*Ni ule wa kuwarudisha sekondari watoto waliopata matatizo mbalimbali ikiwemo ujauzito
Na Mwandishi wetu
WAHITIMU wa Taasisi ya Elimu ya Watu wazima wamempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kurudisha Mpango unaojulikana kama Sequip ambao unawasaidia kuwarudisha sekondari watoto waliopata matatizo mbalimbali ikiwemo ujauzito.
Pongezi hizo zilitolewa Jijini Dar es Salaam wakati wa Mahafali ya 63 ya Taasisi hiyo yaliyofanyika katika ukumbi wa Mwalimu Nyerere.
Mmoja wa wahitimu Mwalimu Kassim Mswahili alisema wanamshukuru Mungu kwa kuhitimu salama na pia wanampongeza sana Rais Samia kwa kuona umuhimu wa kurudisha mpango huo kwani vijana wengi walipata changamoto hizo na badaye kukosa fursa mbalimbali za kikazi.
“Tunampongeza Rais wetu kwa kuona umuhimu katika hili na tuwashukuru pia wafadhili ambao ni benki ya Dunia ambapo mpaka tunaongea hivi sasa vituo viko Nchi nzima vya binafsi na Serikali kwenye Sekondari,”alisema Mwalimu Mswahili na kuongeza;
“Lakini wadau tuendelee kushirikiana kuhamasisha vijana wenye sifa ya kurudi shule kusoma elimu ya sekondari basi wafanye hivyo kwani walioko nje na hawajapata uelewa ni wengi,”.
Hata hivyo alisema kuwa kwa hali inavyoendelea lazima uhamasishaji uendelee kwani jamii haitaepuka elimu ya watu wazima kwani kila mtu ambaye hakupata elimu na anahitaji mafanikio lazima apitie huko.
Naye muhitimu mwingine Van Matimbe, alisema kuwa kwenye jamii upo umuhimu wa kuendelea kuhamasisha watu kwenda kusoma elimu ya watu wazima.
“Jambo hili ni jema na la kufurahisha kwani mnajikuta watu wazima wenye familia zenu mmekusanyika kwa pamoja na kumbuka kila mtu anamajukumu yake na ukiwa unasoma changamoto zinaongezeka hivyo bidii na uvumilivu vinahitajika,” alisema Matimbe.
Mwalimu Mswahili akimulisha keki rafiki katika mahafali ya 63 ya Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima jijini Dar es Salaam.