KOCHA wa Coastal Union, Juma Mwambusi amefunguka kuwa changamoto kubwa ambayo anazidi kupambana nayo katika timu hiyo ni upungufu katika safu ya ushambuliaji.
Coastal juzi ilimaliza duru la kwanza wa Ligi Kuu Bara kwa kutoka sare ya 1-1 na Tabora United ugenini kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, uliopo Tabora.
Matokeo ambayo imeifanya kushika nafasi ya 10 baada ya mechi 15, ikikusanya pointi 17 zilizotokana na ushindi wa mechi nne, sare tano na kupoteza sita ikiwamo kufunga mabao 15 na kufungwa 16.
Mwambusi anayepambana kuiweka timu katika mbio za ubingwa wa msimu ili kuvuka ile ya msimu uliopita ilipomaliza nafasi ya nne alisema anaendelea kupambana nayo bila kuchoka kama kocha akikomaliza zaidi safu ya ushambuliaji.
“Naamini mambo yanaenda taratibu, inatakiwa wachezaji wangu wanielewe hili tutimize tunachokipambania,” alisema na kuongeza kuwa wamekuwa wakitengeza nafasi nyingi, lakini zinazotumika ni chache hivyo wanafanyia kazi jambo hilo.