Mpwapwa. Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa, Dk Sophia Kizigo ameongoza waombolezaji kuuaga miili ya maaskari polisi wawili waliouawa kwa kupigwa risasi na mtuhumiwa wa unyang’anyi wa kutumia silaha, wakiwa kwenye operesheni ya kumkamata.
Akitoa salamu kwa waombolezaji leo Desemba 19, 2024, Dk Kizigo amelaani tukio hilo akisema jamii inapaswa kulikemea kwa nguvu zote ili kuondoa matukio ya aina hiyo.
Amewataka wananchi kushirikiana na Jeshi la Polisi kufichua wahalifu waliopo katika maeneo yao.
“Tukio kama hili si la kuvumilia. Lazima tushirikiane kuhakikisha wahalifu hawapati nafasi katika jamii yetu,” amesema.
Kamishna wa Utawala na Rasilimaliwatu wa Jeshi la Polisi, Tatu Jumbe aliyemwakilisha Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Camillus Wambura amelaani mauaji ya askari hao, akisisitiza umuhimu wa jamii kufichua wahalifu katika mitaa yao.
Amewataka askari kuendelea kuchukua tahadhari wanapokuwa kazini, hasa katika mazingira hatarishi.
“Nawasisitiza askari wetu kuendelea kuwa waangalifu na kutumia weledi wenu kila mnapokuwa kazini. IGP, Camillus Wambura amenituma niwaambie msikate tamaa na endeleeni kutimiza wajibu wenu kwa haki,” amesema.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Kamishna Msaidizi Mwandamizi, George Katabazi amesema tukio hilo ingawa ni la kusikitisha, halitawavunja moyo katika jitihada za kupambana na uhalifu.
Baadhi ya wananchi wa Mpwapwa, akiwemo Mwenyekiti wa Mtaa wa Igovu, Elieza Mwaluko wameeleza kushtushwa na tukio hilo, wakisisitiza umuhimu wa kufuata sheria na kushirikiana na vyombo vya dola kudumisha amani.
Koplo Jairo Kalanda na Konstebo Alfred John waliuawa katika mapambano ya risasi Desemba 18, walipokwenda kumkamata mtuhumiwa Atanasio Malenda (30), nyumbani kwake katika Kijiji cha Msagali, wilayani Mpwapwa.
Kamanda Katabazi alisema jana Desemba 18 kuwa tukio hilo lilitokea saa saba usiku.
Alisema alikuwa akituhumiwa kwa unyang’anyi wa kutumia silaha na kumjeruhi Yohana Lameck, kisha kumpora Sh2 milioni.
Katika majibizano ya risasi, alisema mtuhumiwa alipata majeraha na baadaye alifariki dunia alipokuwa akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Wilaya ya Mpwapwa.
Alisema askari mwingine, Koplo Msuka na raia mmoja, Masima Nyau walijeruhiwa katika tukio hilo na wanaendelea kupatiwa matibabu katika Hospitali ya Wilaya ya Mpwapwa.
Kamanda Katabazi alisema polisi walipata taarifa za kuwepo kwa mtuhumiwa nyumbani kwake na walifika kijijini hapo wakiongozana na uongozi wa kijiji.
Hata hivyo, mtuhumiwa alitoka ndani na kuanza kuwashambulia na katika majibizano ya risasi askari hao waliuawa.