Banda avunja mkataba Baroka | Mwanaspoti

BEKI Mtanzania, Abdi Banda amevunja mkataba na Baroka FC ya Afrika Kusini ikiwa miezi mitatu tangu ajiunge na timu hiyo inashiriki Ligi ya Championship.

Nyota huyo mara ya kwanza alijiunga na Baroka akitokea Simba Julai 12, 2017 na sasa amerejea tena baada ya awali dili lake la kujiunga na Singida Black Stars ya Ligi Kuu Bara iliyokuwa inamtaka kugonga mwamba mwanzoni mwa msimu huu.

Akizungumza na Mwanaspoti, Msimamizi wa mchezaji huyo, Fadhili Omary Sizya alisema Banda amevunja mkataba kwa makubaliano ya pande zote mbili ili kutafuta changamoto sehemu nyingine.

Aliongeza kuwa sio muda sahihi kuzungumzia kiasi cha fedha alichokilipa Banda lakini kwa sasa ni mchezaji huru baada ya kumalizana na timu hiyo.

“Amevunja mkataba na Baroka na sasa ni mchezaji huru, ni makubaliano ya pande zote mbili kiufupi aliufuata uongozi akailipa timu hadi Desemba yuko huru sababu ya kufanya hivyo anataka kupata changamoto sehemu nyingine,” alisema Sizya na kuongeza

“Baroka wanafahamiana vizuri kwa hiyo ni makubaliano ya pande mbili, zipo timu kadhaa Tanzania zimetuma ofa na anaweza kusaini kati ya timu mojawapo.”

Bekii huyo mwenye uwezo wa kumudu kucheza kama beki wa kati, kushoto na hata kiungo mkabaji kabla ya Baroka alizitumikia Richards Bay na Chippa United, Highlands Park na TS Galaxy za Afrika Kusini huku Tanzania akiichezea Simba na Coastal Union.

Related Posts