Ufaransa yapeleka misaada zaidi Mayotte baada ya kimbunga – DW – 18.12.2024

Tani 120 za chakula zinatarajiwa leo kusambwazwa kwa waathirika wa kimbunga hicho wanaokabiliwa na njaa na hatari ya magonjwa. Rais Emmanuel Macron anatarajiwa kufika katika kisiwa hicho siku ya Alhamisi.

Serikali ya Ufaransa imetuma msaada kwa ndege kupitia kisiwa cha Reunion. Tani 100 za chakula zinatarajiwa kutolewa leo katika kisiwa kikubwa cha Grande Terre na tani nyengine 20 katika kisiwa kidogo cha Petite-Terre.

Wafanyakazi visiwani humo wamesema wanajitayarisha kwa janga kubwa la magonjwa kufuatia miili ya watu kutapakaa barabarani bila kufunikwa na watu wanapata tabu kupata maji safi ya kunywa.

Soma pia: Waokoaji wawatafuta manusura wa kimbunga kisiwani Mayotte

Hadi sasa serikali imetangaza vifo vya watu 22 huku zaidi ya watu 1,400 kujeruhiwa vibaya  kutokana na kimbunga hicho, kilichopiga eneo hilo lililochini ya Ufaransa na kusababisha uharibifu wa majengo, miundombinu ya nishati na mawasiliano.

Waziri Mkuu wa Ufaransa Francois Bayrou
Waziri Mkuu wa Ufaransa Francois Bayrou Picha: Bestimage/IMAGO

Waziri Mkuu wa Ufaransa Francois Bayrou ameonya kuwa idadi ya waliokufa na kujeruhiwa huenda ikapanda zaidi kutokana na baadhi ya miili kuhofiwa kukwama chini ya vifusi vya majengo yaliyoporomoka.

” Idadi ya mwisho haijatolewa. waliokufa wanakadiriwa kuwa zaidi ya ishirini, huku wengine 1,500 wakijeruhiwa vibaya. Sote tunajua kwamba idadi hii ya vifo inaweza kuongezeka, na sote tuna wasiwasi juu ya hatima ya wale walioathirika na janga hili na wale ambao hakuweza kulindwa. “

Juhudi za uokoaji zinaendelea

Kwa sasa waokoaji bado wanaendelea kuwatafuta manusura. Licha ya maafa na hasara inayoshuhudiwa katika kisiwa hicho cha Mayotte pia kumeripotiwa uporaji mkubwa kisiwani humo na serikali imeweka marufuku ya kutoka nje usiku ili kukabiliana na hali hiyo.

Rais wa Ufaransa  Emmanuel Macron  amesema kilichotokea Mayotte ni janga huku akitangaza jana jioni kwamba atakitembelea kisiwa hicho siku ya alhamisi akikatisha ziara yake mjini Brussels kukutana na viongozi wa Umoja wa Ulaya.

Vikosi vya uokoaji vikiendelea na kazi huko Mayotte
Vikosi vya uokoaji vikiendelea na kazi huko MayottePicha: Chafion Madi/REUTERS

Amesema ziara hiyo ni ya kuwafariji na kuwaunga mkono raia wake, maafisa na mashirika ya kutoa huduma muhimu. Macron pia alisema anapanga kutangaza kipindi cha maombolezo cha kitaifa akiwa kisiwani humo. 

Waziri wa mambo ya ndani wa Ufaransa Bruno Retailleau, aliyekitembelea kisiwa hicho siku ya Jumatatu akisema asilimia 70 ya wakaazi wameathirika kwa kimbunga hicho.

Soma pia: Maelfu wahofiwa kufa kwa kimbunga Mayotte

Hata hivyo wanasiasa wa upinzani wameikosoa serikali kwa kile walichosema ni kukipuuza kisiwa cha Mayotte na kushindwa kujipanga kukabiliana na majanga asilia yanayohusishwa na mabadiliko ya tabia nchi.

Mayotte ni kisiwa masikini kilicho chini ya himaya ya Ufaransa huku thukuthi moja ya idadi jumla ya watu wanaishi katika maeneo duni huku nyumba zao zikiwa hafifu zisisoweza kustahamili kishindo cha dhoruba kali.

Kimbunga Chido chaua watu wengi Mayotte

To view this video please enable JavaScript, and consider upgrading to a web browser that supports HTML5 video

(Vyanzo: AP, AFP, Reuters)

 

Related Posts