Arusha. Mfumo maalumu wa kielektroniki mahususi kwa ajili ya kushughulikia changamoto na malalamiko ya wateja kwa taasisi za fedha, unatajwa kulinda wateja na kupunguza malalamiko hasa ya watoa mikopo wasiozingatia kanuni na taratibu.
Aidha mfumo huo unatajwa kusaidia watoa huduma za kifedha kutoa huduma bora kwa kuzingatia kanuni na taratibu zilizowekwa.
Kauli hiyo imetolewa leo Alhamisi Desemba 19, 2024 na mtoa huduma za kifedha kutoka taasisi ya Manemane Micro Credit (Moshi), Anselimu Peter, kwenye semina kwa watoa huduma za kifedha iliyofanyika Benki Kuu ya Tanzania (BoT),tawi la Arusha.
Amesema mfumo huo utasaidia kulinda walaji ambaye anahudumiwa na watoa huduma kwani kumekuwa na malalamiko mengi huku mlaji akionewa.
“Mfumo huu ni mzuri kwa kuwalinda walaji kwani kuna mambo mengi huenda mlaji anaonewa na watoa huduma hasa katika ukopeshaji hivyo kupitia mfumo huu mlaji ana uwezo wa kuwasilisha changamoto zake BoT na zikatatuliwa kwa wakati,” amesema.
“Sisi watoa huduma ndogo za fedha utatusaidia pia kwani tutaweza kupokea malalamiko kwa mteja na kuyashughulikia kwa wakati.Watoa huduma wasio la leseni wataogopa kutoa huduma bila kuwa na leseni kwani wataogopa kulalamikiwa na wateja kupitia mfumo,” ameongeza.
Meneja wa Idara ya Uchumi kutoka BOT tawi la Arusha, Aristedes Mrema amesema mfumo huo ambao umeshafanyiwa majaribio utaanza kutumika Januari, 2025.
Amesema moja ya majukimu ya BOT ni kuwalinda watumiaji wa huduma za kifedha pamoja na majukumu mengine ni kuimarisha huduma jumuishi, usimamizi wa fedha na kuwa mfumo huo umelenga kuhakikisha uaminifu katika sekta ya fedha kupitia mwongozo madhubuti wa kushughulikia malalamiko, mwenendo wa soko na kuongeza uelewa kwa watumiaji.
“Kwa kutumia teknolojia,benki imetengeneza mfumo huo wa utatuzi wa malalamiko ha wateja wa huduma za kifedha ili kuboresha mchakato wa kushughulikia malalamiko kwa njia bora ya haki na inayoweza kufikiwa kirahisi,” amesema.
Mrema amesema malalamiko mengi yamekuwa zaidi kuhusu masuala ya mikopo hasa wakopaji wanapotaka kujua madeni yao, wanacheleweshewa hawatumiwi kwa wakati na fedha za wateja kuchukuliwa fedha kwenye akaunti zao.
Naye Imelda Mathew kutoka taasisi ya CAS Microfinance Ltd ya Monduli, amesema mfumo huo utasaidia malalamiko kutatuliwa kwa wakati huku akitaja changamoto kubwa wanayokutana nayo ni pamoja na baadhi ya wateja kuwa na uelewa mdogo.
“Mfumo utasaidia kupunguza gharama kwani watu walikuwa wakitumia gharama kufuatilia malalamiko yao. Changamoto ni pamoja na uelewa wa mteja mfano anapewa mkopo ila wakati wa marejesho anaanza kusumbua.
“Wakati huo unapoanza kufuata utaratibu uliopo kwenye fomu ambapo yeye mwenyewe aliisoma labda kwa haraka hakuelewa kwa sababu ya kiu ya fedha aliyokuwa nayo, ukirudi kwenye mkataba anaona kama hujamtendea haki,” amesema.