Kwa nini kituo cha biashara Ubungo ni muhimu Afrika Mashariki na Kati

Dar es Salaam. Wakati uwekezaji wa nchi ya China kwa Tanzania ukiongoza nchini, Kituo cha Biashara na Usafirishaji cha Ubungo (EACLC) kimetajwa kuwa kiungo cha uwekezaji huo na ukuzaji biashara kwa Afrika Mashariki.

Mwananchi limefanya mahojiano maalumu na meneja wa kituo hicho, Cathy Wang, hivi karibuni, ambapo amezungumzia mambo mbalimbali, ikiwemo matarajio yao baada ya kituo hicho kuanza kazi mapema mwaka 2025 na kitakavyokuwa lango kuu la bidhaa zinazotoka China.

Ifuatayo ni sehemu ya mahojiano hayo kati ya Wang na mwandishi wa Mwananchi, Elias Msuya, yaliyofanyika Ubungo, Dar es Salaam:

Swali: Kituo hiki kina umuhimu gani ikiwa tayari kuna masoko mengine yanayoagiza bidhaa kutoka China?

Jibu: Kituo hiki kitakuwa lango kuu la bidhaa kutoka China kuingia nchini na kusafirisha bidhaa kwa nchi nyingine za Afrika Mashariki. Wafanyabiashara hawatalazimika kuagiza bidhaa nje ya nchi na kusubiri miezi mitatu minne, badala yake watachukua hapa Tanzania.

Swali: Tangu mradi huu umeanza kujengwa, mmechangia vipi uchumi na mtachangiaje kitakapokamilika?

Jibu: Huu mradi una manufaa mengi kwa uchumi wa Tanzania, zikiwamo ajira zitakazozalishwa. Mpaka sasa ambapo mradi bado haujakamilika, kuna ajira za watu 5,000 zimezalishwa na tutakapoanza mradi, angalau ajira 15,000 zitazalishwa na ajira zisizo rasmi zitakuwa 50,000.Naamini mradi huu utakapofunguliwa utakuza biashara na uchumi kwa Tanzania na kwa nchi zinazozunguka.

Pia mradi utawezesha kukua kwa biashara ya mtandaoni na itakapoanza itazalisha ajira nyingi, hasa kwa vijana. Kwa hiyo mradi utakuza biashara, ikiwemo kuongeza uingizaji wa bidhaa na uuzaji wa bidhaa nje ya nchi.

Hebu fikiria miaka ijayo, nchi za Afrika Mashariki hazitalazimika kwenda China kufungasha mizigo, watakuja hapa Dar es Salaam kama wanavyokwenda kuchukua huko, hicho ndicho tunachokusudia.

Kwa hiyo wafanyabiashara wa ndani waje hapa kuchukua bidhaa na tutawaunganisha na wazalishaji wa bidhaa.

Swali: Kumekuwa na hofu ya baadhi ya wafanyabiashara wa eneo la Kariakoo, kwamba mradi huu utazorotesha biashara zao. Unasemaje?
Jibu: Sidhani kwamba mradi huu utazorotesha biashara katika eneo la Kariakoo, kwa sababu Kariakoo ni kubwa sana na ni eneo lililoanzishwa tangu miaka ya 1940, hivyo watu hawataacha kwenda.

Halafu kama tunataka nchi iendelee, hatuwezi kulazimisha kila mtu aende Kariakoo na ujifungie hapo tukisema tusipanue biashara kama tulivyojenga hapa Ubungo.

Swali: Hofu hiyo pia inaelezwa kuwepo kwenye bei zenu zitakazovutia wateja na pengine wakaacha kwenda kwenye masoko mengine yenye bei kubwa. Hilo nalo unalizungumziaje?

Jibu: Kuhusu bei, watakaokuwa wakipanga bei ni wafanyabiashara watakaokuwa wanafanya biashara kwenye kituo hiki.

Sisi tunatengeneza jukwaa kwa Watanzania kufanya biashara na ndiyo maana kuna baadhi ya wafanyabiashara waliokwisha pangisha maduka hapa tumewapeleka China kwenda kujifunza biashara na kuwaunganisha na wazalishaji wa bidhaa mbalimbali.

Hivyo sisi hatushindani na wafanyabishara wa ndani, isipokuwa tunawatengenezea jukwaa kwa ajili ya kurahisisha na kukuza biashara zao.

Swali: Ukiwa mmoja wa wawekezaji kutoka nchini China, unadhani kwa nini Wachina wengi wanakimbilia kuwekeza Afrika, hasa Tanzania?
Jibu: Kinachotuvutia sisi kuja Tanzania ni amani na utulivu wa kisiasa, hivyo wawekezaji wengi wanakuja kwa kuwa wameridhishwa na mazingira ya uwekezaji.

Mimi ni mtu ninayeweza kutoa ushuhuda wa mazingira mazuri ya biashara nchini Tanzania kwa sababu nimekuwepo zaidi ya miaka 10 sasa. Nimeona wakati wa Rais Jakaya Kikwete, nimeona wakati wa Rais John Magufuli na hata sasa.

Mazingira ya kisiasa yako tulivu, mamlaka za kodi na Serikali wako tayari kuzungumza na wawekezaji wakati wote, kwa hiyo kama una jambo hatujaelewana, wako tayari kutusikiliza.

Kumekuwa na makundi ya wawekezaji kutoka nchini China yanayokuja hapa na tunawaeleza fursa za uwekezaji nchini Tanzania na kwa nchi nyingine za Afrika Mashariki na hata kwa nchi za Jumuiya ya Maendeleo ya nchi za Kusini mwa Afrika (Sadc), kwa hiyo kuna fursa kote huko.

Tumekuwa tukipokea makundi ya wawekezaji wakija Tanzania na wanafurahia mazingira ya biashara wakilinganisha na nchi nyingine.

Kuna nchi nyingine hazina mazingira mazuri, hazina sera nzuri za uwekezaji, hakuna usalama na wakati mwingine mfumo wa fedha hauridhishi.

Swali: Mna mpango wa kufungua vituo vingine zaidi ya hapa Ubungo?
Jibu: Ndiyo, tunaweza kuwa na vituo.

Related Posts