Kisa Mpanzu… Simba wakuna vichwa

JANA Ellie Mpanzu hakuanza na wala hakuwa katika benchi la kikosi cha Simba kilichovaana na Ken Gold wakati wa pambano la Ligi Kuu Bara, tofauti na majigambo ya mabosi wa Msimbazi mwamba huyo angeanza kuonekana mara baada ya dirisha dogo la usajili litakapofunguliwa, huku ikielezwa kilichomzuia.

Simba ilimsajili Mpanzu tangu Septemba mwaka huu muda mchache baada ya dirisha kubwa la usajili kufungwa Agosti 31 na ilinezwa angeanza kutumika mara dirisha dogo lililofunguliwa tangu Jumapili, lakini inaelezwa ishu ya jina gani likatwe ili kumpisha Mkongoman huyo ndiyo inayowapasua vichwa mabosi.

Awali ilielezwa kipa Ayoub Lakred angeonyeshwa mlango wa kutokea ili kulipisha jina la Mpanzu na taarifa zingine zikisema huenda akawa ni Joshua Mutale ambaye amekuwa akisumbuliwa na majeraha ya mara kwa mara, lakini mambo yamekuwa tofauti baada ya kuelezwa kumetokea mgawanyiko kwa mabosi wa klabu hiyo.

“Ishu kubwa kwa sasa ni juu ya nani atemwe ili kumpisha Mpanzu, kwani tayari Simba ilikuwa na majina 12 kama kanuni inayoelekeza na wachezaji wengine wana mikataba ambayo kuivunja ni mtihani na gharama kubwa, ila kila kitu kinaenda kuwekwa sawa na jamaa ataanza kucheza,” kilisema chanzo kutoka ndani ya Simba, huku ikielezwa hadi jana mabosi walikuwa wakikuna vichwa kufanya maamuzi ili Mpanzu aliamshe.

Nyota huyo wa zamani wa AS Vita, alichelewa kutua Msimbazi baada ya kutokea kwa dili la kwenda kutesti zali KRC Genk ya Ubelgiji, ambayo hata hivyo mambo yalikwama na kurudia DR Congo kabla ya kuamua kuja nchini kusaini mkataba na Simba iliyomtambulisha Oktoba mwaka huu.

Hata hivyo, juzi Ofisa Habari wa Simba, Ahmed Ally akihojiwa na mtandao wa klabu hiyo alisema mchakato ulikuwa unaendelea na kuhusu nani atakayempisha, umma utafahamishwa kwani viongozi wa klabu walikuwa akipambana na kuwataka Wanasimba kuwa na subira.

“Hadi kesho (jana) tutakuwa na majibu mazuri juu ya mchakato wa usajili wa Mpanzu. Juu ya nani atakayeachwa pia itafahamika na wapenzi na mashabiki wawe na subira kwani mchakato unaendelea vizuri ili kukamilisha usajili wa mchezaji huyo,” alinukuliwa Ahmed, hata hivyo katika kikosi kilichocheza jana hata benchi hakuwepo kuonyesha mambo yalikuwa hayajakaa sawa.

Related Posts