Mahakama yazuia mashahidi kutajwa kesi ya mauaji ya polisi

Dar es Salaam.  Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam imetoa amri ya kutotajwa majina ya mashahidi wala maelezo yao yanayoweza kuwatambulisha katika kesi ya mauaji ya askari polisi wawili.

Askari polisi E.177 Koplo Michael na D.2865 Sajini Francis waliuawa kwa kupigwa risasi Aprili 2015 na kuporwa silaha katika tukio lililotokea Mkoa wa Kipolisi Temeke, Dar es Salaam linalohusishwa na matendo ya kigaidi.

Kutokana na sababu za kiusalama, Mkurugenzi wa Mashitaka nchini (DPP) aliwasilisha ombi la kusikilizwa upande mmoja akiiomba Mahakama itoe amri kuzuia kutaja utambulisho wa mashahidi na mahali walipo.

Maombi hayo namba 26910 dhidi ya Hassan Kube (mshitakiwa wa kwanza) na Mohamed Hassan (mshitakiwa wa pili) yalisikilizwa Desemba 13, 2024 na Jaji Mfawidhi Awamu Mbagwa.

DPP aliomba Mahakama itoe zuio hilo wakati kesi ya mauaji namba 2 ya mwaka 2023 itakopopangwa kwa ajili ya usikilizwaji wa awali katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Pia, aliomba kutowekwa wazi maelezo na nyaraka zinazoweza kuwatambulisha mashahidi wakati wa usikilizwaji wa awali na usikilizwaji kamili wa kesi hiyo ya jinai.

Katika ombi la tatu na la nne, DPP aliiomba Mahakama itoe amri ya kusikilizwa faragha mwenendo wa kesi hiyo na kutoa amri inayotoa ulinzi na ustawi kwa mashahidi wote wa kesi hiyo ili kutoa hakikisho la usalama wao.

Ombi hilo liliambatanishwa viapo viwili vya wakili mwandamizi wa Serikali kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashitaka (NPS), Neema Moshi na kiapo cha Mkuu wa Upelelezi Temeke, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP) Jumanne Amas.

Katika hoja za DPP za maandishi zilizowasilishwa na Wakili wa Serikali, Monica Ndakidemi alieleza wajibu maombi wanakabiliwa na mashitaka ya mauaji ya polisi hao katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Wakili Ndakidemi alidai uchunguzi wa polisi unaonyesha wajibu maombi walikuwa katika genge la uhalifu lenye lengo mahususi la kuvuruga na kuharibu mifumo ya kisiasa, Katiba, uchumi na kuanzisha dola la Kiislamu.

Katika kutekeleza malengo yao, alidai walivamia vituo mbalimbali vya polisi kwa lengo la kupora silaha na baadaye kuzitumia katika kufanikisha malengo hayo na wanazichukulia harakati hizo kama ugaidi.

“Makosa hayo ni makubwa kwa uasili wake na yana madhara makubwa kwa jamii,” alidai wakili Ndakidemi.

Wakili huyo alidai wajibu maombi na washirika wao ambao hawajakamatwa, wanawatisha watu waliopangwa kuwa mashahidi.

Katika uamuzi alioutoa Desemba 18, 2024 Jaji Mbagwa alisema kupitia hati za viapo zilizowasilishwa, inaonyesha wajibu maombi kwa kushirikiana na washirika wao wanahangaika kupata utambulisho wa mashahidi wa kesi hiyo.

Jaji Mbagwa amesema lengo ni kuwazuia mashahidi kutoa ushahidi, hivyo ni jukumu la Mahakama kupima kama ombi la DPP lina mashiko au la.

“Ni jambo la wazi kuwa mashahidi wanachukuliwa kama watu muhimu kupata ukweli ili kutenda haki, ili kulinda mashahidi kuna jitihada mbalimbali za kimataifa na kitaifa zinazofanyika kuweka mifumo ya usalama wao,” amesema Jaji Mbagwa.

Jaji alirejea njia mbalimbali za kimataifa lakini kwa nchini, amesema zipo sheria zinazolinda mashahidi na watoa taarifa kupitia sheria ya kuwalinda mashahidi na Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA).

Amesema ipo sheria ya kuwalinda watoa taarifa  inayojulikana Whistleblower and Witness protection Regulation na tangazo la Serikali (GN) 59 ya 2023 na zote zinatoa fursa ya kuzuia kutaja mashahidi na kesi kusikilizwa faragha.

Jaji amesema ni wazi kutoa majina ya mashahidi na maudhui ya ushahidi wao ni moja ya kanuni ya usikilizwaji wa haki, lakini pia upo umuhimu kuhakikisha mashahidi na familia zao wanalindwa ili kuwashawishi kutoa ushahidi.

Ni kutokana na ukweli huo, ametoa amri ya kutotolewa utambulisho na mahali walipo mashahidi wakati wa hatua ya usikilizwaji wa awali na pia kuwekwa wazi kwa maelezo na nyaraka zitakazowatambulisha mashahidi.

Pia, usikilizwaji utafanyika faragha hivyo umma pamoja na wanahabari hawataruhusiwa.

Related Posts