Mshambuliaji wa Simba, Lionel Ateba amebakisha mabao mawili tu kumfukia kinara wa ufungaji kwenye Ligi Kuu ya NBC, Elvis Rupia baada ya jana kuiongoza timu yake kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Kengold, katika Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam.
Mshambuliaji huyo raia wa Cameroon, aliibuka shujaa wa Simba baada ya kuifungia mabao yote mawili yaliyoiwezesha kuvuna pointi tatu muhimu katika mechi hiyo na kuisogeza hadi nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi ikifikisha pointi 31 lakini kwa Ateba binafsi yamemfanya abakize mabao mawili kumfikia Rupia anayeongoza chati ya kufumania nyavu akiwa na mabao saba.
Ateba aliifungia Simba bao la kuongoza katika dakika ya 35 lililotokana na mkwaju wa penalti iliyotolewa baada ya Awesu Awesu kufanyiwa faulo ndani ya eneo la hatari na mmoja wa walinzi wa Kengold.
Awesu alipokea pasi kutoka kwa Kelvin Kijiri akiwa ndani ya eneo la hatari la Kengold na Ateba hakufanya ajizi kufunga penalti hiyo.
Dakika 10 baadaye, Ateba aliihakikishia Simba bao la pili baada ya kuunganisha kwa kichwa mpira wa kona uliochongwa na Valentine Nouma.
Baada ya kuingia kwa mabao hayo, Kengold ilionekana kuongeza nidhamu na juhudi zaidi katika kujilinda kwa kujaza idadi kubwa ya wachezaji mbele ya lango lake jambo lililoinyima Simba kuongeza idadi ya mabao hadi filimbo ya mwisho ya mchezo ilipopulizwa ingawa timu hiyo ya Mbeya ilishambulia mara kadhaa lango la Simba lakini haikuambulia angalau bao la kufutia machozi.
Nyota wa Kengold aliyeibeba vilivyo safu ya ulinzi ya timu hiyo na kuiwezesha isikutane na kipigo kizito kutoka kwa Simba jana ni kipa Castor Mhagama ambaye aliokoa hatari nyingi zilizoelekezwa langoni mwake na wachezaji wa Simba.
Katika mchezo huo, Simba katika kipindi cha pili iliwatoa Mzamiru Yassin, Fabrice Ngoma, Ladack Chasambi, Kelvin Kijili na Awesu Awesu ambao nafasi zao zilichukuliwa na Mohammed Hussein, Charles Ahoua, Yusuph Kagoma, Joshua Mutale na Augustine Okejepha.
Kichapo cha jana kimeifanya Kengold ibakie na pointi zake sita ilizokusanya katika mechi 15 na inaendelea kushika mkia katika msimamo wa Ligi Kuu.