Morogoro. Tayari miili mingine mitano ya waliokufa kwenye ajali iliyohusisha gari la abiria na lori la mizigo mkoani Morogoro, imetambuliwa na ndugu zao jioni hii katika Hospitali ya Rufaa mkoani Morogoro.
Kutambuliwa huko kunafanya idadi ya miili iliyotambuliwa kufikia 10 kati ya 15 ya waliokufa kwenye ajali hiyo liyotokea usiku wa kuamkia leo Jumatano, Desemba 18, 2024 eneo la Mikese.
Akizungumza na Mwananchi Digital usiku huu, Mganga Mkuu Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Morogoro, Dk Daniel Nkungu amesema miongoni mwa miili iliyotambuliwa ni pamoja na wa mtoto wa kike wa miaka 10, Nurath Rajabu mkazi wa Maseyu.
Dk Nkungu amesema Nurath alifikishwa hospitalini hapo jana usiku akiwa ni miongoni mwa majeruhi lakini alifariki dunia muda mfupi baada ya kuingizwa kwenye chumba cha upasuaji.
“Huyu mtoto alipata majeraha tumboni na mivunjiko kwenye miguu baada ya kufika hapa hospitali tulimkimbiza chumba cha upasuaji, hata hivyo wakati madaktari wanaendelea na upasuaji ghafla moyo ulisimama kufanya kazi, madaktari walijitahudi kuokoa maisha yake lakini kwa bahati mbaya alifariki dunia,” amesema Dk Nkungu.
Taarifa zilizopo zinasema Nurath alikuwa akisafiri na mama yake Veneranda ambaye naye amefariki kwenye ajali hiyo.
Kwa mujibu wa Dk Nkungu amewataja waliotambuliwa kuwa John Paul (25) mkazi wa Tabora, Rehema Juma (35) mkazi wa Jijini Dar es Salaam, Miraji Ramadhani (49) mkazi wa Maseyu na Venelanda Andrea (35) mkazi wa Maseyu.
Amesema baada ya miili hiyo kutambuliwa ndugu wanaendelea na utaratibu wa kuichukua kwa ya mazishi.
Ajali hiyo iliyosababisha vifo vya watu 15 na majeruhi saba ilitokea
usiku wa kuamkia leo katika eneo la Mikese barabara ya Morogoro – Dar es Salaam baada ya basi dogo hilo la abiria lililokuwa likitokea Morogoro kugongana uso kwa uso na lori lililokuwa likitokea Dar es Salaam.