BAADA ya kufanyika tathimini ya washambuliaji wa Yanga kile walichokifanya msimu huu hadi sasa dirisha dogo limefunguliwa, ni wazi uamuzi unaokwenda kufanyika katika eneo hilo hautakuwa na lawama yoyote ile.
Tangu ujio wa Kocha Sead Ramovic aliyetambulishwa kikosini hapo Novemba 15 mwaka huu kuchukua nafasi ya Miguel Gamondi, kumekuwa na majadiliano makubwa ya kuboresha kikosini hicho hasa eneo la ushambuliaji na ulinzi na kunaonekana kuwa na shida kubwa.
Katika ulinzi, tayari Yanga imemsajili kwa mkopo Israel Mwenda hadi mwisho wa msimu huu akitokea Singida Black Stars, pia imefanya mazungumzo ya awali na beki wa kati wa Fountain Gate, Laurian Makame kuangalia uwezekano wa kumpata baada ya kuona ugumu wa kumsajili Lameck Lawi kutoka Coastal Union.
Kwenye suala la kuboresha kikosi, hivi karibuni Mwanaspoti liliripoti mabosi wa timu hiyo wanataka kushusha nyota wapya sita katika eneo la ulinzi, kiungo na ushambuliaji ikiwa ni mapendekezo ya Kocha Ramovic huku ikiendelea kufanyika tathmini ya nyota waliopo.
“Tunafuatilia kwa karibu mchango wa kila mchezaji aliyepo hapa, hatutabaki na mchezaji kwa kutumia historia yake ya nyuma, tutatumia ripoti hizi kufanya maboresho ya kikosi chetu,” alisema kocha huyo.
Maeneo yote hayo yanafanyika maboresho baada ya walipo hivi sasa kuhitaji kuongezewa nguvu ya lazima na golini Djigui Diarra mwenye uhakika wa kuanza kikosi cha kwanza, amewaweka benchi Khomeiny Abubakar aliyecheza mechi tatu za kimashindano msimu huu na Aboutwalib Mshery ambaye hana kabisa nafasi.
Kule mbele panapoonekana kuwa na shida ya kufunga mabao licha ya kwamba timu hiyo ilifanya balaa hatua ya mtoano ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu kwa kufunga mabao 17 katika mechi nne huku ikiwa haijaruhusu nyavu zake kutikiswa, mambo yamebadilika baada ya kuingia makundi na imefunga bao moja pekee na kuruhusu matano.
Ukiachana na kimataifa, michuano ya ndani Yanga kwa kuanza na Ngao ya Jamii, ilifunga mabao matano na kuruhusu moja, hapa ni kipindi ambacho walikuwa moto huku kwenye ligi mechi 11 wakifunga mabao 16 na kuruhusu manne ikiwa ni timu ya pili kwa kuruhusu mabao machache zaidi baada ya Simba (3).
Eneo la ulinzi ukiachana na makipa, mabeki wanaotumika zaidi ni Ibrahim Bacca, Dickson Job, Yao Kouassi na Chadrack Boka huku Bakari Mwamnyeto akiwa kama mbadala eneo la beki wa kati.
Clement Kibabage hivi sasa anacheza wakati Boka anauguza majeraha, wakati Kibwana Shomari angalau siku za karibuni anakaa benchi wakati mwanzo aliishia jukwaani.
Kwa upande wa viungo kuanzia wakabaji hadi wachezeshaji, Khalid Aucho, Maxi Nzengeli, Stephane Aziz Ki, Clatous Chama, Pacome Zouzoua, Mudathir Yahya na Duke Abuya ndiyo wanaopishana sana, huku kwa uchache Aziz Andabwile amehusika kwenye baadhi ya mechi akichezesha beki wa kati.
Salum Abubakar, Shekhan Khamis, Jonas Mkude na Denis Nkane wakiwa hawana uhakika wa namba wakati Farid Mussa majeraha yakimtibulia licha ya kwamba hivi sasa amepona.
Wakati Yanga ikitajwa imekamilisha usajili wa straika, Fahad Bayo raia wa Uganda ili kuimarisha eneo hilo la ushambuliaji, wachezaji wanaocheza eneo hilo, Clement Mzize, Kennedy Musonda, Prince Dube na Jean Baleke, wanaweza kuhukumiwa kwa namba zao kwani nyingi zinaonekana kuwakataa.
Katika mashindano yote msimu huu wakati Yanga ikicheza mechi 20, amecheza mechi 17 huku akiwa na mchango wa mabao sita aliyofunga na Ligi Kuu Bara (2), Ngao ya Jamii (1) na Ligi ya Mabingwa Afrika (3).
Mzize ambaye ni straika mzawa, anaweza kukwepa panga hilo kutokana na faida mbili, uzawa wake, pia umri kwani bado ana miaka 20 akiendelea kujengwa kuja kuwa bora zaidi na kuisaidia timu hiyo. Ukiangalia takwimu zake za ligi, amecheza mechi 10 kati ya 11 kwa dakika 636, huku Ligi ya Mabingwa akicheza mechi tano kwa 224.
Ni mshambuliaji ambaye alitajwa kipindi hiki cha dirisha dogo anaweza kukatwa kwani hakuanza vizuri, lakini kiwango bora alichoonyesha akiitumikia timu ya taifa ya Zambia wakati wa kufuzu michuano ya Afcon alipofunga mabao manne, ukafanyika uamuzi wa kuendelea kumpa nafasi zaidi ya kupambania namba huku ikishuhudiwa mechi za karibuni akianza kikosi cha kwanza tofauti na awali alipokuwa akitumika zaidi Prince Dube kipindi cha Gamondi.
Musonda katika Ligi Kuu Bara, amecheza mechi nane kwa dakika 232 akifunga mabao mawili, hana asisti wakati kimataifa amecheza mechi sita kwa dakika 277, hana bao wala asisti.
Ndiye mchezaji kwenye nafasi ya ushambuliaji aliyecheza mechi chache zaidi ambazo ni nne kwa dakika 166 akifunga bao moja pekee, hana asisti. Taraifa zinaeleza kipindi hiki cha dirisha dogo ataondolewa kikosini hapo kwani ameshindwa kutoa changamoto ya namba kwa wenzake.
Hana bao kwenye ligi zaidi ya asisti moja, lakini kimataifa ana mabao manne msimu huu likiwemo moja hatua ya makundi alilofunga katika sare ya 1-1 dhidi ya TP Mazembe. Huko kimataifa, amecheza mechi zote saba ambazo Yanga imecheza tangu hatua ya awali kwa dakika 306. Upande wa ligi, dakika zake ni 446 akicheza mechi 10 kati ya 11.
Ingawa namba za kwenye ligi kumkataa, lakini Dube alianza vizuri msimu huu hasa Ngao ya Jamii akifanikiwa kutoa asisti moja waliposhinda 1-0 dhidi ya Simba, kisha akafunga bao moja walipoichapa Azam 4-1 na kubeba taji hilo.