Diarra ashtua Yanga, Maxi, Chama majanga

YANGA imekuwa ikipitia kipindi kigumu kwa siku za karibuni baada ya kukosa matokeo mazuri kwenye mechi zake huku Ligi ya Mabingwa Afrika ikiburuza mkia Kundi A baada ya kukusanya pointi moja ikishuka dimbani mara tatu.

Watetezi hao wa Ligi Kuu Bara na washindi mara nyingi wa taji hilo walilobeba mara 30, ukiachana na matokeo ya uwanjani, wamepata pigo jipya likiwamo la kumkosa kipa namba moja, Diarra Djigui kwa muda wa zaidi ya mwezi mmoja ikiwamo mechi mbili kati ya tatu zilizobaki za kimataifa za Ligi ya Mabingwa Afrika.

Kwa sasa kikosi hicho kinakabiliwa na michezo minne ya Ligi Kuu Bara itakayochezwa ndani ya siku 10 kuanzia leo Alhamisi, Desemba 19 hadi Desemba 29, 2024. Mbali na michezo hiyo, pia kuna ile mitatu ya marudiano hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa Afrika kuwania kufuzu robo fainali ambapo miwili nyumbani dhidi ya TP Mazembe na MC Alger na ugenini dhidi ya Al Hilal.

Katika mechi hizo nne za kufunga mwaka na kuhitimisha duru la kwanza wa Ligi Kuu, Yanga inatarajiwa kukosa huduma ya kipa wao namba moja Djigui Diarra.

Diarra ambaye amefanikiwa kucheza mechi tisa za Ligi Kuu Bara msimu huu kati ya 11 na kukusanya clean sheet saba, imeelezwa anatarajiwa kukaa nje ya uwanja kwa takribani wiki 4 hadi sita kutokana na majeraha aliyoyapata.

Taarifa kutoka ndani ya Yanga, ambazo Mwanaspoti imezinasa zinasema kuwa, Diarra ameumia misuli ya kigimbi cha mguu wa kulia, hivyo matibabu yake yatachukua muda mrefu kidogo.

“Aliumia katika mchezo uliopita dhidi ya TP Mazembe hivyo anahitaji matibabu ya kina kutibu tatizo hilo ambapo itachukua wiki nne hadi sita kurejea uwanjani, lakini kuna namna inafanyika katika matibabu yake ambapo ikifanikiwa inaweza kupunguza muda huo wa kukaa nje na kuwa nusu yake,” alisema mtoa taarifa huyo.

Diarra amekuwa mchezaji muhimu katika eneo la lango la kikosi cha Yanga kwani amefanikiwa kwa kiasi kikubwa kuwaweka benchi Khomeiny Abubakar na Aboutwalib Mshery.

Katika mchezo dhidi ya TP Mazembe wa Ligi ya Mabingwa Afrika uliochezwa Desemba 14, mwaka huu na kumalizika kwa sare ya bao 1-1, Diarra aliumia dakika ya 28, akafanyiwa matibabu hadi dakika ya 32, akaendelea na mchezo, lakini hakurejea kipindi cha pili, nafasi yake ikachukuliwa na Khomeiny ambaye huo ulikuwa ni mchezo wa tatu tangu atue Yanga baada ya kucheza miwili ya ligi dhidi ya Coastal Union na Namungo.

Kabla ya Mazembe, Diarra alicheza mechi zote sita za nyuma kuanzia hatua ya awali dhidi ya Vital’O na CBE SA nyumbani na ugenini ambazo zote hakuruhusu bao, kisha mbili za makundi dhidi ya Al Hilal na MC Alger alizoruhusu mabao manne kila mechi akifungwa mawili.

Kuumia kwa Diarra na muda halisi ambao anatarajiwa kukaa nje, ratiba inaonyesha atazikosa mechi sita mpaka tisa ndani ya kipindi hicho cha wiki nne hadi sita.

Kama atakuwa nje kwa wiki nne, atazikosa mechi nne za Ligi Kuu Bara dhidi ya Mashujaa (Desemba 19), Tanzania Prisons (Desemba 22), Dodoma Jiji (Desemba 25) na Fountain Gate (Desemba 29). Pia mechi mbili za marudiano Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya makundi dhidi ya TP Mazembe (Januari 3, 2025) na Al Hilal (Januari 10, 2025).

Lakini ikiwa atakaa nje kwa wiki sita, basi hataonekana uwanjani hadi Januari 28, 2025 katika mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya KMC, hapo kati ataikosa pia mechi ya mwisho Kundi A dhidi ya MC Alger itakayochezwa Januari 17, 2025. Zingine mbili za ligi dhidi ya KenGold (Januari 22, 2025) na JKT Tanzania (Januari 25, 2025).

Mbali na Diarra, nyota mwingine watakaokosekana kwa mujibu wa chanzo hicho ni, Maxi Nzengeli ambaye imeelezwa atakosekana uwanjani kwa takribani siku 10 hadi 14 kutokana na kuumia goti.

“Maxi aliumia goti siku moja kabla ya kucheza dhidi ya TP Mazembe, baada ya mchezo akawa anajisikia vibaya sana. Yeye matibabu yake yatachukua siku 10 hadi 14 kurejea uwanjani,” kilisema chanzo.

Maxi ambaye naye amekuwa sehemu ya wachezaji muhimu wa kikosi cha kwanza cha Yanga msimu huu, katika mchezo huo dhidi ya TP Mazembe alishindwa kuendelea kipindi cha pili baada ya kile cha kwanza kumaliza, nafasi yake ikachukuliwa na Clement Mzize.

Katika kipindi cha siku 10 hadi 14, Maxi naye anaweza kuzikosa mechi nne zilizobaki za ligi kumaliza mzunguko wa kwanza.

Clatous Chama anaingia kwenye listi ya wachezaji majeruhi wa Yanga ikielezwa atakosekana kwa takribani wiki mbili mpaka tatu kutokana na kuumia kiwiko.

Chama alipata tatizo hilo katika mchezo dhidi ya TP Mazembe ambapo aliingia dakika ya 76 kuchukua nafasi ya Duke Abuya.

Kipindi cha wiki mbili hadi tatu, kinamfanya Chama kuzikosa mechi nne zilizobaki za kumaliza mzunguko wa kwanza.

“Atahitaji takriban wiki mbili hadi tatu kwa ajili ya kupona jeraha hilo. Anatakiwa kuwa makini katika mazoezi yake ili kupunguza hatari ya kuangukia eneo lenye jeraha. Katika kipindi cha matibabu yake anatakiwa kufanya mazoezi ya gym,” kilisema chanzo.

Chama amekuwa na mchango mkubwa kwenye kikosi hicho akifanikiwa kucheza jumla ya mechi 18 kwa dakika 877. Mechi 11 ni za ligi akifunga bao moja na asisti tatu huku Ligi ya Mabingwa Afrika akicheza mechi saba, amefunga mabao matatu na asisti nne.

Wengine ni Aziz Andabwile ambaye alikuwa majeruhi wa muda mrefu, anatarajiwa kurejea uwanjani wiki ijayo huku Kennedy Musonda aliyeumia kidole gumba cha mguu wa kushoto, amepewa siku tatu za mapumziko kabla ya kuendelea na uchunguzi mwingine zaidi.

“Tatizo lake lilitokea siku nane zilizopita. Jeraha halijapona kutokana na msuguano wa viatu wakati wa kupiga mpira. Kwa sasa anapaswa ashiriki mazoezi yasiyohusisha mguu wa kushoto kugusa mpira kwa siku 3 zaidi ili kuruhusu jeraha kupona.

“Anaweza kuvaa viatu laini vya michezo na kushiriki mazoezi yasiyohusisha kupiga mpira, kama kukimbia au kukokota mpira kwa mguu mmoja,” kilisema chanzo.

Kukosekana kwa wachezaji hao kwa muda tofauti, inamlazimu Kocha Mkuu wa Yanga, Sead Ramovic kuwatumia nyota wengine kuziba nafasi zao.

Katika eneo la kipa, Khomeiny atachukua nafasi ya Diarra, wakati Chama, Maxi na Musonda nafasi zao wanaweza kucheza Aziz Ki, Mudathir Yahya na Clement Mzize.

Wakati huo, beki wa kushoto wa kikosi hicho, Chadrack Boka, anaendelea na mazoezi ya utimamu wa mwili chini ya kocha wa viungo huku ukiangaliwa uwezekano wa kuingizwa taratibu kwenye mechi za ushindani.

Related Posts