Arusha. Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Mtume Boniface Mwamposa wa Kanisa la Inuka Uangaze na Kampuni ya Utalii ya Leopard Tours kwa pamoja wametoa pikipiki 60 kwa Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha kwa lengo la kuimarisha usalama na kukuza utalii.
Pikipiki hizo zimekabidhiwa leo Jumatano Desemba 18, 2024 kwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda ambaye amewashukuru wadau hao kwa kuendelea kulisaidia Jeshi la Polisi akiahidi pikipiki hizo zitatumika kuimarisha usalama.
Makonda amesema Jeshi la Polisi linafanya kazi usiku na mchana ingawa hakuna watu wanaojitokeza kulipongeza, ila pale kunapokuwa na dosari hulinyooshea kidole.
“Wakati mwingine wanafanya kazi katika mazingira magumu wakiwa na changamoto ya vitendea kazi, mimi nikasema ili nipate nguvu ya kuwalaumu, acha niwatafutie kwanza vitendea kazi, ili baadaye niulize kwa nini hiki kitu hakifanyiki na tuna kila kitu,”amesema mkuu huyo wa mkoa.
Amesema kati ya pikipiki hizo 60, kila taasisi imetoa pikipiki 20.
Kwa upande wake Meneja Uhusiano na Elimu kwa Umma wa NSSF, Lulu Mengele amesema baada ya kupokea ombi kutoka ofisi ya mkuu huyo wa mkoa wameamua kushiriki kwa sababu ya umuhimu wa Jeshi la Polisi.
“Kwa kulisaidia Jeshi la Polisi tukasema hata wanachama wa NSSF watakuwa salama na kuendelea kufanya shughuli mbalimbali za kuwapatia kipato na kuendelea kuchangia kwenye mfuko,” amesema Lulu.
Naye Mtume Mwamposa amesema jambo hilo ni muhimu kwa kuwa kila wanaposikia mkuu huyo anazungumzia usalama wa mkoa wake, nao wameamua kumuunga mkono kwa kuchangia.
“Na mimi kwa kujua umuhimu wa kazi za Polisi wetu nikasema hili jambo linalozungumzwa na mkuu wa mkoa lazima na sisi tuweke mkono wetu, nikasema hata kama niko Dar es Salaam najua kazi ya Polisi, najua usalama maana yake nini katika miji yetu,”amesema Mwamposa na kuongeza;
“Tunafanya mikutano mikubwa, polisi ndiyo watu ambao wanahangaika huku na kule kusimama na sisi ili kuhakikisha raia wako salama. Sisi tunashukuru tumetoa pia pikipiki 20 lakini wakati ukifika tena, tutafanya vitu vingine na huyu akifanya hivi, yule akafanya vile taifa litakuwa salama.”
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Justine Masejo ameshukuru kwa msaada huo na kueleza kuwa Makonda alipowasili mkoani humo alizungumza nao na kuwauliza mahitaji yao.
“Tulikueleza mahitaji yetu ni vifaa ukatuahidi, hizi pikipiki ni awamu ya pili na tunazo zaidi ya 100.Wewe umetimiza sehemu yako naomba na mimi na askari wangu tutimize sehemu yetu ambayo tumeahidi, tunashukuru wadau kwa msaada huu,” amesema Kamanda Masejo.