NEWZ ALERT: WATU 14 WAFARIKI DUNIA, SABA WAJERUHIWA KWA AJALI YA GARI MOROGORO

Watu 14 wamefariki dunia na wengine saba kujeruhiwa baada ya gari kubwa la mizigo kugongana uso kwa uso na gari dogo la abiria majira ya saa 2 usiku eneo la Mikese Mkoani Morogoro.

Kwa mujibu wa Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro Dkt. Daniel Nkungu wakati akiongea na waandishi wa Habari Disemba 17, 2024 hospitalini hapo amesema, hospitali hiyo imepokea majeruhi 7 na miili ya watu 14 waliofariki katika ajali hiyo ambapo 8 kati yao ni wanaume na 6 ni wanawake hiyo ikiwa ni taarifa ya awali.

Akifafanua zaidi, Dkt. Nkungu amesema kati ya majeruhi 7 wanaume ni wanne na watatu ni wanawake na kwa upande wa waliofariki Nane ni wanaume na sita ni wanawake kati yao mwili mmoja ni wa mtoto.

“.. Hapa Hospitalini tumepokea majeruhi 7 na miili ya watu 14 waliofariki….kati yao miili 8 ya wanaume na miili 6 ya wananwake.” Amesema Dkt. Daniel Nkungu.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima aliyefika hospitalini hapo mara tu baada ya ajali, ametoa pole kwa watanzania wote kwa kuondokewa na watanzania wenzetu 14 kutokana na ajali hiyo, huku akiwasisitiza madereva kufuata sheria za barabarani ili kuepusha ajali zisizo za lazima kutokea.

Related Posts