wakisema, “tumekuja kumsikiliza ‘mwamba atoe kauli.”

Ilipofika saa saba mchana umati wa wanachama uliongezeka, hatua iliyowalazimu wengine kubaki nje ya nyumba ya Mbowe ambapo waliwekewa turubali maaalumu na viti kwa ajili ya kumsubiri Mbowe.

Kama hiyo haitoshi, zilifungwa runinga tatu katika turubali hilo kwa ajili ya kuwawezesha wanachama kufuatilia tukio hilo moja kwa moja wakiwa wameketi nje ya nyumba hiyo.

Mwananchi ilishuhudia zaidi magari matano ya Toyota Coaster yaliyokuwa yamebeba viongozi na makada wa Chadema waliowasindikiza wenyeviti wa mikoa 23 waliokwenda kwa Mbowe kumshawishi agombee.

Miongoni mwa wenyeti wanaomuunga mkono Mbowe wanatoka mikoa ya Shinyanga, mikoa ya kichama ya (Temeke, Kinondoni), Arusha, Simiyu, Dodoma, Morogoro, Tanga, Manyara, Kilimanjaro, Pemba, Mwanza na Kagera.

Baada ya Mbowe kuzungumza, Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Shinyanga, Emmanuel Ntobi amesema, “tumefurahi na kufarijika majibu ya kwamba atatoa uamuzi wa ombi ndani saa 48. Tunavyoona kwa umma na wapigakura tuliowawakilisha inaonyesha mwenyekiti atakubaliana ombi letu.”

Mathayo Torongey, Mwenyekiti wa Chadema Wilaya ya Bagamoyo Mkoa wa Pwani amesema, “Tumekuja kusindikiza viongozi wetu wa mkoa wana jambo lao hapa. Ujumbe ulioletwa kwako   mwenyekiti wanaomba usiukatae utawaumiza watu wengi waliofika leo.”

Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake la Chadema (Bawacha) Kanda ya Pwani, Rose Moshi, amesema, “sisi wanawake tunaungana nanyi kumsihi Mbowe akubalia kuchukua fomu ya kuwania uenyekiti.Tuna sababu ya kumuomba moja, ni mtu imara, amepitia nyakati ngumu lakini hakuwahi kuyumba.”

“Katika miaka 20 Chadema imekuwa na mafanikio makubwa, tuna kila sababu kukuomba uendelee sisi tutakuchangia Sh1.5 milioni ili uchukue fomu,” amesema Moshi.

Mwenyekiti wa Chadema mkoa wa Kinondoni, Henry Kileo amesema baadhi amesema wanaunga kila hatua iliyofanywa na wenyeviti wenzao kuhusu kumshawishi Mbowe kuwania uenyekiti.

“Lazima misheni ikamilike, lazima mwamba amalizie kuiondoa CCM madarakani hilo anaweza,” amesema Kileo.

Related Posts