KAGERA Sugar imeanza msako mapema katika harakati za kukiboresha kikosi chao ikisaka wachezaji wa nne waliotokana na ripoti ya kocha wao Melis Medo.
Medo amewasilisha ripoti yake ya maboresho kwa mabosi wa juu wa Kagera, huku akitaka walima Miwa hao kumpa nafasi ya kuongeza wachezaji wanne kupitia dirisha dogo la usajili watakaokuja kuongeza nguvu.
Kwenye ripoti hiyo ambayo Mwanaspoti imepenyezewa na mabosi wa juu wa Kagera, Ni kwamba Medo anahitaji kipa wa maana atakayekuja kusaidiana na makipa wawili Ramadhan Chalamanda na Said Kipao.
Mbali na kipa huyo pia ripoti hiyo ya Medo inahitaji beki mmoja wa kushoto na washambuliaji wawili wenye ubora mkubwa ambapo wachezaji hao wote wawe wazawa.
“Tunataka kuwapata wazawa ambao wana uzoefu tunaoamini uwezo wao utakuja kuongeza kitu wakichanganyika na Hawa tutakaowabakiza,”alisema bosi wa juu wa Kagera Sugar.
“Tumeshaanza kuzungumza na baadhi ya wachezaji ambao kocha amewapendekeza na kila kitu kinakwenda sawasawa kutokana na klabu wanazozichezea zinataka kuwatoa kwa mkopo.”
Kagera Sugar ipo eneo la hatari kwenye msimamo wa Ligi wakishikilia nafasi ya 14 wakiwa na pointi 11 ambapo hesabu zao ni kujiondoa hapo ili isizidishe hesabu za kuweza kushuka daraja.