Utafiti: Wasomi hawachangamkii mikopo ya asilimia 10 isiyo na riba

Musoma. Wahitimu wa vyuo vikuu nchini, hasa vijana, wamehimizwa kuchangamkia fursa ya mikopo isiyokuwa na riba inayotolewa na Serikali kupitia halmashauri kwa lengo la kujiajiri na kuondokana na dhana potofu kwamba inawalenga watu wasiosoma.

Aidha, vyuo vikuu vimetakiwa kuwekeza katika mitalaa inayolenga kukidhi mahitaji ya jamii na inayotekelezeka kwa ufanisi.

Hayo yamesemwa leo Jumatano Desemba 18, 2024 wakati wa uwasilishaji wa matokeo ya utafiti uliofanywa na Chuo Kikuu cha Mwalimu Julius Nyerere cha Kilimo na Teknolojia (MJNUAT) juu ya changamoto za mikopo inayotolewa na halmashauri nchini.

Utafiti huo umeangazia nini kifanyike ili mikopo hiyo iweze kuwa na matokeo chanya katika maendeleo ya  jamii.

Wakizungumza katika warsha ya kupokea matokeo hayo, baadhi ya washiriki wamesema mikopo hiyo inaweza kutumika kama suluhisho la ukosefu wa ajira nchini endapo itatumiwa vema na wahitimu wa elimu ya juu nchini hasa vijana.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti mkoani Mara, Maulidi Madeni amesema kwa sasa vijana bado hawajaweza kunufaika na fursa za mikopo hiyo kutokana na dhana iliyojikita vichwani mwao, kuwa ni maalumu kwa makundi ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu ambao hawajapata nafasi ya kujiendeleza kielimu, jambo ambalo sio kweli.

Akitoa matokeo ya utafiti huo, Mhadhiri Mwandamizi na Mratibu wa uandaaji wa mitaala wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Kampasi ya Duce, Dk Hezron Onditi amesema kuwepo kwa mitalaa inayojibu changamoto za jamii ni hatua muhimu katika kufanikisha dira ya maendeleo ya taifa.

“Bado kuna changamoto katika mitalaa ya vyuo vyetu, hali inayosababisha wahitimu, wakiwemo vijana, kushindwa kutumia elimu yao kujiajiri, badala yake, wengi wanategemea ajira rasmi, ilhali kuna fursa nyingi zinazoweza kutumiwa kujiajiri, kama vile mikopo ya asilimia 10,” amesema Dk Onditi.

Utafiti huo unaonyesha kuwa iwapo vyuo vitaandaa mitalaa inayolenga kutatua changamoto za jamii, ikiwemo tatizo la ukosefu wa ajira, wahitimu wataweza kuanzisha miradi ya kujiajiri na hata kuwaajiri wengine.

Ameongeza kuwa, mitalaa inapaswa kumfanya mhitimu kuwa mbunifu, mwenye maono na uwezo wa kutumia fursa zilizopo kuibua ajira. Hata hivyo, amesema kwa sasa, wahitimu wengi wanakosa uwezo huo kwa sababu ya kasoro katika mitalaa inayotumika.

“Suala la mafunzo kwa vitendo linapaswa kupewa kipaumbele. Wanafunzi wanatakiwa kufanya mafunzo ya vitendo kwa muda mrefu zaidi, kwani utafiti unaonyesha kuwa nafasi ya mafunzo ya vitendo ni ndogo kwa sasa. Hii inasababisha waajiri kulazimika kuwapa wahitimu mafunzo ya ziada kwa sababu wanakuwa na ujuzi hafifu katika masuala waliyosomea,” amesema Dk Onditi.

Kwa upande wake, Mhadhiri Msaidizi wa Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine, Aika Aku amesema utafiti huo umebaini pia kuwa ukosefu wa elimu kwa wanufaika wa mikopo ni moja ya changamoto kubwa.

“Hili pia linasababisha washindwe kusimamia miradi yao na hujikuta miradi yao inakwama kuendelea,” amesema.

Ameshauri Serikali kuweka utaratibu wa kutoa mafunzo kwa wanufaika wa mikopo juu ya namna ya kuendesha miradi na biashara kabla na baada ya kupokea mikopo.

Pia, amependekeza kuongeza kiwango cha mkopo kulingana na aina ya biashara au mradi husika, badala ya kuweka kiwango cha jumla kwa waombaji wote.

“Kwa mfano, unapotoa Sh2 milioni au milioni 5 bila kuzingatia mahitaji ya mradi husika, hii haifai. Kuna miradi inayohitaji kiasi kikubwa zaidi cha fedha na mafunzo kwa wanufaika ni muhimu ili miradi iwe endelevu na yenye manufaa kwa jamii,” amesema Dk Aku.

Akifungua warsha hiyo, Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara, Gerald Kusaya amesema matokeo ya utafiti huo yamekuja wakati muafaka, kufuatia hatua ya Serikali kufungua dirisha la mikopo hiyo baada ya kusitishwa kwa muda kwa ajili ya maboresho.

Kusaya amesema mikopo hiyo inalenga kuinua kiuchumi makundi ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.

Aidha, amesema kuwa utafiti kama huo una mchango mkubwa katika kufanikisha malengo ya Serikali, kwa sababu tatizo la ukosefu wa ajira ni changamoto ya bara zima la Afrika.

Related Posts