UKUTA wa Yanga kwa sasa kuna mabeki wawili wa kati wa maana Ibrahim Abdullah ‘Bacca’ na nahodha msaidizi, Dickson Job ambao wanaibeba timu hiyo katika michuano ya ndani na ile ya kimataifa, lakini kocha mmoja aliyeweka rekodi hivi karibuni, amevunja mkimya na kuwapa mchongo wa maana kwa mustakabali wa soka na maisha yao kwa ujumla.
Aliyeyasema hayo ni Kocha, Hemed Suleiman ‘Morocco’ anayewafundisha wachezaji hao ndani ya Taifa Stars, akisema mabeki hao wawili ni wakati muafaka sasa kuanza kufikiria kucheza soka la ushindani zaidi nje ya Tanzania.
Kocha huyo mzawa, amewaka wachezaji hao wanaokipiga pia timu ya taifa, kupambana sasa ili nao wakacheze soka la kulipwa kabla umri haujawatupa mkono.
Morocco aliyeweka rekodi ya kuiongoza Stars kufuzu fainali za Mataifa Afrika 2025 akiwa kocha mzawa, alisema mabeki hao wawili wameshafanya kila kitu kwenye soka la ndani na kwa viwango vyao sasa ni wakati muafaka kwenda kuendeleza makali waliyonayo nje ya nchi kwa kucheza soka la kulipwa huko.
Nyota huyo wa zamani wa kimataifa wa Zanzibar aliyewahi kutamba na Coastal Union, alisema endapo wataendelea kubaki zaidi nchini nafasi hiyo itaondoka kwa kuwa umri utakwenda lakini pia kama viwango vyao vitapungua itakuwa ngumu kupata nafasi hiyo.
“Unamuona Bacca na Job wale wote wanatakiwa kwenda kucheza soka la ushindani zaidi nje ya nchi na wanatakiwa kuweka mkazo sasa kwenda huko badala ya kuendelea kubaki hapa nchini,” alisema Morocco na kuongeza; “Kwa sasa wameshafanya makubwa hapa nchini, wana uzoefu wa kutosha, kama watafanya hivyo sasa itaisaidia hata timu ya taifa kuongeza watu bora zaidi.”
Kauli hiyo ya Morocco inaungana na kocha wa zamani wa Yanga, Mbelgiji Torm Saintfiet ambaye wakati anaifundisha Gambia aliwahi kumuona Bacca katika fainali za Mataifa zilizofanyika Ivory Coast akisema beki huyo ana sifa nyingi za kucheza Ulaya.
Mbali na mabeki hao wawili, Morocco pia amemtaja kiungo Feisal Salum ‘Fei Toto’ akisema naye anatakiwa kuanza hesabu za kuondoka nchini kwenda kuendeleza kiwango chake.
“Yupo pia Feisal, ukiangalia kuanzia alipokuwa Yanga na hata sasa Azam amekuwa na muendelezo mkubwa kwanini asiende nje kwasasa hii itamfanya akawe bora zaidi lakini angalia pia umri wake huu ndio wakati mzuri kwake kufanya maamuzi haya makubwa,” alisema Morocco.