Dar es Salaam. Ingawa ushindi wa Profesa Ibrahim Lipumba katika nafasi ya uenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF) Taifa ni furaha kwake na baadhi ya makada, wanazuoni wanauona kama ni kaburi la chama hicho.
Wasiwasi wa wanazuoni hao kuhusu kupotea zaidi kwa chama hicho kilichowahi kuwa kikuu cha upinzani Tanzania, unatokana na wanachoeleza kuwa hakutakuwa na kipya chini ya uongozi wake.
Profesa Lipumba ameongoza CUF kwa miaka 25 na baada ya ushindi katika uchaguzi wa Desemba 18, 2024, ataongoza chama hicho kwa miaka 30.
Katika uchaguzi huo, mwanasiasa huyo mkongwe aliyebobea katika uchumi, alipata kura 216 akiwashinda wenzake saba. Mgombea mmoja alijitoa.
Profesa Lipumba alifuatiwa na aliyekuwa Katibu Mkuu wa chama hicho, Hamad Masoud aliyepata kura 181, huku Makamu Mwenyekiti mstaafu wa CUF (Bara), Maftah Nachuma akifuatia kwa kura 102.
Mbunge wa zamani wa Bukoba Mjini, Wilfred Lwakatare alipata kura 78, Juma Nkumbi kura sita, Athumani Kanali kura tano, Chifu Lutayosa Yemba na Nkunyuntila Chiwale walipata kura mbili kila mmoja.
Katika uchaguzi wa nafasi hiyo, zilipigwa kura 592 halali. Mwenyekiti wa kamati ya uchaguzi, Mashaka Ngole alimtangaza Profesa Lipumba kuwa mshindi.
Wakati matokeo yanatangazwa, Profesa Lipumba hakuwepo ukumbini na hata alipotafutwa azungumzie mipango yake katika awamu hii ya uongozi, simu yake haikupokewa.
Ushindi una tafsiri tofauti
Profesa Ambrose Kessy, mwanazuoni wa sayansi ya siasa amesema ushindi wa Profesa Lipumba ni tukio lenye tafsiri nyingi, si tu kwa CUF kama chama, bali pia kwa mustakabali wa siasa za vyama vingi nchini.
Kwanza, amesema inafaa kutathmini hali ya CUF katika miaka ya hivi karibuni. CUF, ambacho kilikuwa mojawapo ya vyama vya upinzani vilivyojijengea nafasi kubwa hasa katika siasa za Zanzibar, kimepoteza mvuto mkubwa tangu migogoro ya ndani ilipoibuka.
Kwa ushindi huu wa Profesa Lipumba, CUF inaendelea kuwa chama kinachoongozwa na sura ileile kwa zaidi ya miongo miwili.
“Hili linaibua maswali kadhaa ya msingi kuhusu uwezo wa chama kuleta fikra mpya au kuimarisha mvuto wake kisiasa. Katika muktadha huu, CUF ya sasa inaweza kutazamwa kama chama ambacho bado kinaendelea kupambana na athari za mpasuko wa ndani.
“Hili linawanyima nafasi ya kushindana kikamilifu na vyama vingine vya upinzani kama ACT-Wazalendo na Chadema ambavyo vinaonekana kuimarika zaidi,” amesema.
Amesema kwa ushindi huo, Profesa Lipumba anakabiliwa na changamoto kubwa za kujaribu kufufua chama ambacho kwa mtazamo wa wengi, kimepoteza mwelekeo wake wa awali.
Hata hivyo, amesema ushindi huo unatoa ishara kwamba bado kuna wafuasi ndani ya chama wanaomwamini.
“Hili linaweza kumaanisha kuwa anayo nafasi ya kujenga upya chama, lakini ni lazima achukue hatua za kimkakati, ikiwa ni pamoja na kuondokana na siasa za migawanyiko, kuvutia kizazi kipya cha wanachama na kutafuta ushirikiano wa kimkakati na vyama vingine vya upinzani.
“Bila mabadiliko haya, CUF inaweza kuendelea kuwa chama cha mkoa au kushindwa kushindana kwenye ulingo wa siasa za kitaifa,” amesema.
Ushindi wa Profesa Lipumba kwa mtazamo wa Dk Avith Mushi, mchambuzi wa masuala ya siasa kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), ni dalili ya kukosekana mbinu ya kutengeneza mrithi wa nafasi hiyo ndani ya CUF.
Amesema muda mrefu alioongoza mwanasiasa huyo haukumtosha kufanya mageuzi yoyote ndani ya chama hicho, hivyo hana kipya atakachofanya.
Dk Avith amesema haioni CUF katika mwelekeo chanya baada ya ushindi wa Profesa Lipumba, badala yake itaendelea kupoteza mwelekeo.
“Nafikiri hata hii hatua ya kuwa na kiongozi yuleyule ambaye kwa muda mrefu ameshindwa kufanya lolote la tofauti, basi kuna udhaifu ndani ya chama,” amesema.
Amefafanua udhaifu huo ni kushindwa kutengeneza viongozi watakaomrithi Profesa Lipumba, ambaye kwa mtazamo wake sasa alitakiwa abaki kuwa mshauri.
Hoja hiyo inashabihiana na iliyotolewa na mwanazuoni mwingine aliyewahi kuwa kiongozi wa juu ndani ya chama hicho, Profesa Abdallah Safari aliyesema haoni dalili ya mabadiliko kwa uongozi wa Profesa Lipumba.
“Ni kama wanaendeleza usultani, kama tunawapiga vita CCM wamekaa muda mrefu madarakani, sasa tuna uhalali wa uongozi kutobadilika? Tunaonekana wachekashaji, CUF imeshakufa,” amesema.
Kwa hatua iliyofikiwa sasa, Profesa Safari amesema hata ule mtindo wa zamani wa wafuasi wa chama hicho kupanda malori kumfuata Profesa Lipumba haupo tena akidai amepoteza mvuto.
“Kuna kipindi malori aina ya Fuso 70 yalikwenda Tanga uwanja wa Tangamano kumfuata Lipumba, sasa hivi haipo. Nasema hivi, CUF chini ya uongozi wa Lipumba haiwezi kufikia hatua ile tena, haiwezi…” amesema.
Kwa upande wake Ramadhani Manyeko, mchambuzi mwingine wa masuala ya siasa, amesema haoni CUF ikifanya vizuri chini ya uongozi huu kwa miaka mitano ijayo, hasa katika uchaguzi wa mwaka 2025.
“Naiona CUF itakayozidi kudumaa, maana hata washindani wake walikuwa watu wake wa karibu, ndiyo maana kwa muda mrefu nimekuwa nashauri hivi vyama kuweka ukomo wa uongozi. ACT-Wazalendo wameweka ukomo wa vipindi viwili,” amesema.
Amesisitiza ukomo wa uongozi katika vyama ni muhimu, akidai hakuna jipya chini ya Profesa Lipumba, licha ya ukweli kwamba amefanya mengi enzi hizo.
“Sioni kipya chini ya Profesa (Lipumba) sikatai amefanya kazi yake enzi akiwa na Maalim Seif Sharif Hamad (marehemu), lakini kwa sasa sioni jipya hata viongozi wa chini wa CUF hawaonyeshi kumuunga mkono, kwa sababu wakati wake umeshapita,” amedai.
Mmoja wa wagombea waliochuana na Profesa Lipumba katika uchaguzi huo, Nachuma amesema kulikuwa na kasoro kadhaa, hasa karatasi za kupigia kura zilizotumika akidai zilikuwa tofauti na walizokubaliana kwenye vikao vya chama.
“Nilikuwa makamu mwenyekiti, nilishiriki vikao vyote vya kuelekea uchaguzi huu, kuna mambo tulipitisha lakini yamekuwa tofauti. Tulikubaliana karatasi za kura ziwe rangi nne, lakini cha ajabu zimeletwa zingine ambazo hatukukubaliana, ambazo ukijaza peni inatokea upande wa pili,” amesema.
Amesema alipohoji kuhusu hilo, alijibiwa zilibadilishwa pasipo maelezo ya kina ya sababu ya mabadiliko hayo.
Hata hivyo, ameonyesha nia ya kukata rufaa akisema ataiwasilisha kwa mamlaka husika ili haki itendeke.
Ingawa nafasi yake ilikuwa na wagombea tisa, Profesa Lipumba alipoinuka kujinadi mbele ya wajumbe, sehemu kubwa ya wafuasi wa chama hicho waliinuka kwenda kumsikiliza.
Hilo halikushuhudiwa kwa wagombea wengine, waliishia kusikilizwa na wajumbe halli wa mkutano mkuu pekee.
Usiku mzito, nyuso zenye chovu na macho legevu yaliyolemewa na usingizi, uzilibadilika ghafla lilipotajwa jina la Profesa Lipumba kuwa mshindi wa nafasi hiyo.
Sehemu kubwa ya wajumbe walisimama kushangilia, huku wachache wakionyesha kutokuwa na furaha.
Nafasi ya makamu mwenyekiti
Kwa upande wa nafasi ya Makamu Mwenyekiti -Bara, Othman Dunga aliibuka mshindi akipata kura 182 kati ya 533 zilizopigwa.
Dunga alifuatiwa na Miraji Mtibwiliko aliyepata kura 159, Magdalena Sakaya (140), Juma Nkumbi (34), Mohamed Ngulangwa (29) na Komein Rwihura (18).
Jumla ya kura 542 zilipigwa katika uchaguzi huo, huku 533 zikiwa halali na tisa ziliharibika.
Ngole alitangaza pia matokeo ya uchaguzi wa makamu mwenyekiti- Zanzibar uliokuwa na wagombea watano.
Katika nafasi hiyo, Mbarouk Seif Salim aliyepata kura 159 ndiye aliyeibuka mshindi, huku Husna Mohamed Abdallah akifuatia kwa kura 150.
Haroub Mohamed Shamis alipata kura 117, Ali Rashid Ali (74) na Mohamed Habibu Mnyaa (56). Katika uchaguzi huo, kura saba ziliharibika kati ya 563 zilizopigwa.