Mwanza. Katika kipindi cha Januari hadi Desemba 2024, Jeshi la Polisi mkoani Mwanza limetoa taarifa ya matukio zaidi ya 12 ya mauaji yanayotokana na wivu wa mapenzi, huku wadau wakishauri njia kadhaa ya kukabiliana na mauaji hayo.
Miongoni mwa matukio hayo ni yaliyotokea Desemba 14 ba 15, 2024 ambapo jeshi hilo linawashikilia wakazi wawili wa mkoani humo akiwemo mvuvi wa Wilaya ya Ilemela kwa tuhuma za kuwaua wake zao kisa wivu wa mapenzi.
Akizungumza Desemba 19, 2024 Kamanda wa Polisi mkoani Mwanza, Wilbrod Mutafungwa amesema tukio la kwanza lilifanywa na Cornelio Kuboja (39) aliyemuua mkewe, Leticia Samwel (46) wote wakazi wa Mtaa wa Nyagungu Kata ya Ilemela.
“Mnamo Desemba 14, 2024 saa 12 asubuhi Mtaa wa Nyagungulu, Kata ya Ilemela, kulipatikana mwili wa marehemu Leticia Samwel (46) mkulima na mkazi wa Nyagungulu aliyeuawa na mume wake aitwae Cornelio Kuboja (39) mvuvi na mkazi wa Nyagungulu, chanzo cha mauaji ni wivu wa mapenzi,” amesema Mutafungwa
Kamanda huyo amesema tukio jingine la mauaji yaliyosababishwa na wivu wa mapenzi lilitokea Desemba 15, 2024 saa nne usiku katika kijiji cha Jojiro kata ya Ng’hundi wilayani Kwimba ambapo Wella Mayunga (48) aliuawa kwa kushambuliwa na mume wake, Makoye Machiya (49). Aidha, Mutafungwa amesema watuhumiwa wamekamatwa huku taratibu za kisheria zikiendelea.
Tukio lingine lilitokea Oktoba 24, 2024 ambapo mkazi wa Bugarika Bendera tatu wilayani Nyamagana, Amos Mwita (17) alikamatwa kwa tuhuma za kumuua jirani yake, Daniela Kisire (18) kisa wivu wa mapenzi.
Mutafungwa amesema tukio hilo lilitokea saa 1:00 jioni ambapo Mwita alimchoma Daniel na kitu chenye ncha kali shingoni na kusababisha kifo chake wakimgombea binti wa miaka 14.
Inadaiwa kwamba marehemu Daniel alimtaka kimapenzi binti huyo mkazi wa Bugarika nakumkataaa na baadaye alianza mahusiano ya kimapenzi na Mwita ambaye ni rafiki wa Daniel.
Aprili mwaka huu pia mkazi wa Mwamanyili Halmashauri ya Buchosa mkoani Mwanza, Jackson Kalamji (49) alidaiwa kumuua mkewe, Mariam Bulacha (42) kwa kumchoma visu sehemu mbalimbali mwilini, baada ya kumtilia shaka kuwa na uhusiano wa kimapenzi na mwanaume mwingine.
Tukio lingine lilitokea Julai 18, 2024 ambapo jeshi hilo lilimkamata mkazi wa Nyakasela Kata ya Nyakariro Sengerema mkoani Mwanza, Lupande Ng’wani (43) aliyedaiwa kumuua Mwajuma Yugele kwa kumpiga na kitu kizito kichwani chanzo kikiwa ni wivu wa mapenzi.
Julai 28, 2024 mtoto wa miaka mitatu, Lukonya Kisumo aliuuawa kwa kunyongwa shingoni na baba yake mzazi, Kisumo Emmanuel (38) baada ya kumtuhumu mkewe kuzaa na mwanaume mwingine, kisha kuchukua mwili wa mtoto huyo na kuutupa katika kisima cha maji kilichopo kwenye shamba la mpunga naye kujinyonga juu ya mti.
Katika tukio lingine, Kamanda Mutafungwa alitoa taarifa kuwa Julai 30, 2024 mkazi wa Kisamba Kata ya Lubugu wilayani Magu mkoani humo, Fednand Mabula (41) alimuua mke wake, Christina Kisinza (40) kwa kumkata na kitu chenye ncha kali shingoni kisha naye kujinyonga baada ya kutekeleza mauaji hayo, chanzo cha mauaji hayo kikitajwa kuwa ni wivu wa mapenzi.
Wakati huohuo, mkazi wa Kijiji cha Isegeng’e Kata ya Mwakiliambiti Wilaya ya Kwimba mkoani humo, Benjamini Masanye (29) alituhumiwa kumuua mpenzi wake, Veronica Ndabile (23) kwa kumkata na kitu chenye ncha kali maeneo mbalimbali ya mwili wake. Tukio alilodaiwa kulifanya Julai 31, 2024, saa 2:30 usiku.
Njia yakutokomeza mauaji hayo Mhadhiri mwandamizi na Mkuu wa Kitivo cha Falsafa Chuo cha Saut, Padri Innocent Sanga amesema ili kutokomeza mauaji hayo ni muhimu wenza waanze kuandaliwa kuwa mke na mume kabla ya kufunga ndoa na kuishi pamoja, huku akishauri kuwepo program maalumu kwenye vyombo vya habari za kuelimisha na kuonesha wivu huo unavyoangamiza maisha.
“Huko nyuma wazazi wetu mambo kama haya yalikuwa hayapo watu kuuana kwaajili ya mapenzi lakini kwa sababu gani? kulikuwa na maandalizi mazuri, mume wako ni nani mke wako ni nani? kulikuwa na jando, unyago na kadharika… Watu wanajifunza kuheshimiana,”amesema Padri Sanga na kuongeza.
“Nina fikiri kuwa kitu hiki hata kikienda katika mafunzo yetu kwenye mitaala pengine tutakuwa waoga kuwafundisha watoto wa sekondari mahusiano ya kimapenzi lakini imefika wakati tunaona ni janga watu wanauana ni kwanini tusitafute namna hata kwenye taaluma yetu viwepo vipengele vya namna hiyo? vyakuongelea mahusiano na kuua huu wivu unaokomaa,” amesema.
Amesema Serikali za mitaa, vijiji na vitongoji zianze kuchukua hatua mapema hasa mabalozi kwa kuwa dalili za matukio hayo huanza mapema kwa wenza kugombana, kutoleana lugha mbaya na wakati mwingine uvumi wa kuuwana husambaa eneo husika.
“Maneno huwa yanaibuka kwamba huyu anamuonea wivu fulani…yanaanza palepale ila hatua hazichukuliwi. Serikali ingekazia kuanzia uongozi wa chini kwamba unapoona kitu hiki, neno, malumbano baina ya wapenzi wawili ni lazima uingie mapema na pia sheria fulani itungwe juu ya mahusiano kwa sababu unajua wapezi wanapouana ni janga la Taifa,” amesisitiza.
“Serikali inaweza kuepusha janga la mauaji kwa kutunga sheria viongozi wachini kule wafanye nini wanapoona ugomvi wa namna hiyo,”ameongeza
Mkazi wa Kasulu, Francis Nyakamwe (80) amesema mauaji enzi za ujana wao yalikuwepo lakini si kwa kiasi kikubwa kama yanavyotokea miaka ya hivi karibuni huku akisisitiza wazazi waanze kupandikiza imani za kidini kwa watoto wao kuanzia utotoni.
“Shetani anataka kwenda na wengi motoni, kilichobaki ni kumuomba Mungu tu lakini pia imani za kidini zianze kupandikizwa kwa watoto tangu wakiwa hawajui kitu ili wakue wakijua kuua ni laana na malipo yake ni motoni,” amesema Nyakamwe.
Mkazi wa jijini Mwanza, Rukia Hamdani (65) amesema enzi za ujana wazee wao walibuni mbinu ya kuwaaminisha kuwa kuua ni laana si ya muuaji pekee bali, familia yake na ukoo mzima utapata laana hiyo hadi atakapotakaswa.
“Hapakuwepo matukio ya aina hii kwakuwa jamii iliamini mauaji ya aina yoyote na kwa sababu yoyote ni laani kwa familia na ukoo mzima. Na pindi mauaji yalipofanyika, ilikuwa ni lazima matambiko ya kumtakasa muuaji na familia yake yafanyike kuondoa laani katika jamii,” amesema Rukia.
Mkakati wa Serikali kumaliza mauji ya wivu wa mapenzi
Julai 27, 2024 Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Mwanaidi Ali Khamis wakati akijibu swali la msingi la Mbunge wa Wingwi (CCM) Omaari Issa Kombo, amesema miongoni mwa mikakati ya Serikali kudhibiti mauaji yatokanayo na wivu wa mapenzi ni kutoa huduma ya afya ya akili.
Mkakati mwingine ni kutoa msaada wa kisaikolojia kwa jamii na kutoa hifadhi ya dharula kwa manusura wa ukatili wa vitendo hivyo.
Mikakati hiyo ilitolewa baada ya Kombo kuhoji Serikali ina mikakati gani ya kukabiliana na vitendo vya ukatili ikiwemo mauaji yanayotokea kwenye jamii kwa sababu za wivu wa kimapenzi. “Mikakati hiyo imebainishwa katika Mpango Kazi wa Taifa wa Pili wa Kutokomeza Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto pamoja na Sera ya Jinsia na Maendeleo ya Wanawake ya Mwaka 2023 kwa lengo la kukabiliana na vitendo vya ukatili ikiwemo mauaji yanayotokea kwenye jamii kwa sababu za wivu wa kimapenzi,” amesema Mwanaidi.
Takwimu za mauaji mkoani Mwanza Kwa mujibu wa takwimu za ripoti ya hali ya uhalifu na matukio ya usalama barabarani kwa kipindi cha Januari hadi Desemba 2023, mauaji 101 yaliripotiwa mkoani Mwanza kati ya mauaji 2,259 yaliyoripotiwa katika mikoa ya kipolisi Tanzania bara.
Katika ripoti hiyo, vyanzo vya mauaji hayo vilivyotajwa ni wivu wa mapenzi au ugoni, visasi, tamaa ya kupata mali kinyume cha sheria, ulevi, migogoro ya ardhi na mali pamoja na imani za kishirikina.
Huku, baadhi ya mikakati iliyotajwa katika ripoti hiyo ili kuepusha mauaji hayo ni jeshi la polisi kuhamasisha wadau mbalimbali kuendelea na kuimarisha utoaji wa elimu rika kwa vijana ili waweze kuzikabili changamoto za mahusiano ya kijinsia.
Na kuhamasisha jamii kuwatumia watalaamu wa Ushauri nasaha pindi wanapopatwa na changamoto za afya ya akili na migogoro mbalimbali katika jamii, kutoa elimu kwa umma kwa njia mbalimbali ili jamii ibadilike na kuacha kujichukulia sheria mkononi pamoja na kushirikisha taasisi za kidini kuhamasisha jamii ili kuachana na imani potofu za kishirikina.