Mpango wa kufuatilia mienendo ya viongozi wa umma kuanza mwakani

Musoma. Serikali imetangaza mpango wa kuanza kufuatilia mienendo na tabia za viongozi wa umma wanapokuwa nje ya ofisi.

Imesema lengo ni kutaka kuhakikisha wanazingatia maadili na kufuata makatazo na viapo vyao kwa mujibu wa sheria.

Ufuatiliaji huo, ambao unatarajiwa kuanza mapema mwaka ujao, unalenga kubaini kama matendo ya viongozi yanalingana na maadili yanayotarajiwa na Watanzania.

Katibu wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Fabian Pokela, ameyasema hayo leo Desemba 18, 2024, mjini Musoma katika mafunzo ya maadili kwa viongozi wa umma.

Amesema ufuatiliaji huo utatoa majibu juu ya hali halisi ya mienendo ya viongozi na hatua stahiki zitachukuliwa kwa mujibu wa sheria kwa wale watakaobainika kukiuka.

Pokela amesema; “Hatuwezi kuweka wazi njia zitakazotumika katika ufuatiliaji huu kwa sasa, lakini matokeo yatakayopatikana yatachunguzwa na hatua za kisheria kuchukuliwa pale itakapohitajika.”

amesisitiza kuwa viongozi wa umma wanawakilisha taswira ya Serikali, hivyo tabia zao zinapaswa kuendana na maadili ya Kitanzania.

Na ameonya kuwa tabia zisizofaa, kama vile matumizi mabaya ya muda katika sehemu zisizofaa, zinadhalilisha Serikali mbele ya wananchi.

Mkuu wa Mkoa wa Mara, Evans Mtambi akifungua mafunzo hayo ametoa wito kwa viongozi kufanya kazi kwa kuzingatia weledi na kuacha mazoea.

“Uadilifu ni zaidi ya sheria. Bila uadilifu, Serikali haiwezi kufanikisha malengo yake,” amesema Mtambi.

Amewaagiza pia wakurugenzi wa halmashauri kutoa mafunzo kwa viongozi wa serikali za mitaa ili kuwajengea uwezo wa kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi na kuendana na kasi ya maendeleo ya Serikali.

Washiriki wa mafunzo hayo wamesema yamekuwa chachu ya uelewa wa namna bora ya kutimiza majukumu yao.

Ofisa Elimu wa Sekondari Wilaya ya Serengeti, Chatta Lukela, amesema mafunzo hayo yamebainisha umuhimu wa kufuata maadili na weledi, huku Diwani wa Mwigobero, Mariam Sospeter, akisisitiza haja ya mafunzo ya mara kwa mara kwa viongozi ili kuboresha utendaji wao.

Mafunzo hayo yameainisha masuala muhimu kama mavazi yanayofaa kwa viongozi wa umma, pamoja na mbinu za kukuza maadili, weledi na uwajibikaji katika utumishi wa umma.

Related Posts