Arusha. Serikali ya Mkoa wa Arusha kwa kushirikiana na wataalamu wa maendeleo ya jamii imeweka malengo ya kuwafuta ombaomba wote ndani ya Jiji la Arusha ndani ya miezi sita.
Hatua hii inalenga kupunguza kero kwa watalii, wageni na wafanyabiashara jijini humo.
Azimio hilo lilifikiwa katika Kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC) kilichofanyika leo Alhamisi Desemba 19, 2024.
Katika kikao hicho, mjumbe Viola Likindikoki amesisitiza ongezeko la ombaomba limekuwa changamoto kubwa na inashusha hadhi ya Jiji la Arusha.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Arusha, Mussa Missaile amesema wengi ni walemavu wanaoishi mitaani katika mazingira hatarishi. “Hali hii siyo tu inahatarisha maisha yao, bali pia inadhoofisha taswira ya jiji,” amesema.
Hata hivyo amesema serikali imeanza kukusanya taarifa za ombaomba hao kwa kushirikiana na wenyeviti wa mitaa ili kuwasaidia kwa njia mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kuwarejesha makwao au kuwawezesha kuanzisha shughuli za kiuchumi.
“Kwa sasa, halmashauri ya jiji ina zaidi ya Sh6 bilioni za mikopo ya asilimia 10 kwa vikundi vya wanawake, vijana, na walemavu. Tunawashauri walemavu kuacha kuomba mitaani na badala yake waombe mikopo hii kwa ajili ya biashara halali,” amesema Missaile.
Akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda, Mwenyekiti wa kikao hicho, Dadi Kolimba amesisitiza umuhimu wa kuwasaidia ombaomba halisi na kuwachukulia hatua wale wanaotumia hali yao kama fursa ya kiuchumi kwa faida ya wengine.
Mwenyekiti wa Kamati ya Maendeleo ya Jamii ya Jiji la Arusha, Isaya Doita amesema kuna haja ya kufanya utafiti wa kina ili kubaini idadi kamili ya ombaomba na mahitaji yao halisi.
Amesema hatua za kushughulikia changamoto hii zitakamilika ifikapo Juni 2025 na hatua hiyo amesema inalenga kuboresha hadhi ya Jiji la Arusha na kuboresha maisha ya walemavu na watu wengine wenye uhitaji maalumu.