DKT. BITEKO APONGEZA TAMASHA IJUKA OMUKA

*Na Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati*

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amempongeza Mkuu wa Mkoa wa Kagera Hajjat Fatma Mwassa kwa maandalizi mazuri ya Kongamano la Uwekezaji mkoani humo litakaloibua fursa za uwekezaji na kukuza uchumi wa mkoa.

Dkt. Biteko ametoa pongezi hizo leo Desemba 19, 2024 mkoani Kagera wakati akizungumza katika Tamasha la Pili la Uwekezaji la mkoa huo ikiwa sehemu ya Wiki ya Ijuka Omuka (Kumbuka Nyumbani).

“ Nawapongeza waandaaji wa Kongamano hili na kama kuna watu wamekuja kuwekeza hapa napenda kuwapongeza wale mlioitikia wito tangu kwenye kongamano la kwanza na kuja kuwekeza hapa,” amesema Dkt. Biteko.

Amesisitiza “ Maombi yangu baada ya mkutano huu waje wengine kuwekeza na tutumie fursa hii ya uwepo wa mkoa huu kijiografia na kutumia fursa zilizopo,”

Aidha, amewaasa wananchi wa Mkoa wa Kagera kuunga mkono jitihada za Mkuu wa Mkoa na kumpa ushirikiano wa kutosha katika kutekeleza majukumu yake.

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Innocent Bashungwa amesema chimbuko la Tamasha hilo ni maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan aliyeta ifanyike tathmini ili kujua sababu za kudorora kwa uchumi na maendeleo ya Mkoa wa Kagera. Amesema mnamo mwaka 2022 wadau walikutana na kuainisha chanzo cha mkwamo kama mkoa.

“ Wananchi wa Kagera tuna bahati ya kupata ushirikiano mkubwa kutoka kwa Rais Samia na utashi wake wa kisiasa unasaidia mkoa wetu kutupa miradi mbalimbali ya maendeleo na hivyo inatupa fursa zaidi ya kukuza uchumi wetu,” amesema Mhe. Bashungwa.

Ameendelea kueleza kuwa sababu za kijiografia kwa mkoa wa Kagera pia zinauweka katika nafasi ya kimkakati kuleta maendeleo “Kijiografia tunamshukuru Mungu mkoa wetu upo eneo la kimkakati na tuna rasilimali watu wa kutosha hivyo tunawakumbusha wenzetu waliopo maeneo mbalimbali ndani na nje ya nchi kukumbuka nyumbani licha ya majukumu yao huko walipo,”

Mhe. Bashungwa ameishukuru Serikali kwa utekelezaji wa miradi wa miradi mikubwa kama vile ujenzi wa daraja la Kigongo – Busisi ambalo linatarajiwa kuzinduliwa mwezi Februari 2025, ujenzi wa barabara na pamoja na kuzungumizia hitaji la mkoa wa Kagera kuingia kwenye Gridi ya Taifa.

Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Mhe. Hajjat Fatma Mwassa amesema kuwa lengo la Tamasha hilo la Pili la Uwekezaji la Mkoa wa Kagera ni kutoa fursa kwa Serikali na mrejesho kwa wadau juu ya mafanikio na mipango ya Serikali kuhusu uchumi wa mkoa huo.

Akielezea wasilisho lake la miradi na fursa zilizopo mkoani humo, ametaja baadhi ya miradi inayoendelea kutekelezwa kuwa ni ujenzi wa barabara za kimkakati zenye urefu wa km 265.4 zinazogharimu shilingi bilioni 340.49 na ujenzi wa madaraja matano utakaogharimu shilingi bilioni 45.2.

Miradi mingine ni vituo vinne vya umeme vilivyojengwa kwa shilingi bilioni 163.

Katika sekta ya kilimo, Mhe. Mwassa amesema mkoa wake una mikataba miwili ya miradi ya umwagiliaji inayogharimu shilingi bilioni 2.9.

Halikadhalika, mkoa huo unatekeleza miradi mikubwa ya maji ya itakayogharimu kiasi cha shilingi bilioni 191 na kunufaisha zaidi ya wananchi 500,000.

Ameendelea kusema mkoa wake umepakana na nchi jirani nne na mikoa ya Kanda ya Ziwa Victoria na hivyo kuwahakikishia soko la uhakika wa bidhaa.

Aidha, amewapongeza wawekezaji mkoani humo kwa kujenga viwanda baada ya kuvutiwa na fursa zilizopo mkoani humo.

Pia, ametoa wito kwa wananchi kufuga samaki na dagaa katika vizimba na kuongeza thamani ili waweze kuuza nje ya nchi badala ya sasa ambapo wanunuzi kutoka nje ya nchi wananunua dagaa moja kwa moja kwa wafugaji wadogo.

Mhe. Mwassa amehamasisha uwekezaji wa hoteli mkoani humo “Mikutano hii ya Jumuiya ya Afrika Mashariki haifanyiki hapa Kagera kwa sababu hatuna uwezo wa kuhudumia idadi kubwa ya watu, mfano Polisi kutoka nchi hizi za Jumuiya ya Afrika Mashariki walipenda kuja hapa kufanyia mkutano wao haikuwezekana kwa sababu hatuna ukumbi wa kuhifadhi watu 3,000 kwa pamoja hivyo walienda mahali pengine” amebainisha Mhe. Mwassa.

Vilevile, Mhe. Mwassa ameonesha kiu yake ya kuona uwanja wa ndege wa Omukajunguti ukijengwa na kukamilika ili kutoa huduma kwa wananchi na kuchochea ukuaji wa uchumi wa mkoa huo.

Mhandisi kutoka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Emannuel Mayanga amesema kuwa kupitia Miradi ya Kupendezesha Miji (TACTIC) Manispaa ya Bukoba itanufaika na ujenzi wa barabara zenye urefu km 10.75, uwekaji wa zaidi ya taa za barabarani zaidi 800 zitakazosaidia kuangaza Bukoba wakati wa usiku, uboreshaji wa kingo za Mto Kanoni pamoja na uboreshaji wa soko.

Kupitia tamasha hilo wadau na wawekezaji wamejadiliana kuhusu fursa mbalimbali za uwekezaji zilizopo mkoani humo.

Related Posts