Guede aanika kilichomponza | Mwanaspoti

STRAIKA wa zamani wa Yanga aliyekuwa akikipiga Singida Black Stars kabla ya kutemwa mapema wiki hii, Joseph Guede amefunguka sababu zilizomwondoa ndani ya kikosi hicho, huku akishindwa kufichua kama kuna dili lolote jipya nchini alilolipata.

Guede alijiunga na Singida mwanzoni mwa msimu huu kwa mkataba wa mwaka mmoja akitokea Yanga aliyoitumikia kwa miezi sita kabla ya makubaliano ya pande mbili yaliyositisha mkataba huo.

Akizungumza na Mwanaspoti, alifichua majeraha ndiyo yaliyomtibulia.

Nyota huyo raia wa Ivory Coast, Alisema ni kweli wamefikia makubaliano ya kuvunja mkataba na timu hiyo,  lakini anaamini shida kubwa ni hali ya majeraha aliyoyapata mwanzoni mwa msimu na kumfanya kushindwa kujitolea kwa bidii ndani ya kikosi hicho.

“Kukaa nje kwa muda nikijiuguza jeraha nililolipata mwanzo mwa msimu huu na kukosa nafasi ya kucheza mara kwa mara, ndiyo sababu iliyoniondoa kwenye kikosi cha timu hiyo,” alisema Guede aliyemaliza na mabao sita katika nusu msimu alioitumikia Yanga iliyomsajili kuchukua nafasi ya Hafiz Konkoni.

“Nimeitumikia Singida kwa miezi sita, hivyo, bado nilikuwa na mkataba wa miezi mingine sita ili kuumaliza lakini mara baada ya kuitwa mezani tulikubaliana kuvunja mkataba,” alifichua mshambuliaji huyo aliyerivusha Yanga kwenda robo fainali ya Ligi ya Mabingwa msimu uliopita alipofunga bao la mwisho la nne wakati wakiiua CR Belouizdad kwa mabao 4-0 jijini Dar es Salaam.

Guede alisema msimu mmoja aliocheza Tanzania akiitumikia Yanga na Singida umekuwa na milima na mabonde, lakini amefurahia maisha ya nje ya mpira kutokana na namna watanzania wanavyopenda mpira.

“Tanzania wanapenda sana mpira na wana upendo lakini mambo ya ndani ya uwanja yana changamoto nyingi ambazo zinahitaji ukomavu ili uweze kustahimili na kuweza kuendana na kasi ya ushindani iliyopo,” alisema Guede ambaye hajafunga bao lolote la Ligi akiwa na kikosi hicho zaidi ya kuasisti tu mara moja.

Related Posts